RAIS John Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho ya sherehe ya Siku ya Wafanyakazi Duniani maarufu Mei Mosi ambayo kitaifa yatafanyika mkoani Dodoma.
Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Tanzania (TUCTA), Nicholas Mgaya alisema Tucta waliwasilisha maombi rasmi ya kumuomba Rais Magufuli kuwa mgeni rasmi kwenye maadhimisho hayo na tayari wamepata taarifa rasmi kutoka Ofisi ya Waziri Mkuu kuwa Rais amekubali kuwa mgeni rasmi.
Mgaya alisema hayo jana mjini Dodoma wakati wa mkutano baina ya Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana na timu ya maandalizi ya sherehe za Mei Mosi Kitaifa, ambao mkutano huo ulikuwa na lengo la kujadili na kuendelea kuweka mipango na maandalizi ya kufanikisha sherehe za mwaka huu kwa mafanikio makubwa.
Alisema ili kufanikisha sherehe za Mei Mosi, Tucta Makao makuu watachangia nusu ya gharama zote za sherehe nzima na nusu inayobaki itachangiwa na wadau mbalimbali wakiwemo waajiri ambapo kwa mujibu wa Kamati ya Maandalizi Bajeti nzima ya sherehe ya mwaka huu ni Sh milioni 29.6.
Kwa upande wake, Mkuu wa Mkoa Rugimbana aliishukuru Tucta na Serikali kwa ujumla kwa kuupa Mkoa wa Dodoma ambao ni Makao Makuu ya Nchi heshima ya kipekee ya kuwa mwenyeji wa maadhimisho ya sherehe ya Sikukuu ya Mei Mosi Kitaifa mwaka huu.
Naye Katibu wa Tucta Mkoa wa Dodoma, Ramadhani Mwendwa alisema tayari wameunda kamati ya maandalizi ya sherehe na jukumu kubwa lililoko mbele ni kutafuta fedha na michango kutoka kwa wadau, wengi wao wakiwa ni waajiri serikalini.
No comments:
Post a Comment