Rais wa Chama cha Walimu Tanzania Gratian Mukoba.
UCHAGUZI wa Chama Cha Walimu Tanzania (CWT) mkoa wa Simiyu uliofanyika jana, nusura uvunjike baada ya baadhi ya wagombea, kuanza kutuhumiana ndani ya ukumbi wakati wakijieleza kwa wajumbe.
Mmoja wa wagombea hao ambaye alikuwa akigombea nafasi ya Uwakilishi wa Kamati Tendaji Taifa, Chananja Buluba alipopewa nafasi ya kujieleza, alidai kuwa uchaguzi huo umegubikwa na vitendo vya rushwa.
Alidai kuna baadhi ya wajumbe walipewa Sh 50,000 hadi Sh 100,000 kutoka kwa wagombea wa nafasi za Uwakilishi wa Kamati Tendaji Taifa, Mwenyekiti na Mweka Hazina.
Akiwa anazomewa na baadhi ya wajumbe hao, mgombea huyo alieleza kuwa mbali na kupewa fedha, baadhi ya wajumbe walilipiwa sehemu za kulala kwa siku tatu pamoja na chakula.
Hali hiyo ilionekana kuwakera wajumbe wa uchaguzi huo na kumtaka athibitishe mbele yao na kuwataja watu ambao walipewa pesa, kulipiwa sehemu za kulala pamoja na chakula.
Akiwa tayari kutaka kuwataja wahusika wa vitendo hivyo, mgombea huyo alizuiliwa na Mratibu wa Uchaguzi huo ambaye ni Katibu wa CWT mkoani hapa, Fatuma Bakari kwa madai kuwa alikuwa amekiuka taratibu za uchaguzi.
Kitendo cha kuzuiliwa na katibu huyo, kilionekana kumkera mgombea huyo na kuacha kujieleza mbele za wajumbe hao, ambapo aliamua kuwaita waandishi wa habari nje ya ukumbi wa mkutano ili kuwaeleza hali hiyo.
" Nimechukia sana kitendo cha Mratibu ambaye ni Katibu CWT Mkoa kunizuia...hali ya uchaguzi huu imechafuliwa sana na rushwa, wagombea wamegawa pesa kama karanga na sijui wametoa wapi wakati wao ni walimu kama mimi," alisema Buluba.
Alibainisha kuwa pesa walizokuwa wakizitoa wagombea hao, zilikuwa na ufadhili kutoka katika vyama vikubwa vya siasa, alivyovitaja.
Alisisitiza kuwa hakuna mwalimu ambaye anaweza kumpatia mwalimu mwenzake, kiwango hicho kikubwa cha pesa. " Nina muda mrefu katika taaluma hii ya walimu...hizi pesa ni nyingi, wajumbe wote walipewa pesa hasa nafasi hizo za juu...watu wanalipiwa sehemu za kulala, chakula bure kwa siku tatu...tuligundua kuna ufadhili mkubwa wa vyama," alisema.
Hata hivyo, licha ya baadhi ya wajumbe kupewa kiasi hicho, alibainisha kuwepo kwa baadhi ya wagombea waliojitoa kugombea nafasi mbalimbali baada ya kupewa Sh 500,000. Buluba aliitaka Takukuru kuchunguza hali hiyo, kabla hajachukua maamuzi mengine, huku akitishia kuachana na chama hicho na kuanzisha chama kingine mbadala wa CWT.
" Najipanga kuanzisha mbadala wa CWT kwa sababu chama hiki ni rushwa kila sehemu kila mara.. CWT ya sasa imeshindwa kuwatetea walimu na badala yake kimegeuka kuwa chama cha kisiasa," alisema.
Katibu wa chama hicho ambaye ndiye alikuwa Mratibu wa uchaguzi huo, Fatuma Bakari alikiri kupata taarifa za kuwepo kwa vitendo hivyo, huku akidai kuwa hakuna mtu ambaye ametajwa kufanya vitendo hivyo.
" Taarifa hata sisi tumepewa kuwepo kwa vitendo hivyo, ndiyo maana kwenye uchaguzi nimemzuia mgombea huyo kuwataja wahusika kwa sababu kanuni za uchaguzi zinakataza, lakini ningeliruhusu kikao kilikuwa kinavunjika kutokana na hali niliyoiona," alisema Bakari.
Uchaguzi huo ulifanyika na Dwese Kulwa alichaguliwa kuwa Mwenyekiti kwa kura 52. Mweka Hazina ni Joyce Nkomangwa aliyepata kura 45 na Mwakilishi wa Kamati Tendaji Taifa ni Julius Mategemeo, aliyepata kura 50.CHANZO:HABARI LEO
No comments:
Post a Comment