SIKU moja baada ya jeshi la polisi kuwaaga kwa heshima za kijeshi askari wake wawili kati ya wanne waliouawa wakiwa kazini katika kituo cha Stakishari, Ukonga, Dar es Salaam, jeshi hilo limeongeza nguvu katika operesheni kwa kujumuisha mikoa ya jirani.
Mikoa hiyo ni pamoja na Pwani na Tanga pamoja na mikoa mingine iliyo
karibu ili kuhakikisha wahalifu waliofanya kitendo hicho cha kinyama
wanapatikana.
Kauli hiyo imetolewa na Kamanda wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam,
Kamishna Suleiman Kova wakati akizungumza na waandishi wa habari jana
jijini Dar es Salaam.
Kamishna Kova alisema hatua hiyo inatokana na kuhakikisha kuwa
wahalifu hao waliofanya mauaji hayo ya askari wanne na raia watatu
wanapatikana na sheria kuchukua mkondo wake.
Alisema tukio hilo lina viashiria vya ugaidi, hivyo jeshi hilo halitafumba macho kwani matukio kama hayo yamekuwa yakijirudia.
“Polisi wamekuwa wakiuawa bila hatia yoyote, lakini hii inatokana na
ukaribu uliopo katio ya polisi na raia, hivyo majambazi kutumia mwanya
huu kufanya uhalifu ambao si wa kuiba fedha bali kutoa roho za watu na
kuiba silaha,” alisema Kova.
Alisema hatua ya kufanya operesheni katika mikoa ya jirani ni
kuhakikisha kuwa wahalifu hao hawakimbilii katika mikoa ya jirani,
ambapo pia alisema mikoa mingine iliyoguswa na tukio hilo nayo imejiunga
katika operesheni hiyo.
Alisema pia kuanzia sasa wameamua kuimarisha ulinzi kwenye vituo vya
polisi hivyo kuwataka wananchi kutokuwa na wasiwasi watakapokutana na
hali tofauti katika vituo vya polisi.
Aidha, Kova aliwapongeza wananchi kwa ushirikiano waliouonesha
wakisisitiza kuwa ushirikiano huo unaleta moyo na kufanya wazidi
kuwatumikia zaidi, ambapo pia alisema michango kwa ajili ya familia za
maofisa wa polisi waliouawa imefikia Sh milioni 8.5.
No comments:
Post a Comment