Friday, 24 April 2015

MTWARA YAPATA MKAKATI WA MAWASILIANO WA KUKABILIANA NA MAAFA

Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu shughuli za Maafa ofisi ya Waziri Mkuu, Brig.Jen. Mubazi Msuya (wa pili kulia) akifuatilia majadiliano wakati wa uwasilishaji wa Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara tarehe 23 Aprili, 2015, kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Mkoani Mtwara, Bw. Johansen Bukwari.
Baadhi ya washiriki wa warsha ya uwasilishaji wa Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara wakifuatilia uwasilishwaji wa mkakati huo, uliofanywa na Ofisi ya Waziri Mkuu, Idara ya Uratibu wa Shughuli za Maafa mkoani Mtwara tarehe 23 Aprili, 2015.
Mkurugenzi wa Idara ya Uratibu shughuli za Maafa ofisi ya Waziri Mkuu, Brig.Jen. Mubazi Msuya (Walio kaa wa pili kushoto) akiwa na washiriki wa warsha ya Kuwasilisha Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara mara baada ya kuwasilisha mkakati huo tarehe 23 Aprili, 2015, wa kwanza kulia kwake ni Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Mkoani Mtwara, Bw. Johansen Bukwari.
Ofisi ya waziri Mkuu kupitia Idara ya Uratibu wa Shughuli za maafa imewasilisha Mkakati wa Mawasiliano wa kukabiliana na maafa kwa mkoa wa Mtwara. Mkakati huo umetayarishwa kwa ajili ya kuhakikisha kwamba kunakuwa na Mtiririko unaoeleweka wa taarifa za tahadhari kabla ya maafa, wakati wa maafa na baada ya maafa kutokea.
Mkakati huo umezingatia majanga ambayo yamekuwa yakitokea mara kwa mara na kusababisha madhara makubwa mkoani Mtwara. Majanga hayo ni; Ukame, mafuriko na mlipuko wa kipindupindu.
Akizungumza wakati wa warsha ya kuwasilisha mkakati huo maafa mkoani Mtwara tarehe 23 Aprili, 2015, Katibu Tawala Msaidizi (Uchumi na Uzalishaji) Mkoani Mtwara, Bw. Johansen Bukwari alifafanu kuwa mkakati huo utaongeza nguvu ya jamii kuwa na utayari wa kukabiliana na majanga yanayowakabili ili kuokoa maisha na mali zao.
Bukwari, "Halmashauri za Mtwara Mikindani na Vijijini zimekuwa na tatizo la kukumbwa na mafuriko, ukame na magonjwa ya mlipuko mara kwa mara kutokana na mabadiliko ya tabia nchi, ujenzi katika maeneo hatarishi pamoja na miundombinu duni, kupitia mkakati huu kila mmoja wetu kwa kuzingatia nafasi aliyonayo ataweza kutekeleza wajibu wake kwa ufanisi."
Awali akimkaribisha Katibu Tawala katika warsha hiyo, Mkurugenzi Idara ya Uratibu wa shughuli za Maafa, Ofisi ya Waziri Mkuu, Brig.Jen.
Mubazi Msuya alieleza kuwa uwepo wa mkakati huo mkoani Mtwara unawezesha ufanisi wa hatua zilizokuwa zinachukuliwa na serikali mkoani humo za kukabiliana na maafa.
"Serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali za kuhakikisha madhara yaliyotokea mkoani Mtwara hayajirudii ikiwa ni pamoja na kutoa elimu kuhusu athari za ujenzi na kuendesha shughuli za uchumi katika maeneo hatarishi, umuhimu wa usafi wa mazingira matumizi ya mbegu zinazostahimili ukame pamoja na kuzuia ujenzi katika maeneo hatarishi" alisema Msuya.
Ofisi ya Waziri Mkuu kupitia Ufadhili wa Shirika la Kuhudumia Watoto la Umoja wa Mataifa (UNICEF), imeweza kuandaa mpango huo unaolenga kuboresha menejimenti ya maafa katika ngazi ya mikoa nchini

No comments: