Watuhumiwa kesi mauaji ya Kamanda Barlow warejeshwa rumande
Watuhumiwa
saba katika kesi ya mauaji ya aliyekuwa Kamanda wa Polisi Mkoa wa
Mwanza, Liberatus Barlow, kwa mara nyingine jana walifikishwa katika
Mahakama ya Hakimu Mkazi jijini hapa na kisha kurejeshwa rumande. Waliofikishwa
mahakamani hapo jana ni mtuhumiwa namba moja, Muganyizi Michael (36),
ambaye ni mkazi wa Nyakabungo na Magige Mwita Marwa, maarufu kama
“Tatoo” (48) mkazi wa Bugarika, jijini hapa.
Wengine ni Abdalah Petro anayefahamika pia kwa jina la “Amos Abdalah” (32), ambaye ni mkazi wa Mjimwema, Abdulrahman Ismail (28), ambaye ni mkazi wa Mkudi, jijini hapa, Chacha Wekena Mwita (50), ambaye ni mkazi wa Gongolamboto, Buganze Edward Luseta (22), ambaye ni mkazi wa Tandika na Bhokle Marwa Mwita (42), ambaye ni mkazi wa Mombasa Ukonga, jijini Dar es Salaam.
Watuhumiwa hao, ambao wengi wao walionekana kudhoofu kiafya,
walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi wa Mahakama hiyo, George Mwambapa, na
kesi yao ilitajwa tu na kisha kupangiwa tarehe nyingine ya kutajwa
tena.
Kesi hiyo, ambayo upelelezi wake ulielezwa kuwa bado haujakamilika,
imepangwa kutajwa tena Januari 24, mwaka huu, na watuhumiwa wamerejeshwa
rumande.
Kama ilivyo ada, watuhumiwa hao walifikishwa mahakamani hapo wakiwa
wamefungwa pingu wawili wawili, huku wakiwa chini ya ulinzi wa askari
polisi.
Hata hivyo, tofauti na huko nyuma, ambako watuhumiwa hao walikuwa
wakifikishwa mahakamani hapo kwa heka heka nyingi, huku wakisindikizwa
na idadi kubwa ya askari polisi wenye bunduki, jana walionekana
kusindikizwa katika chumba cha mahakama na askari watatu pekee, huku
mmoja tu ndiye alikuwa na bunduki.
Katika kesi hiyo watuhumiwa hao kwa pamoja wanadaiwa kuwa Oktoba 13,
mwaka jana, majira ya kati ya saa 7:00 na saa 8:00 usiku, katika eneo la
Minazi Mitatu Kitangiri, Wilaya ya Ilemela, jijini Mwanza, walimuua kwa
kumpiga risasi Barlow.
No comments:
Post a Comment