Monday, 27 April 2015

Dr. Slaa: CHADEMA Tukiingia Ikulu Tutaifuta Katiba Inayopendekezwa na Kuanza Mchakato Upya



Katibu Mkuu wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Dk.  Willibrod Slaa (pichani), amesema kuwa iwapo Watanzania watakipa  ridhaa  chama hicho  ili  kushika dola  katika uchaguzi wa mwaka huu, kitu cha  kwanza watakachoanza nacho  ni kuifuta Katiba inayopendekezwa sasa na kuanzisha mchakato wa Katiba yenye maslahi ya wananchi.

Dk.  Slaa alisema hayo wakati wa mkutano wa hadhara uliofanyika mjini hapa katika viwanja vya Shule ya Msingi Kiwanja cha Ndege,  Manispaa ya Morogoro na kuudhuriwa na umati mkubwa wa watu.

Alisema Katiba iliyopendekezwa na kupigiwa debe hivi sasa na Chama cha Mapinduzi(CCM) haina maslahi yoyote kwa  wananchi wa pande zote mbili za Muungano na kwamba ipo kwa ajili  ya kunufaisha viongozi wachache, hivyo wakiingia madarakani wataifuta mara moja.

Dk. Slaa alisema kuwa Katiba ya Wananchi wa pande zote mbili ambayo inagusa maslahi yao na kutetea haki zao ni rasimu  iliyopelekwa katika Bunge Maalum iliyoandaliwa na  aliyekuwa Mwenyekiti wa tume ya mabadiliko ya Katiba, Jaji Joseph Warioba.

“Sote tunamfahamu Jaji Warioba, alikuwa Waziri Mkuu wa nchi na ndiye aliyekuwa Mwenyekiti wa Tume ya mabadiliko ya Katiba na katika tume yake alikusanya mapendekezo yenu nyinyi wananchi, lakini kwa maslahi yao hasa viongozi wa Chama cha Mapinduzi (CCM) wakatoa maoni yenu na kuweka maslahi yao ,sasa nyie tuchagueni tuingie Ikulu tuwarudishie Katiba yenu,” alisema Dk. Slaa.
 
Alisema Jaji Warioba ni mmoja wa viongozi wachache wenye uchungu na nchi hii na ndio maana wakati wa kukusanya maoni alizingatia maslahi ya wananchi wote bila kuangalia rangi, kabila pamoja na itikadi ya vyama vya siasa.

Dk. Slaa alisema kuwa katika mchakato watakaounzisha endapo watapewa dola na Watanzania ni kuunganisha mapendekezo yote ya wananchi waliyotoa katika iliyokuwa tume ya Jaji Warioba ukiwamo muundo wa Serikali tatu ambao unakatiliwa na Serikali ya CCM.

No comments: