Monday 20 April 2015

MOYO ATIMULIWA CCM ZANZIBAR


Chama cha Mapinduzi Zanzibar (CCM) kimemfukuza uanachama Mwanasiasa Mkongwe Hassan Nassor Moyo baada ya kubainika amekuwa akifanya vitendo vinavyokwenda kinyume na maadili ya chama ikiwamo kuhutubia mikutano ya hadhara inayoitishwa na Chama cha Wananchi (CUF) na kukejeli misingi ya Mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar imefahamika visiwani humo jana.
Uamuzi wa kumfukuza mwanasiasa huyo ulifikiwa jana na Kikao cha Halimashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Magharibi kilichofanyika katika Tawi la CCM Mbweni chini ya Mwenyekiti wa CCM mkoa huo, Yussuf Mohamed Yussuf ambapo wajumbe wote waliunga mkono ajenda ya moyo kufukuzwa uanachama wake.
Akizungumza na Mwananchi Katibu wa CCM mkoa wa Magharibi, Azziza Mapuri alisema kwamba hatua hiyo imefikiwa baada ya kikao kujiridhisha kuwa Mzee Moyo alikuwa akifanya vitendo vinavyokwenda kinyune na miiko na maadili ya chama.
Mapuri alisema kwamba uchunguzi uliyofanywa kuanzia ngazi ya Tawi Fuoni, Jimbo, Wilaya hadi Mkoa ripoti zote zimeonyesha Moyo alikuwa akivunja miiko na maadili ya chama kutokana na kitendo chake cha kuhudhuria mikutano ya CUF na kupanda katika majukwaa na kukejeli misingi ya mapinduzi na Muungano wa Tanganyika na Zanzibar.
"Kwa kutumia Ibara ya 93 (14) ya Katiba ya CCM Mzee Moyo tumemfukuza uanachama wa CCM baada ya kikao kupitia ripoti zote za uchunguzi na kujiridhisha alikuwa akivunja maadili na miiko ya chama chake," alisema Mapuri.
Alisema kwamba katiba ya CCM imeweka miongozo, maadili na kanuni na kila mwanachama wake anatakiwa kuheshimu, lakini Mzee Moyo ameshindwa kuheshimu na kufikia kukosoa chama hadharani badala ya kutumia taratibu za vikao vya chama.
Alisema kutokana na nguvu za kikatiba walizopewa Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya mkoa kupitia kifungu cha 93 (14) cha katiba ya CCM, Mzee Moyo amefukuzwa bila ya kuhitaji baraka za wazee wa chama kwa vile ni utekelezaji wa katiba.
Hata hivyo alisema kwamba kama Mzee Moyo atakuwa hakuridhika na uamuzi huo bado ana haki ya kukata rufaa katika vikao vya ngazi ya juu, lakini alisema kulingana na ushaidi waliokusanya Moyo hawezi kushinda sehemu yoyote hata kama akiamua kukimbilia mahakamani.
Akizungumza na Mwananchi jana Moyo alisema kwamba ameshangazwa na uamuzi huo, hata hivyo hafikirii kukata rufaa kwa sababu haoni sababu za msingi za kuendelea kubakia ndani ya CCM wakati wameonyesha hawamtaki.
Moyo alisema kwamba yeye ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ndiyo maana amekuwa akifanya kazi ya kulinda misingi ya Serikali ya Umoja wa Kitaifa (SUK) kwa kuwakumbusha viongozi na wananchi umuhimu wa kuwepo kwa serikali ya pamoja kupitia mikutano ya hadhara na makongamano.
"Sina mpango wa kukata rufaa sioni umuhimu wa kubakia CCM kama wenyewe hawanitaki na wala sina nia ya kukata rufaa, " alisema Moyo.
Hata hivyo alisema yupo safarini nje ya Zanzibar lakini hadi jana alikuwa bado hajapokea rasmi barua ya kufukuzwa uanachama wake.CHANZO MWANANCHI

No comments: