Thursday, 30 April 2015

Vyama vinavyounda UKAWA vyatoa msimamo juu ya njama za kuahirisha uchaguzi mkuu mwaka huu.


 Vyama vinavyounda umoja wa katiba ya wananchi UKAWA vimetoa msimamo wao juu ya njama za kuahirisha uchaguzi mkuu unaotakiwa kufanyika OCTOBA mwaka huu na kwamba hawako tayari serikali iliyopo madarakani iongezewe muda,huku ukiitaka tume kutoka hadharani na mpango maalum na ratiba  nzima ya maandalizi ya uchaguzi mkuu badala ya kuishia kusema kuwa uchaguzi uko pale pale.
Akielezea msimamo huo jijini dar es salaam mwenyekiti wa NCCR-MAGEUZI Mh. James Mbatia amesema endapo tume ya uchaguzi itaendelea na utaratibu uliotumika mkoani njombe itatumia zaidi ya miaka 10 kuandikisha na kuongeza kuwa kwa sasa suala la kura ya maoni liwekwe pembeni na serikali isitishe mambo yote yasiyokuwa ya msingi ielekeze nguvu zake kwenye zoezi la uboreshaji wa daftari la wapiga kura ili limalizike kwa wakati.
 
Kwa upande wake mwenyekiti wa chadema Mh Freeman Mbowe amesema hakuna mgawanyiko ndani ya ukawa licha ya kuwepo kwa changamoto za hapa na pale na kwamba tayari wameshafanya mgawanyo wa majimbo kwa asilimia 95 ambayo wamekubaliana isipokuwa majimbo 12 ambayo bado wanavutana lakini bado wako kwenye masahauriano.
 
Mwenyekiti wa CUF Prof. Ibrahimu Lipumba amesisitiza kuwa UKAWA haiungi mkono jaribio lolote la kufanya marekebisho ya katiba ya sasa kwa lengo la kuongeza muda wa utawala uliopo madarakani kwani kwa kufanya hivyo ni kwenda kinyume na katiba ya nchi na ukiukwaji wa sheria  huku akiitadharisha serikali kutokuipeleka nchi kwenye machafuko yanayotokea burundi hivi sasa.

No comments: