Monday 7 July 2014

UTAPELI JIJILA MBEYA




Mbeya.  Jiji la Mbeya kwa kushirikiana na kampuni moja inadaiwa kufanya utapeli kwa vijana zaidi ya 900 na kuvuna mamilioni ya fedha za vijana hao kwa madai ya kupatiwa mafunzo ya komputa.

Takwimu zilizopatikana hadi jana ni kwamba Jiji hilo kwa kushirikiana na Kampuni iliyojulikana kwa jina KEAR Computer Training Centre, wamejipatia kiasi cha zaidi ya Sh46 milioni kutoka kwa vijana hao.

Mbali ya vijana hao kutapeliwa, ilielezwa kwamba nao utapeli huo ulilenga pia kwenye sekondari tisa na shule za msingi 22 za Serikali jijijini hapa ambapo wanafunzi waliagizwa kutoa Sh1,000 kila mmoja kwa ajili ya picha za wanafunzi watakaoingia kwenye mpango huo.

Ofisa Elimu ya Sekondari, Lydia Herbert alikiri kuwa kwa tukio hilo akisema ndiye aliyeshiriki kuzungumza na mwenye kampuni ya Kear aliyetajwa kwa jina la Uttu Kingwande na kwamba aliahidi kuwapatia mafunzo walimu wawili wawili  kutoka kila shule.

Lydia alisema Kigwande alifika ofisi ya jiji akiwa na nyaraka zilizoonyesha kwamba aliwahi kufanya kazi Dodoma na Temeke Dar es Salaam na pia alifanya mazungumzo na viongozi mbalimbali ya jiji akiwahakikishia kutoa misaada ya kompyuta.

Wakisimulia mkasa huo kwa niaba ya wenzao wanafunzi 10,( majina yanahifadhiwa) walisema mapema  Mei mwaka huu viongozi wa Jiji wakiongozwa na Naibu Meya wa Jiji hilo, Chifoda Fungo na watendaji wa Serikali za Mitaa walifika katika Kata zote wakiwa wameambatana na mtu aliyetajwa kuwa ni  jina la Uttu Kingwande kuwa ni mkurugenzi wa Kampuni hiyo huku wakiwa  na nyaraka zote za kuitambulisha kampuni hiyo.

 “Tuliambiwa kuwa  watakaokuwa tayari watume maombi  kupitia kwa wenyeviti na watendaji wa Serikali za Mitaa kwa ajili ya kujiunga na chuo hicho ambacho kituo chake kilikuwa katika Shule ya Sekondari ya Mbeya. Na sisi tulipoona viongozi wa Serikali ndio wanaopita na kutuhamasisha kitu hicho huku wakiwa na nyaraka zote hatukuwa na shaka yoyote, tukajitokeza wanafunzi zaidi ya 900 na tulipofika pale tukaambiwa mafunzo hayo ni bure isipokuwa kila mwanafunzi atachangia Sh40,000 kwa ajili ya cheti na usajili wa kuhitimu mafunzo hayo na wote tulitoa”

Walisema wanafunzi 150 kati yao walichanga Sh70,000 zingine kila mmoja ili kupata kompyuta mpakato na baada ya hapo Mkurugenzi huyo aliondoka kwa madai kuwa anafuata kompyuta hizo lakini mpaka sasa hajarudi.

Tumesikia mhasibu wake Rehema  Ramadhani  amekamatwa hivyo tumeshtuka na tunapojaribu kufuatilia  hatuoni mwanga’’ walisema.

Akizungumza kwa  njia ya simu, Naibu Meya wa jiji hilo, Chifoda Fungo ambaye pia ni diwani wa Kata ya Uyole Kati, alikiri kuutambua mradi huo na kwamba yeye alifanya kazi kawenye kata yake pekee na haamini kwamba ni utapeli.

“Sio kweli kwamba nilizunguka kata zote, mimi nilipita kuwahamasisha wananchi wa kata yangu na baada ya kuona jambo hilo la kheri nikawahidi kuwachangia kiasi fulani cha fedha vijana watakaotoka kwenye kata yangu na si vingenevyo” alisema Fungo.

Naye Mkurugenzi wa Jiji Mussa Zungiza akiwa mkoani Tanga kikazi alikiri kuutambua mpango huo na kwamba mchakato ulivyokuja haukuonekana kuwa wa utapeli, lakini sasa hali imegeuka na kutaka kulichafua jiji.

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya, Ahmed Msangi alipoulizwa juu ya sakata hilo alikiri kumhoji ofisa wa kampuni hiyona kwamba uchunguzi unaendelea.

No comments: