Thursday, 30 April 2015

Madaktari bingwa 16 wa upasuaji wa moyo kutoka nchini AUSTRALIA wamewafanyia upasuaji wa moyo Watoto 15 hospitali ya Bugando


Madaktari bingwa kumi na sita wa upasuaji wa moyo kutoka nchini AUSTRALIA wameshirikiana na madaktari bingwa wawili wa hospitali ya rufaa BUGANDO kufanya upasuaji mkubwa wa moyo kwa watoto 15 waliokosa gharama za kupelekwa nje ya nchi kutokana na gharama kubwa za operesheni ya moyo.
Sehemu ya gharama za upasuaji huo zimetolewa na hospitali ya rufaa BUGANDO huku wazazi wa watoto hao wakichangia shilingi laki moja kama gharama ya vifaa, huku hospitali hiyo ikitumia zaidi ya shilingi milioni sabini na tano kugharimia gharama za upasuaji kwa watoto hao wanaotokea katika familia maskini zenye kipato duni. Iwapo watoto hao wangepelekwa india kwa ajili ya kufanyiwa upasuaji wa moyo kila mmoja angetakiwa kulipia shilingi milioni 20.
 
Hawa ni madaktari bingwa pamoja na wasaidizi wao wakiwa katika chumba cha upasuaji wa moyo cha hospitali ya rufaa bugando ambapo ndani ya chumba hiki kazi inayoendelea ni ya kumfanyia upasuaji wa moyo mtoto Janeth Enock mwenye umri wa miaka 10 – na kwa mujibu wa daktari bingwa wa moyo Dk. Godwin Godfrey Shalau upasuaji huo umechukua saa 5.30 kukamilika kwa mafanikio makubwa.
 
Mkurugenzi mkuu wa hospitali ya rufaa Bugando Prof. Dk. Kien Mteta anasema kwamba operesheni kubwa za moyo hapa nchini ni za gharama kubwa, lakini kwa kutambua kuwa thamani ya maisha ya binadamu ni zaidi ya kitu chochote, ndiyo maana hospitali hiyo licha ya kukabiliwa na changamoto ya upungufu wa madaktari bingwa wa upasuaji wa moyo, vifaa tiba na dawa pamoja na vyumba maalumu vya upasuaji, imejitolea kufadhili gharama za upasuaji kwa watoto hao 15 wasio na uwezo.

No comments: