Mwalwisi akisaini mkataba
KOCHA
mkuu msaidizi wa zamani wa Mbeya City, Maka Mwalwisi ametua katika
klabu ya Kimondo baada ya leo kusaini mkataba wa miaka miwili kuitumikia
klabu hiyo inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara (FDL).
Mkurugenzi wa Kimondo FC, Elick Ambakisye, ndiye aliyemsainisha kocha
huyo mkataba leo mbele ya waandishi wa habari jijini hapa na kueleza
kuwa Mwalwisi ana uwezo mkubwa wa kufundisha mpira baada ya kujiridhisha
na kiwango chake akiwa na klabu za City na Panone FC ya Kilimanjaro
Naye Mwalwisi amesema amechukua uamuzi wa kutua katika klabu hiyo ya
Mbozi ili kuisaidia kufanya vizuri FDL na kupanda Ligi Kuu msimu ujao.
"Nilikuwa na mkataba wa mwaka mmoja na Panone FC ambao umemalizika na
ndiyo maana nimesaini mkataba mpya leo. Nimefurahi kujiunga na Kimondo
FC maana ni timu ya nyumbani," amesema Mwalwisi na kuongeza:
"Nina uhakika tutapanda Ligi Kuu ikiwa wachezaji na uongozi tutatimiza
majukumu yetu ipasavyo na kushirikiana kwa kila jambo muhimu kwa timu."
Mwalwisi alikuwa msaidizi wa kocha mkuu wa Mbeya City msimu wa 2013/14
wa Ligi Kuu Tanzania Bara walipomaliza nafasi ya tatu kwenye msimamo wa
ligi hiyo nyuma ya Yanga na Azam FC.
Msimu uliopita alijiunga na Panone FC iliyoshiriki FDL, lakini
haikufanikiwa kupanda Ligi Kuu. Timu za Majimaji ya Songea, African
Sports ya Tanga, Mwadui FC ya Shinyanga na Toto Africans ya Mwanza
zilipanda Ligi Kuu.
No comments:
Post a Comment