Ilidaiwa kuwa mwalimu huyo alifanya uamuzi huo wa kujitosa majini alipokuwa safarini akitokea eneo la Kinesi kwenda Musoma mjini kwa kutumia usafiri wa kivuko.
Akithibitisha kutokea kwa tukio hilo, Kaimu Kamanda wa Polisi Tarime Rorya, Sweetbert Njewike alisema kuwa tukio hilo la mwalimu Zachma kujitosa ziwani lilitokea Juni 24 mwaka huu majira ya mchana wakati mwalimu huyo akisafiri kwa kutumia kivuko kutoka Kinesi kwenda Musoma mjini.
“Kuna tukio la mwalimu mmoja wa shule ya msingi Kibumaye aliyejulikana kwa jina la Nelson Zachma (50) kujitosa majini, na tukio hili lilitokea Juni 24 mwaka huu majira ya mchana wakati akisafiri kuelekea Musoma mjini akitokea eneo la Kinesi,” alisema Njewike.
Alisema mara baada ya kujitosa majini, juhudi za uokoaji zilifanywa na wapiga mbizi wa kivuko hicho lakini hazikuzaa matunda ndipo marehemu alipozama ndani ya maji na mwili wake kuopolewa siku tatu baadaye yaani Juni 30 katika mtaa wa Rebu Tarime.
Alisema sababu za mwalimu huyo kuchukua uamuzi wa kujitosa majini hazijajulikana na polisi bado wanaendelea na uchunguzi wa tukio hilo ili kubaini nini chanzo cha mwalimu huyo kuamua kujiua.
Mmoja wa mashuhuda wa tukio hilo aliyejulikana kwa jina la Lucia Kibacho (40) alisema kuwa walipofika katikati ya kivuko, Zachma alimpatia namba za simu za ndugu zake na kumwomba awapatie taarifa zake na ndipo akajirusha ndani ya maji.
“Mimi nilikuwa nimekaa karibu naye, tulipofika katikati ya ziwa, akaniambia chukua hizi namba ni za ndugu zangu uwajulishe kuwa mimi nimejitosa majini na nimekufa, mara akajirusha majini,” alisema Kibacho.
Lakini taarifa za awali zinaonesha kuwa, baadhi ya waombolezaji waliokuwa nyumbani kwa marehemu walisikika wakisema kuwa Zachma alikuwa na mgogoro wa ndani na mke wake na huenda ikawa ni moja ya sababu za yeye kuchukua uamuzi huo.[HABARI LEO]
No comments:
Post a Comment