Friday 5 February 2016

Waasi Wa Burundi Wakimbilia Nchini Kushawishi Watanzania Wajiunge Na Vikundi Vya Waasi


BAADHI ya askari waasi wa Burundi, wamebainika kukimbilia nchini na kuanza kushawishi vijana wajisajili ili wajiunge na vikundi vya waasi.

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa alisema hayo jana alipokuwa akifunga Mkutano wa Pili wa Bunge mjini Dodoma jana na kuwataka wakimbizi na wananchi, kushirikiana na vyombo vya usalama, kutoa taarifa za uhalifu.

“Kutokana na ujio wa wimbi kubwa la wakimbizi kutoka Burundi, kumejitokeza matukio ya uhalifu wa kutumia silaha za moto ndani na nje ya kambi ya wakimbizi ya Nyarugusu.“ 

"Aidha, kutokana na upekuzi na ukaguzi kwa wakimbizi unaofanywa kwa pamoja na vyombo vya dola sanjari na taarifa za ki-intelijensia, imebainika kuwepo kwa askari waasi waliokimbia pamoja na raia wa kawaida, ambao wanajaribu kuwashawishi vijana kujisajili ili kujiunga na vikundi vya waasi,”alisema Majaliwa.

Pamoja na changamoto hiyo, ambapo kambi za wakimbizi zilizoko mikoa ya Kigoma, Katavi, Tabora na Tanga zinahifadhi wakimbizi wapatao 218,895 kutoka mataifa ya Burundi (156,377), Congo-DRC (62,176), Somalia (150) na mataifa mchanganyiko (192) ikiwemo Rwanda, Uganda, Sudan Kusini na Ethiopia, hali usalama katika nchi kwa ujumla ni shwari.

Akizungumzia kuimarisha maadili na utendaji serikalini, Majaliwa alisema Serikali imedhamiria kurejesha nidhamu na maadili ya watendaji wa Serikali na watumishi wa umma katika kutoa huduma mbalimbali kwa wananchi.

“Katika kuhakikisha watumishi wa umma na Watanzania wote wanafanya kazi, Mheshimiwa Dk John Pombe Magufuli, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania amekuja na kauli mbiu ya Hapa Kazi Tu.

 “Tafsiri ya falsafa hii ni kuwataka Watanzania wote katika nafasi mbalimbali walizopo, kufanya kazi kwa bidii na kujiepusha na vitendo vya uzembe, urasimu na kutenda kazi kwa mazoea,” alisema.

Alimtaka kila mwananchi, kuwa na nidhamu ya kazi na kuhakikisha anafikia malengo yaliyowekwa na kuwakumbusha watumishi wa umma kuwa, wamepewa dhamana ya kuwahudumia wananchi kwa niaba ya Serikali.

Kwa kuzingatia wajibu huo, amewataka watumishi hao kuhakikisha wanawahudumia wananchi kwa haki, weledi, uadilifu na kwa taaluma zao na kuhakikisha kuwa wanatatua kero za wananchi.

Waziri Mkuu alisema wanatambua kuwa wapo watumishi wanaotekeleza vyema majukumu yao, lakini pia wapo watumishi ambao hawazingatii maadili ya kazi zao na pia wanafanya kazi kwa uzembe.

“Serikali haitaacha kuchukua hatua za nidhamu kwa watumishi wote wasiozingatia kikamilifu sheria, kanuni na taratibu katika utumishi wa Umma. 

"Aidha, kwa kuzingatia maelekezo ya Mheshimiwa Rais, viongozi na watumishi wote wa umma lazima tufanye kazi kwa kuzingatia weledi na kujiamini. Kila mtu anapaswa kujitathmini kama dhamana aliyopewa anaitendea haki,” alisema.

Kuhusu dhana ya kutumbua majipu, Majaliwa alisema Rais ametumia dhana hiyo kusimamia uwajibikaji, hasa kwa wale wenye dalili ya kukosa maadili ya utumishi wa umma.

No comments: