Tuesday 22 December 2015

IRINGA,WANAFUNZI 153211 KUJIUNGA KIDATO CHA KWANZA 2016

Ufaulu wa wanafunzi waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi (PSLE) mwaka 2015 mkoani Iringa umeongezeka ukilinganisha na mwaka jana, ambapo ufaulu kwa mwaka huu ni asilimia 73.25, wakati mwaka jana ulikuwa ni asilimia 68.58, sawa na ongezeko la asimilia 4.67.

Hayo yalisemwa na Afisa Elimu Taaluma wa Mkoa wa Iringa, Euzebio Mtavangu hivi karibuni wakati akitoa taarifa ya mwelekeo wa matokeo ya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi 2015 kwa wajumbe wa kamati ya uchaguzi wa mkoa wa kuchagua wanafunzi wataojiunga kidato cha kwanza mwaka 2016.

Alisema kuwa kuongezeka kwa ufaulu mwaka huu mkoani Iringa ni kutokana na utekelezaji mzuri wa mpango wa matokeo makubwa sasa (BRN) ulioanzisha na serikali hivi karibuni.

Alisema kuwa wanafunzi waliofaulu mwaka 2015 ni 15,311 (7,163 wavulana na 8,148 wasichana) ambapo wanafunzi wote waliofaulu mwaka huu wamechaguliwa kujiunga na kidato cha kwanza mwaka 2016.

Katika mwaka 2014 matokeo ya watahiniwa waliofaulu mtihani wa kumaliza elimu ya msingi walikuwa ni wanafunzi 14,650 (6,835 wavulana na 7,815 wasichana).

Mtavangu aliongeza kuwa kwa mwaka 2015 wanafunzi 413 (258 wavulana na 155 wasichana) ambao ni asilimia mbili hawakufanya mtihani wakilinganishwa na 177 (109 wavulana na 68 wasichana) ikiwa ni asilimia moja kwa mwaka 2014.

“Sababu za wasiofanya mtihani ni utoro, vifo, ugonjwa, mimba na kuhama. Idadi ya utoro kwa wanafunzi mwaka huu ni kubwa ukilinganisha na mwaka jana, ambapo mwaka 2015 utoro ulikuwa ni wanafunzi 399 wakati mwaka 2014 utoro kwa wanafunzi ulikuwa ni 158,” alisema.

Mtihani wa kumaliza elimu ya msingi ulifanyika tarehe 09-10 Septemba 2015 nchini kote.

Aidha, alisema kuwa shule za msingi 467 kati ya shule 491 ndio zilizokuwa na watahiniwa wa mtihani wa kumaliza elimu ya msingi kwa mwaka 2015 mkoani Iringa.

Mtavangu alisema kuwa watahiniwa waliofanya mtihani na kumaliza elimu ya msingi 2015 wanaendelea kujibu maswali ya mitihani kwa kutumia fomu za ‘Optical Mark Reader’ (OMR).

Alisema kuwa matumizi ya fomu za OMR yalianza mwaka 2012 na lengo la kutumia OMR ni kusoma moja kwa moja kwa kompyuta majibu ya mtahiniwa kutoka katika karatasi yake ya majibu na kuokoa muda wa usahihishaji.

Takwimu za watahiniwa waliofanya mtihani wa kumaliza elimu ya msingi mwaka 2015 ni wanafunzi 20,905 (9,612 wavulana na 11,293 wasichana) na waliofaulu ni jumla ya wanafunzi 15,311 (7163 wavulana na 8148 wasichana), sawa na asilimia 73.25.

Hata hivyo, kiwango cha kumaliza elimu ya msingi (completion rate) mkoani Iringa kimeongezeka kutoka asilimia 77.2 (2014) hadi kufikia asilimia 81.1 (2015).

Mwenyekiti wa Kamati ya Uchaguzi wa Mkoa ya kuchagua wanafunzi wataojiunga kidato cha kwanza mwaka 2016 alikuwa ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Iringa (RAS), Ayubu Wamoja.(P.T)

No comments: