Thursday, 22 December 2016

TAMKO LA PAMOJA KULAANI KITENDO CHA KUWEKWA KIZUIZINI MWANDISHI WA HABARI WA KITUO CHA ITV KHALFAN LIUNDI MKOANI ARUSHA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Baraza la Habari Tanzania (MCT) pamoja na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) , tumesikitishwa na vitendo vinavyoendelea nchini,   chini ya uratibu  wa baadhi ya viongozi wa serikali za Mitaa ( hasa Wakuu wa Wilaya) vya kutaka kunyamazisha ama kuzuia kabisa waandishi wasifanye kazi zao kwa uhuru.  Matukio kadhaa yanaonyesha kuwa uhuru wa waandishi wa habari kutafuta na kutoa habari umezidi kubinywa na kujenga hofu miongoni mwa wanahabari kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa toka viongozi wapya waingie madarakani.

Mwandishi wa habari wa kituo cha Televisheni (ITV), Bwana Khalfan Liundi ameendelea kushikiliwa na Polisi Wilayani Arumeru kwa amri ya Mkuu wa Wilaya hiyo Alexander Mnyeti toka tarehe 21/12/2016 hadi hivi sasa tunapotoa tamko hili bila kifikishwa mahakamani. Taarifa za awali kutoka Arusha zinaonyesha kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru hakupendezwa na taarifa iliyorushwa na ITV tarehe 20/12/2016 na kuonyesha wananchi waliokuwa wakiandamana kudai haki yao ya kupata maji. Kwa mujibu wa wandishi wa habari mkoani Arusha mwandishi huyu amekamatwa kwa kutoa taarifa hiyo ya maji ambayo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya inaonekana kuwa ni ya kichochezi.

Matukio ya viongozi wa Serikali za Mitaa hasa Wakuu wa Wilaya kutishia na kutoa amri waandishi kuwekwa kuzuizini wanapotoa taarifa toka maeneo yao ya kazi yamefikia zaidi ya matano toka January 2016.  Kwa mujibu wa Sheria ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya ya mwaka 1962 na Sheria ya Serikali za Mitaa zilizokuwa pia zinaumika kipindi cha mkoloni Mkuu wa Wilaya au Mkoa ana mamlaka ya kuamrisha polisi kumweka mtu yoyote kuzuizini na kumlaza rumande na kesho yake kumwachia bila mashtaka yoyote. Yafuatayo ni baadhi ya Matukio ya kutiwa kizuizini kwa waandishi wa habari kwa amri za wakuu wa wilaya;

i) Tabora Igunga mwandishi wa Chanel Ten Jumbe ismail aliswekwa rumande kwa masaa na kwakosa la kurupoti maandamano ya wananchi
ii) Mwandishi wa ITV Kanda ya ziwa Cosmas Makongo alikamatwa tarehe  8/10/2016 kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera, Shaaban Lissu (Mwanahabari mwenzake) baada ya kuripoti janga la njaa iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa wilaya hiyo, na baada ya hapo alitakiwa kukanusha habari aliyoiripoti na ndiyo akawekwa lumande kwa takribani saa 2 kabla ya kuachiwa.
iii) Mwandishi wa Radio Free Africa na Gazeti la Mwananchi, Baraka Tiluzilamsomi ambaye alikamatwa 6th /4/2016 na kuwekwa mahabusu kwa saa 7 baada ya amri ya mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe, aliyedai mwandishi huyo aliingia eneo la hospitali ya wilaya ya Chato bila kupata kibali kutoka kwake.
iv) Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, aliwakamata waandishi wa habari wa kituo cha Radio Ebony FM cha mjini Iringa na kuwaachia tarehe 1/4/2016 siku baada ya kuwafikisha kituoni.
v) Mkuu wa Wialya ya Kibaha, Assumpter Mshama, alitumia mamlaka yake tarehe 29/11/2016 kumwita mwandishi wa Mwananchi Sanjto Msafiri mbele ya mkutano na kumsuta na huku akimtaka akanushe habari ambayo aliitoa mbele ya wafanyabiashara. Mkuu wa Wilaya alidai taarifa alizotoa mwandishi ni za kumchonganisha na Rais na hakufuraihishwa nazo.
vi) Mkuu wa Wilaya ya Handeni, ambaye aliwahi kuwa mtangazaji wa kituo cha ITV, Godwin Gondwe, aliamuru Polisi kuwasweka ndani waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia tukio la kufukuzwa kwa wachimbaji wadogo 3000 eneo la mlima wa mazigamba Kijiji cha Nyasa, Wilayani humo. Tukio hilo lilitokea 4/11/2016 majira ya saa nane mchana ambapo mwandishi wa Clouds Tv, Saleh Masoud na mwandishi wa Star Tv, Mackdonald walikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa saa nane huku mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima akifanikiwa kutoroka.

Haya ni baadhi ya matukio yanayodhihirisha kuwa uhuru wa kutafuta na kutoa habari hapa nchini upo shakani kwa sasa. Matumizi haya ya mamlaka ya viongozi kutaka waandishi ama watetetezi wa haki za binadamu kutoa taarifa zitakazowafuraisha au zinazoficha ukweli umejenga hofu kubwa miongoni wa waandishi na watanzania kwa ujumla.

Vitendo hivi vya Wakuu wa Wilaya vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Ibara ya 18 (kama ilivyorekebishwa mwaka 2005) inatoa haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza habari bila kufungwa/kuzuiliwa na mipaka ya kitaifa. Katiba inakataza kuingiliwa kwa mawasiliano binafsi na wakati huo huo ina vifungu vyenye kutoa haki ya kupewa taarifa kwa wakati wote katika matukio mbalimbali ya nchi na duniani kwa ujumla ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na jamii.  Ibara ya 18 ya Katiba imetoa imesisitiza kuwa, kila mtu;
a) Ana uhuru wa kutoa maoni na kueleza mawazo yake;
b) Ana haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya kitaifa;
c) Ana uhuru wa kuwasiliana na kupata ulinzi bila ya kuingiliwa mawasiliano yake; na
d)  Ana haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu ya maisha na shughuli za watu na pia masuala muhimu kwa jamii.
    Wito wetu;
• Tunawataka viongozi   wanaotumia madaraka yao kwa lengo la kutaka waandishi waandike kile kinachowapendezesha wajirekebishe kwani wanachokifanya ni kinyume na katiba.
• Sheria zote zinatoa mamlaka kwa wakuu Wilaya/Mkoa kuwaweka kuzuizini waandishi ama raia wanaotoa taarifa au maoni kinzani kufutwa katika orodha ya sheria za Tanzania.
• Viongozi watakaona kuwa waandishi wahabari wamewakosea wapeleke malalamiko yao katika Baraza la Habari (MCT), badala ya kuchukua hatua za kuwa walalamikaji, wakamataji na watoa hukumu katika masuala yahusiyo tasnia ya habari.
• Viongozi waache kufanya kazi kwa woga kwa kutaka kuficha taarifa za matatizo ya wananchi kwa kuogopa kutumbuliwa.  Kitendo hiki kinapaswa kukemewa kwani matatizo mengi ya wananchi yatakosa utatuzi kwa hofu za viongozi kuonekana maeneo yao yanamatatizo.
• Tunamshauri Mh, Rais John Pombe Magufuli kuchukua hatua stahiki kwa viongozi watakaonekana kuzuia waandishi wasifanye kazi ya kuhabarisha umma pamoja na ofisi yake matatizo yanayowakumba wananchi
• Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejipambanua kuwa ya wanyonge, haina budi kufanya kazi karibu na waandishi wa habari pamoja watetetezi wa haki za binadamu ili kufikia malengo yake ya kumsaidia mwananchi wa kawaida.
• Tunamtaka Mkuu wa Wilaya ya Arumeru amwachie mwandishi Liundi na kumwomba radhi kwa kumweka ndani bila sababu za msingi. Tunamshauri kama ana malalamiko na Mwandihsi huyo apeleke malalamiko yake MCT.
• Tunawasihi Jeshi la Polisi Wilayani Arumeru kutoa ushirikiano kwa wakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), alietumwa wilaya humo  kwa kazi ya kusimamia maswala yote ya kisheria dhidi ya Khalfani Liundi.

Tamko limetolewa leo tarehe 22/12/2016 na;
Kajubi Mukajanga,
Mkurugeniz Mtendaji-MCT

Deogratius Nsokolo,
Rais Umoja wa Vilabu vya Waandishi Tanzania-UTPC

Onesmo OlengurumwA,
Mratibu Taifa-THRDC

C & P

Mkuu wa Wilaya aagiza kukamatwa mwandishi wa habari wa ITV


Mwandishi wa habari wa Kituo cha ITV mkoani Arusha, Khalfan Lihundi, anashikiliwa na polisi katika Kituo cha Polisi Usa River, wilayani Arumeru kwa tuhuma za kuandika habari zinazodaiwa kuwa ni za uchochezi.

Lihundi alikamatwa jana jijini hapa majira ya saa nane mchana na askari anayedaiwa kutumwa na Mkuu wa Wilaya ya Arumeru, Alexander Mnyeti.

Mmoja wa waandishi wa habari walioshuhudia tukio hilo, Basil Elias, alisema kuwa, walipokuwa ofisini, alifika ofisa wa polisi akidai ametumwa kumfuata Lihundi kwa ajili ya mahojiano.

Kwa mujibu wa Elias ambaye alimnukuu ofisa huyo wa polisi, Lihundi anadaiwa kuandika habari ya uchochezi kuhusu mgogoro wa maji bila kumhoji mkuu huyo wa wilaya.

“Habari hiyo inayodaiwa kuwa ni ya uchochezi, ilikuwa ni malalamiko ya wananchi juu ya tatizo la maji katika wilaya hiyo,” alisema Elias.

Akizungumzia tukio hilo, Mwenyekiti wa Chama  cha Waandishi wa Habari, Mkoa wa  Arusha (APC), Claud Gwandu, pamoja na kulaani  tukio hilo, alisema hatua hiyo haikubaliki kwani  haikufuata taratibu za kuadhibu mwandishi wa habari.

“Hili ni tukio la kulaani na halikubaliki kwani kama mwandishi amekosea, zinapaswa kufuatwa taratibu na siyo kukamatwa kama mhalifu.

“Kilichofanyika ni matumizi mabaya ya madaraka, hivyo viongozi wa kuteuliwa hasa wakuu wa wilaya, wawe na utaratibu wa kufuata taratibu kwani mwandishi akikosea, kuna taratibu za kufuata, tunachotaka apewe dhamana,”alisema Gwandu.

Naye Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Arusha, Charles Mkumbo, alisema amesikia kuna mwandishi amekamatwa kwa kosa la uchochezi.

“Mkuu wa wilaya ametumia mamlaka yake ya sheria inayomruhusu kumweka ndani mtu hadi saa 48. Kwa hiyo, siwezi kuingilia kati suala hilo,”alisema Kamanda  Mkumbo.

Tundu Lissu akamatwa na Jeshi la Polisi


TUNDU Lissu, Mbunge wa Singida Mashariki kupitia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) anashikiliwa na Jeshi la Polisi katika Kituo Kikuu cha Kanda Maalumu ya Dar es Salaam

“Nashikiliwa na polisi hapa Kituo Kikuu kutokana na ile press conference (mkutano na waandishi wa habari) kuhusu kupotea kwa Ben Saanane,”alimweleza mwandishi wa habari hii kupitia simu leo.

Mwandishi alimtafuta Lissu kutaka kujua baadhi ya mambo, ndipo alipopokea simu na kueleza hivyo. Hakuna taarifa zaidi mpaka sasa.

Saanane ambaye ni Msaidizi wa Mwenyekiti wa CHADEMA Taifa-Freeman Mbowe alipotea ghafla takribani mwezi mmoja sasa na hajulikani alipo.

Wafuasi wa CHADEMA wamekuwa wakimsaka kiongozi huyo bila mafanikio yoyote jambo ambalo limeendelea kuzua hofu kama yu hai ama ameuawa.

Tarehe 14 Desemba mwaka huu, Lissu alizungumza na waandishi wa habari katika Makao Makuu ya chama hicho, Kinondoni jijini Dar es Salaam akiomba vyombo vya ulinzi kusaidia kupatikana kwa kiongozi huyo.

Chanzo: Mwanahalisi

Tuesday, 20 December 2016

Taasisi zinazohamasisha ushoga kufutwa


WAZIRI wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mwigulu Nchemba ametaka apewe taarifa kuhusu taasisi na mashirika yasiyo ya kiserikali (NGO) wanaohamasisha au kutangaza ndoa za jinsia moja nchini ili azifutie usajili mara moja.

Aidha ametaka kutajwa kwa watu wanaojihusisha na vitendo hivyo ili wachukuliwe hatua za kisheria kwa kujihusisha na vitendo hivyo ambavyo vinapigwa vita dunia nzima.

Nchemba aliyasema hayo jana mjini Kibaha alipokuwa akizungumza na taasisi za Kijeshi za mkoa huo zikiwemo Uhamiaji, Polisi, Magereza na Zimamoto juu ya kujua changamoto mbalimbali zinazowakabili.

Alisema kuwa taasisi hizo hazifai kwani zinafanya kazi ya laana ambayo ni kinyume cha maadili ya Kitanzania na hazistahili kuendelea kufanya kazi kwa upotoshaji huo.

“Leteni majina ya taasisi hizo ili tuzifute kwani hazistahili kuendelea kufanya jambo hilo ambalo ni laana na halipaswi kufumbiwa macho ndani ya jamii,” alisema Nchemba.

Kamanda wa polisi mkoani Pwani Bonaventura Mushongi alisema kuwa jeshi hilo linakabiliwa na changamoto mbalimbali ikiwa ni pamoja na upungufu wa vitendea kazi, ikiwa ni pamoja na magari.

Mushongi alisema kuwa licha ya kukabiliwa na changamoto hizo wamekuwa wakikabiliana na uhalifu kwenye mkoa huo ambao umekuwa kimbilio la wahalifu kutoka mikoa jirani ya Dar es Salaam.

Saturday, 17 December 2016

Gari la Mbunge Sugu lapata ajali na kuuwa mtoto.    

Gari la Mbunge wa Mbeya mjini Mh. Joseph Mbilinyi maarufu kwa jina la Sugu kupitia tiketi ya CHADEMA limepata ajali leo asubuhi ktk maeneo la iyunga na kusababisha kifo cha mtoto aliefahamika kwa jina moja la Rachael,

Wakati huo huo gari la trafiki ambalo lilikuwa likiwahi eneo la tukio ambalo  mbunge Joseph Mbilinyi amepatia ajali nalo likapata ajali katika maeneo ya Isanga ambapo trafiki wanne waliokuwepo katika gari hilo wamenusurika kifo, kati yao watatu wa walipata matibabu katika Hospital ya Rufaa Mbeya na kuruhusiwa na mmoja ambae alipata jeraha kichwani anaendelea kupata matibabu ambapo kwa mujibu wa muuguzi msaidizi wa zamu hospital ya rufaa Mbeya  bw. Hamisi Myongo amesema askari huyo ataruhusiwa leo hii baada ya  matibabu kukamilika. 
Kwa upande wake mbunge Sugu ambae hakuwa tayari kuzungumzia zaidi ajali hiyo amesema wakati ajali hiyo ikitokea nae alikuwa ktk gari hilo ambalo lilikuwa likiendeshwa na dereva wake  ambapo amesema amesikitishwa na tukio hilo 

Na Asha Athuman

Friday, 16 December 2016

C hama cha Waandishi wa Habari mkoani Mbeya kimetoa tamko la kupinga hukumu iliyotolewa dhidi ya dereva wa Shanta Mining alie sababisha ajali kwa waandishi watatu!!

Kulia ni mwenyekiti wa Chama Cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mbeya Bw. Modest Nkulu akitoa taarifa kwa waandishi wa habari hawapo pichani, kushoto ni mweka hazina wa Chama cha Waandishi wa Habari mkoa wa Mbeya Bi. Esther Macha.
 

Waandishi wa Habari mkoani Mbeya wakimsikiliza kwa umakini Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Bw. Modest Nkulu wakati akitoa tamko.
Wa kwanza kulia ni Bw. Gabriel Kandonga na wapili kutoka kulia ni Bi. Aines Thobias (wahanga wa ajali) wakisikiliza kwa umakini, wakati mwenyekiti Nkulu, wapili kutoka kushoto akitoa tamko la kupinga hukumu.

Chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya (MBPC) kimeeleza kuto kuwa na imani na hukumu iliyotolewa na Mahakama ya Wilaya ya Mbeya baada ya kumwachia huru Herman Joseph  mwenye (33) dereva  wa gari lenye  namba za usajiri T,321 CDA aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Shanta Mining, ambaye aliwagonga waandishi  watatu ambao walikuwa wakitumia usafiri wa pikipiki aina ya King Loin yenye namba za usajili Mc 923 AZQ  uliyo kuwa ikiendeshwa na Gabriel Kandonga wakati wakitekeleza majukumu yao ya kikazi.

Akizungumza na waandishi wa habari wakati akitoa taarifa ya kuto ridhishwa na mwenendo wa kesi  pamoja na hukumu  Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa wa Mbeya  (MBPC) ndugu Modestus Nkulu amesema ajali hiyo ambayo ilitokea mnamo tarehe 31/8/2016 katika barabara ya kutoka Mbalizi kuelekea Mkwajuni chunya ikihusisha gari aina ya Toyota Land Cruiser mali ya Shanta Maning  na  pikipiki ambayo ilikuwa ikitumiwa na waandishi wa habari ndugu Gabriel Kandonga, Ibrahim Yasin na Aines Thobias.

Mwenyekiti Nkulu amesema baada ya ajali hiyo, mnano tarehe 31.8.2016 kesi  yenye kumbukumbu namba MB/TR/RB/3828/2016 ilifunguliwa katika kituo cha mbalizi (Wilaya ya kipolisi Mbalizi) ambapo katika upelelezi ilishughulikiwa na WP 5830 CPL LUCY na mchoraji wa ramani ya ajali G 3944 PC MUSA wakati mkaguzi wa vyombo vya moto VIHECLE INSPECTOR wa polisi E 4677 CPL HAJI huku kesi iliyo sajiliwa kwa namba 108/2016 iliendeshwa na kusikilizwa chini ya Hakimu mkazi wa mahakama ya Wilaya Zawadi  Laizer na wakili wa serikali Catherin Paulokwa.

Aidha Nkulu akaeleza mazingira yaliyopelekea wanahabari mkoani Mbeya kukosa imani na mwenendo wa kesi pamoja  hukumu iliyotolewa mnano tarehe 13/12/2016 na mahakama hiyo ni kuendesha kesi bila mashahidi muhimu(wahanga wa tukio) kuitwa mahakamani, ambapo Nkulu alisema kufika kwa wahanga mahakamani kungesaidia mahakama kuona hali za majeruhi pamoja na uhalisia na ukubwa wa kosa.

Akifafanua zaidi mwenyekiti Nkulu amesema kuwa baada ya hukumu hiyo kutolewa uongozi wa chama cha waandishi wa habari wa mkoa wa mbeya ukiongozwa na Modest Nkulu ambae ni Mwenyekiti wa Mbeya Press Club  mnamo tarehe 14/12/2-16 ulilazimika kubisha hodi katika ofisi ya mwanasheria mkuu wa serikali ndugu Joseph Pande ili kuwasilisha masikitiko yao dhidi ya mwenendo wa kesi pamoja na hukumu iliyotolewa.

Aidha anaongeza kuwa baada ya kufanikiwa kufanya mazungumzo na mwanasheria mkuu wa mkoa wa mbeya ndugu Joseph Pande na kueleza masikitiko yake kuanzia mwenendo wa kesi tangu polisi, ofisi ya mwanasheria na mahakama, mwanasheria huyo alikiri ofisi yake kupokea taarifa ya upande wa mashitaka kushindwa hivyo ofisi yake imejipanga kushughulikia suala hilo kwa kukata rufaaa kupinga hukumu hiyo.

Hata hivyo katika kupinga hukumu hiyo chama cha waandishi wa habari mkoa wa Mbeya na wanachama wake walikuwa na tamko rasmi linalo ashiria kupiga hukumu hiyo likieleza maneno  yafuatayo  “Kwa umoja wetu kama waandishi wa habari mkoa wa Mbeya, tunapinga hukumu hiyo, kwa kuwa tunahisi haijazingatia haki na usawa kwa wahusika wote hususani wa jamhuri ambao ni walalamikaji”

MVUA YAEZUA NYUMBA KUMI MLANGALI, MKOANI SONGWE

BWANAHARUSI AINGIA MITINI MUDA MCHACHE KABLA YA NDOA JIJINI MBEYA

Samwel Mwakalobo Bwanaharusi ambaye ameingia mitini muda mchache kabla kuingia kanisani kufunga ndoa  katika kanisa la K.K.K.T Isanga jijini Mbeya.

Mwisho wa mwaka 2016 huenda ukamaliza na kituko cha aina yake katika  Mitaa ya Isanga Jijini Mbeya Mkoa wa Mbeya  mara baada ya bwanaharusi kuingia mitini masaa machache kabla ya kufunga ndoa.

Tukio hilo la aina yake limeibua maswali mengi kwa ndugu jamaa na marafiki ambao walikuwa tayari kwa maandalizi ya kuhudhuria harusi hiyo kuanzia kanisani hadi ukumbini.

Imeelezwa kuwa mipango yote ya harusi ilifanyika kwa pande zote mbili kushiriki  kwa kufuata taratibu zote zinazotakiwa kufuatwa hadi hatua ya mwisho ya kuingia kanisani ambapo kama kawaida ndugu jamaa wote walihudhuria kanisani kwa lengo la kushuhudia  tukio hilo .

Tukio rasmi lilianza majira ya saa 7 mchana katika kanisa la K.K.K.T Usharika wa   Isanga jijini Mbeya Desemba 16  ambapo kama kawaida Bibi harusi akiongozana na wapambe wake akifuata na msafara wa magari zaidi ya manne akitokea Saloon  na kuingia kanisani hapo.

Baada ya bibi harusi kuingia kanisani tayari kwa kufunga ndoa hiyo taarifa zilianza kuenea kuwa bwanaharusi hayupo kanisani hapo na hajulikani mahali alipo.

Kadri muda ulivyozidi kwenda bila bwana harusi kufika kanisani hapo baadhi ya Ndugu, jamaa  na watu waliohudhuria harusi hiyo walianza kuhoji ambapo kwa muda huo yalipita zaidi ya masaa 4 bila chochote kuendelea kanisani hapo.

Kadi ya mwaliko kwa ajili ya sherehe
Bibi harusi Given Mgaya Mkazi wa Isanga jijini Mbeya

Akielezea mkasa huo Mchungaji kanisa la K.K.K.T Usharika wa Isanga Ndugu  Andagile Mwakijungu amesema jambo hilo amelipokea kwa masikitiko makubwa kwani halijawahi tokea toka ameanza kutoa  huduma kanisani hapo.

Amesema taratibu zote za kufungwa ndoa hiyo zilifanyika na Jana Desemba 15  majira ya saa 10 jioni  wahusika wote Samwel Mwakalobo   ambaye ni bwana harusi na Given Mgaya ambaye ni bibi harusi walifika nyumbani kwa baba mchungaji  na kuafikiana kuwa harusi hiyo ifanyike leo majira ya saa 7 mchana Desemba 16 kanisani hapo hivyo kitendo cha bwanahurusi kutofika bila sababu yoyote yeye mwenyewe imestua hasa kutokana na mipango ilivyokuwa imepangwa vizuri .

Amesema jambo hilo limetokea wakati yeye akiendelea kufanya maandalizi ya  kusubiri kutoa huduma ya kufunga ndoa kati ya wawili hao  .

Amesema wakati akiendelea kusubiri ili kufungisha ndoa hiyo walitokea ndugu upande wa mume ambao waliomba msaada kwa mchungaji ili awasaidie kumtafuta kijana wao ambaye ni bwanaharusi  kwa njia yoyote ili kufaham chanzo kilichopelekea kushindwa kufika kanisani hapo bila kutoa sababu zozote.

Amesema alichukua jukumu la kumtafuta kijana huyo ambapo alifanikiwa kumpata na kuzungumza nae ambapo kijana huyo alimueleza kuwa anatatizo na baadae angefika   kwa mchungaji ili kumueleza.

Bibi harusi akitolewa kanisani huku akiwa amefunikwa khanga na wapambe wake kuelekea nyumbani baada ya shughuli ya ufungaji ndoa kushindikana kutokana na mume kuingia mitini pasipo sababu katika kanisa la K.K.K T Usharika wa Isanga jijini Mbeya .

“Baada ya wazazi kufika na kunieleza kuwa nisaidie kumtafuta kijana wao nilichukua jukumu hilo na nilifanya hivyo na nilifanikiwa kumpata lakini alicho nijibu nikuwa mchungaji ninatatizo hivyo nitafika ofisini kwako kukueleza na kwa sasa nipo njiani nikitokea Tunduma ”Amesema

Mchungaji amesema kuwa wakati wanaendelea na majadiliano ya nini kifanyike  ghafla walipata ujumbe kutoka kwa mpambe wa bwanaharusi ambao ulitumwa na bwanahaurusi mwenyewe ukieleza  kuwa asingeweza kufika ili kufunga ndoa hiyo bila kueleza sababu yoyote.

Kufuatia tukio la bwanaharusi kuingia mitini huku jitihada za kumpata kushindiana Mchungaji huyo aliamua kusitisha zoezi la ufungaji wa ndoa hiyo.

“Nimejaribu kutafuta suluhisho la ndoa hii ili ifungwe licha ya kuchelewa lakini mpaka sasa hakuna dalili zozote kuwa ndoa hii itafungwa kwani bwanaharusi hajulikani alipo hivyo nimesitisha ndoa hii na niwaombee ndugu mkafanye jitihada zenu kumtafuta kijana huyu na mfikie muafaka kwa pande zote mbili ”Alisema Mchungaji.

Amesema taratibu za ndoa zinataka siku 21 ndoa ifungwe hivyo yeye kama mchungaji kisheria ndiye mdhamini na mtangazaji wa kisheria kwa suala la ndoa ya mwaka 71 ambayo inampa mamlaka ya kueleza kwanini ndoa haikufungwa  kwa siku 21 kwa mujibu wa sheria.

Bibi harusi atolewa kanisani akiwa amevuliwa shera …………………

Katika kile ambacho kilisubiliwa kwa hamu na ndugu na jamaa kuona hitimisho la ndoa hiyo  ambapo bibi harusi aliingizwa katika gari maalumu bila kuvalishwa shera pamoja na kufunikwa kanga na kuondoka kanisani hapo majira ya saa 10 jioni wakielekea pasipo julikana huku baadhi ya ndugu wakionesha majonzi na wengine kutokwa na machozi kwa kutoa amni kile kilichotokea .

Waliochanga kwa ajili ya sherehe ya usiku……………

Mara baada ya sinema hiyo kukamilika kanisani ndugu na jamaa waliochanga pesa zao kwa ajili ya kuhudhuria sherehe ya usiku walianza kueleza kuwa watafika ukumbini kama kawaida na kula chakula na kunywa ili kufidia pesa yao.

Sherehe hiyo ilipangwa kufanyika katika Ukumbi wa Mkapa Hall jijini Mbeya na kuhudhuriwa na watu zaidi ya mia tatu ambapokila kwa michango wanakamati ilikuwa laki moja na wengine shilingi elfu 70.

Tuesday, 13 December 2016

HALMASHAURI YA JIJI LA MBEYA YAINGIA MKATABA KUBORESHA MIUNDOMBINU.

Meya wa jiji la Mbeya David Mwashilindi akisaini Mkataba kwa ajili ya uboreshaji wa Miundombinu ya barabara katika jiji la Mbeya.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)
Baadhi ya Wakandarasi wa makampuni mbalimbali ya jiji la Mbeya wakisaini mikataba kwa ajili ya uboreshaji wa miundombinu ya barabara katka baadhi ya kata jijini Mbeya hafla ambayo imehudhuriwa pia na baadhi ya madiwani na watendaji wa halmashauri ya jiji katika ofisi ya Meya.(Picha na David Nyembe wa Fahari News)




HALMASHAURI ya Jiji la Mbeya, leo imeingia mkataba na makandarasi mbalimbali wa ujenzi wa miundombinu ya barabara pamoja na madaraja katika Kata 14.

Mkataba huo, umesainiwa na Mstahiki Meya wa Jiji la Mbeya, David Mwashilindi huku ukishuhudiwa na baadhi ya madiwani wa Kata husika pamoja na mwanasheria wa halmashauri hiyo Davis Mbembela.

Awali akizungumzia tukio hilo kabla ya kusaini, Meya Mwashilindi amesema, mkatba huo,  unalenga kuboresha miundombinu katika baadhi ya kata katika halmashauri hiyo  ambapo kazi hiyo inataraji kuanza mapema mwezi huu.

Aidha, amesema  kuwa mkataba huo unagharimu kiasi cha shilingi milioni 300 na kwamba kazi kubwa itakayofanyika ni uboreshaji wa barabara na matengenezo ya madaraja katika kata 14 kati ya 36 zilizomo ndani ya Jiji la Mbeya.

“Kampuni zilizoingia mkataba leo ni tano na zote ni makandarasi wa ndani na kubwa zaidi ni wazawa,”amesema.

Pia,  Mwashilindi amewataka makandarasi waliochukua kazi hizo kuhakikisha wanafanya kazi kwa kiwango kinachotakiwa na kwa muda muafaka huku akiwatoa hofu juu ya fedha, kwani bajeti ya matengenezo hayo tayari imeidhinishwa..

Hata hivyo, katika kuhakikisha zoezi hilo linafanikiwa kwa asilimia 100, Mwashilindi amewataka watendaji pamoja na madiwani kuhakikisha wanatembelea na kukagua miradi hiyo, wakati ikiendelea kufanyika na kuachana na tabia ya kusubili mradi ukamilike na kukabidhiwa na ndipo kuanza kubaini kasoro.

“Serikali imekuwa ikitumia fedha nyingi na asilimia kubwa inatokana na kodi za wananchi hivyo ninawaombeni madiwani na watumishi hasa wa idara husika kuhakikisha mnatembelea na kuukagua mradi huu wakati wote wa mchakato, sitapenda kusikia changamoto mara baada ya mradi kukamilika,”amesema.

Mwisho.

Serikali ya China kujenga kiwanja cha kisasa Chalinze

Serikali ya China imetoa ufadhili wa ujenzi wa uwanja wa Michezo kwa shule ya msingi Msoga iliyopo halmashauri ya wilaya ya Chalinze….

Akizungumza katika hafla ya kuoneshwa eneo patakapojengwa uwanja huo  Rais mstaafu wa awamu ya nne Dkt Jakaya Kikwete  ameishukuru serikali ya China kwa msaada huo kwakuwa Michezo ni Kitu muhimu kwa watoto huku akitoa rai kwa halmashauri ya chalinze kulinda eneo hilo.

Kwaupande wake mwakilishi wa balozi wa China amesema kuwa China inajivunia uhusiano mwema uliopo kati ya China na Tanzania,na watahakikisha wanajenga uwanja huo kwa wakati ili kuwapa fursa watoto kufurahia michezo.

Nae Mbunge wa Chalinze Ridhiwani Kikwete ametoa rai kwa wananchi wake kuhakikisha eneo lililotengwa linalindwa ili dhamira ya china kujenga uwanja huo itimie

Ufadhili wa ujenzi wa uwanja huo wa michezo kwa watoto wa Msoga ni muendelezo wa ufadhili wa China katika kijiji cha Msoga baada ya kujenga shule ya msingi Msoga.

Sunday, 11 December 2016

Washindi wa EATV AWARDS 2016 hawa hapa



Historia imeandikwa kwenye tasnia ya sanaa nchini ambapo kwa mara ya kwanza tukio la utoaji wa tuzo za #EATVAwards kwa wasanii wa muziki na filamu Afrika Mashariki, limefanyika usiku wa kuamkia leo katika ukumbi wa Mlimani City jijini Dar es salaam. 
 

Tuzo hizo zilizoandaliwa na East Africa Television Ltd, zimekuwa za kwanza Afrika Mashariki, ambapo wasanii mbali mbali wamefanikiwa kujinyakulia tuzo zao.
  
Tazama orodha nzima ya washindi hapa chini..
  
Kipengele cha mwanamuziki bora wa kiume 
G Nako – 'Original'
Sheta –'Namjua'
Mwana FA – 'Ahsanteni kwa Kuja'
Alikiba – 'Aje' --- MSHINDI 
Ben Pol – 'Moyo Mashine'
  
Mwana muziki bora wa kike 
Lilian Mbabazi – 'Yoola'
Ruby – 'Forever'
Lady Jay dee – 'Ndindindi' --- MSHINDI 
Linah – 'No stress'
Vanessa Mdee – 'Niroge'
  
Mwanamuziki bora chipukizi 
Manfongo – 'Hainaga ushemeji' --- MSHINDI 
Feza Kessy – 'Sanuka'
Rukia Jumbe (Ruky Baby) – 'Mpasuo'
Bright – 'Nitunzie'
Mayunga – 'Nice couple'
  
Kundi bora la mwaka 
Navy kenzo – 'Kamatia chini'--- MSHINDI 
Mashauzi Clasic - 'Kismat'
Team Mistari – 'Tuzidi'
Sauti Sol – 'Unconditional bae'
Wakali wao – 'Chozi langu utalilipa'
  
Video bora ya mwaka 
Njogereza – Navio
Namjua – Shetta
Aje – Alikiba -- MSHINDI 
Don't Bother – Joh Makini
Ndindindi – Lady Jaydee
  
Wimbo bora wa mwaka
Don't bother – Joh Makini
Ndindindi - Lady Jayedee
Kamatia chini - Navy Kenzo
Moyo mashine – Ben Pol
Aje – Alikiba --- MSHINDI 
  
Filamu bora ya mwaka 
Facebook profile
  
Safari ya Gwalu --- MSHINDI 
Mfadhili wangu
Hii ni laana
Nimekosea wapi
  
Muigizaji bora wa kiume 
Meya Shabani Khamisi
  
Salim Ahmed (Gabo) --- MSHINDI 
Daudi Machael (Duma)
Doto Hussein Matotola
Said Mkukila
  
Muigizaji bora wa kike 
Chuchu Hansy --- MSHINDI 
Rachel Bithulo
Frida Kajala Masanja
Khadija Ally
  
TUZO YA HESHIMA
DJ Maarufu bongo Boniventure Kilossa (Dj Bonny Love) ndiye mtu aliyepewa tuzo maalum ya heshima, akitambuliwa kutokana na mchango wake kwenye tasnia ya sanaa hapa nchini

Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika sherehe za kuzaliwa Mtume Muhammad (S.A.W) zitakazofanyika kitaifa mkoani Singida.

WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa anatarajiwa kuwa mgeni rasmi kwenye Siku ya Maulid ya kuzaliwa kwa Mtume Muhammad (S.A.W) ambayo kitaifa itaadhimishwa mkoani Singida.

Katibu wa Bakwata Mkoa wa Singida, Alhaji Buruhani Mlau alisema sherehe za Kitaifa za Maulid ya Mtume Mohammad (SAW) kwa mwaka huu zinatarajiwa kufanyika Mkoani Singida katika Kijiji cha Shelui, wilayani Iramba, Singida.

Wiki iliyopita, akitangaza utaratibu wa sherehe hizo, Mufti wa Tanzania, Sheikh Abubakar Zubeir alisema kwa mwaka huu, Maulid itasomwa usiku wa Desemba 11 na mapumziko yatakuwa siku inayofuata yaani Desemba 12. 

Mufti wa Tanzania aliwataka Waislamu wote nchini waadhimishe Siku ya Maulid kwa kufanya usafi, kupanda miti na kuchangia damu.

“Waislamu wanatakiwa kutumia siku hiyo kwa kufanya matendo mema na yenye kumpendeza Mwenyezi Mungu ikiwa ni pamoja na kufanya usafi kwenye mitaa yao na kuchangia damu ili kusaidia wenye uhitaji huo,” alisema.

MADA YA UJASIRIAMALI: TATIZO MTAJI NDIYO ISHU:

Karibu Jumapili hii katika mada ya ujasiriamali. Lengo letu kubwa ni kupata ujuzi, elimu au maarifa mbalimbali kupitia ukurasa huu.

Mada ya leo inajikita zaidi kwa watu ambao wamekuwa wakilia kuwa wanashindwa kufanya jambo fulani kwa sababu ya kukosa mtaji.

Hivi ni kweli kwa elimu, ujinga, ufahamu wako, maeneo unayoishi, namna unavyoishi inakosa mtaji.

Kilio kikubwa cha Wanadamu wengi duniani ni kuhusu mtaji, mtu anaamini akiwa na mtaji haweI kukosa cha kufanya lakini katika uhalisi ni kweli kwamba mtaji ndiyo kila kitu.

Ni kweli lakini si kweli, mtaji ambao wengi wamekuwa wakidhania ni fedha pekee, ila wanasahau kuwa kuna mtaji rasilimali watu, wanasahau mtaji inaweza kuwa rasilimali aridhi, wanasahau kuwa mtaji mkubwa ni kuwa na WAZO la kitu unachotaka kukifanya.

Unaweza kuwa na mtaji lakini ukakosa cha kufanya au kama utafanya basi utafanikiwa nimagumashimagumashi kwa sababu tu huna elimu na hicho kitu, hukuwa na wazo hilo miaka miwili kabla.

Ndiyo maana utasikia kuna misemo kama kubaka fani, kwa mtindo wako wa kupata pesa na kurukia kufanya biashara fulani, huko ni sawa na kuibaka hiyo biashara.

Mtaji haujawahi kuwa tatizo bali tatizo ni wewe mwenyewe, ingawa wengi wanaamini mtaji ni pesa kwa sababu ndizi zinazotumika katika maisha ya kila siku. kama kweli mtaji ni MAWAZO kwa nini usiyatumie yakupe mtaji pesa.

Kama mtaji ni watu kwa nini usiwatumie watu hao kukupatia mtaji utakaougeuza kuwa pesa. Kama mtaji ni aridhi mbona huitumii kwa kuigeuza kuwa pesa.

Hili ni tatizo, mtaji ni kile ulichonacho, achana na mawazo ya kutaka kupata mtaji pesa wakati wa mawazo, aridhi na watu hujautumia.

Acha kukilaumu kuwan
TATIZO ni mtaji, hata kama ndiyo unataka nani akutafutie huo mtaji, unadhani nani yuko tayari kukupa wewe mtaji pesa wakati mwezi wa kwanza ada imekaribia. Mama mwenye nyumba anadai hela ya pango, bili ya maji na umeme vinamsubiri.

Umiza akili kutumia mtaji ulionao kuingiza pesa, leo hii kuna watu wanaishi kwa sababu tu walikuwa na wazo fulani ambalo waluligeuza nakuwa mtaji pesa.

Nimalize kwa kukaribisha ushauri au maoni ya moja kwa moja au inbox.

Saturday, 10 December 2016

Rais Magufuli Atoa Msamaha Kwa Wafungwa 5,678 Katika Maadhimisho Ya Miaka 55 Ya Uhuru Wa Tanzania Bara

Katika kuadhimisha miaka 55 ya Uhuru wa Tanzania Bara tarehe  9 Disemba, 2016 Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa kutumia madaraka aliyopewa chini ya Ibara ya 45(1)(d) ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ametoa msamaha kwa wafungwa wafuatao:-

(i) Wafungwa wote wamepunguziwa moja ya sita (1/6) ya vifungo vyao zaidi ya punguzo la kawaida linalotolewa chini ya kifungu 49(1) cha Sheria ya Magereza Sura ya 58 isipokuwa wafungwa walioorodheshwa katika Ibara ya 2 (i-xx).

(ii)Wafungwa wagonjwa wenye magonjwa kama UKIMWI, KIFUA KIKUU (TB) na SARATANI (CANCER) ambao wako kwenye “terminal stage”. Wafungwa ambao wamethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iii)Wafungwa wazee wenye umri wa miaka sabini (70) au zaidi ambao umri huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

(iv)Wafungwa wa kike walioingia na mimba gerezani, pamoja na wale walioingia na watoto wanaonyonya na wasionyonya.

(v)Wafungwa wenye ulemavu wa mwili na akili (Physical disability and mental disability) ambao ulemavu huo umethibitishwa na Jopo la Waganga chini ya Uenyekiti wa Mganga Mkuu wa Mkoa/Mganga Mkuu wa Wilaya.

2.Aidha, Msamaha huu wa Mheshimiwa Rais hautawahusu wafungwa wafuatao:-

(i)Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa.

(ii)Wafungwa waliohukumiwa adhabu ya kunyongwa na adhabu hiyo kubadilishwa kuwa kifungo cha maisha au kifungo gerezani.

(iii)Wafungwa waliohukumiwa kifungo cha maisha gerezani.

(iv)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji na matumizi ya madawa ya kulevya kama vile cocaine, heroin, bhangi n.k.

(v)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kujihusisha na uombaji, upokeaji au utoaji rushwa.

(vi)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya unyang’anyi na unyang’anyi wa kutumia silaha au kujaribu kutenda makosa hayo (robbery with violence, armed robbery and attempt robbery).

(vii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya kupatikana na silaha, risasi au milipuko isivyo halali (firearms, ammunitions and explosives).

(viii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya shambulio la aibu, kunajisi, kubaka na kulawiti, au kujaribu kutenda makosa hayo.

(ix)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa kosa la kuwapa mimba wanafunzi wa Shule za Msingi na Shule za Sekondari na ambao walitenda kosa hilo wakiwa na umri wa miaka kumi na nane (18) na kuendelea.

(x)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya wizi wa magari na pikipiki au kujaribu kutenda makosa hayo.

(xi)Wafungwa wanaotumikia kifungo chini ya Sheria ya Bodi ya Parole (Act. No. 25/1994) na Sheria ya Huduma kwa Jamii (Act. No. 6/2002).

(xii)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kifungo kwa makosa ya kutumia vibaya madaraka yao.

(xiii)Wafungwa waliowahi kupunguziwa kifungo na Msamaha wa Mheshimiwa Rais na bado wangali wanaendelea kutumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

(xiv)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kuzuia watoto kupata masomo.

(xv)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la utekaji wa watoto, kupoka na kufanya biashara ya binadamu (Human Trafficking).

(xvi)Wafungwa waliopatikana na hatia na kuhukumiwa kwa kosa la kukutwa na viungo vya binadamu.

(xvii)Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kujihusisha na usafirishaji wa nyara za Serikali na ujangili (Poachers).

(xviii)Wafungwa wanaotumikia kifungo kwa makosa ya        wizi/ubadhirifu wa fedha za Serikali.

(xix)Wafungwa wanaotumikia vifungo kwa makosa ya kutoroka au kujaribu kutoroka chini ya ulinzi halali.

(xx)Wafungwa walioingia gerezani baada ya tarehe 9/10/2016.

3.Wafungwa wapatao 5,678 watafaidika na msamaha huu baada ya kupunguziwa 1/6 ya vifungo vyao ambapo 1,340 wataachiliwa huru na wafungwa 4,338 watanufaika na kubaki gerezani wakitumikia sehemu ya kifungo kilichobaki.

 

 Ni mategemeo ya Serikali kwamba watakaoachiliwa huru watarejea tena katika jamii kushirikiana na wenzao katika ujenzi wa Taifa na kwamba watajiepusha kutenda makosa ili wasirejee tena gerezani.

Imesainiwa na;

Meja Jenerali  Projest  Rwegasira

KATIBU MKUU WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI

9/12/2016

Friday, 9 December 2016

M zee wangu Kilomoni nakukumbusha… ‘AKILI YA KUAMBIWA CHANGANYA NA YAKO’

Na John Joseph
TANGU naanza kupata uelewa wa kutambua vitu, nilizikuta Simba na Yanga zikiwa ni klabu kubwa na zenye mtaji mkubwa wa mashabiki japo wanachama ‘hai’ hawakuwa wengi.

Asikudanganye mtu hizi timu zinapendwa na Watanzania, ilifikia hatua kila Mtanzania ambaye anazaliwa na kuanza kupata ufahamu kama nilivyokuwa mimi ilikuwa ni lazima achague kuishabikia moja kati ya timu hizo mbili labda tu awe siyo mtu wa michezo.

Nikiwa mdogo hata mama yangu japo siyo mtu wa soka lakini alikuwa akishangilia moja ya timu hizo na kutaniana na baba yangu ilipotokea mmoja wao timu yake imefungwa.

Miaka ya zamani kuna matajiri wachache walitumia fursa ya klabu hizo kuwa na mtaji wa watu wengi kujineemesha binafsi kwa gia ya kuwa wadhamini au wafadhili. Lakini natambua kuwa wapo waliotoa fedha zao kwa mapenzi na hawakuwa na lengo la kuingiza kwa mlango wa nyuma.

Matajiri wengi walijineemesha kwa mlango wa nyuma na sisi tulishangilia bila kujua, leo hii matajiri wa kizazi cha sasa wanataka kuingia kwenye klabu hizo kujineemesha kwa mlango wa mbele au naweza kusema ni wa halali, tunaanza kuwapiga vita.

Yusuf Manji anaitaka Yanga lakini fitina anazokutana nazo anazijua yeye na watu wake wa karibu, Mohamed Dewji ‘Mo’ anataka kuwekeza ndani ya Simba, naye kama ilivyo kwa Manji anakutwa na yaleyale.

Najua hakuna biashara inayoanza kisha ikawa sahihi kwa kila kitu lakini tunatakiwa kujifunza kuwa dunia ya leo siyo ya mwaka 1993. Tunatakiwa kubadilika.

Kuwakosoa Manji na Mo inatakiwa iwe katika msingi wa kuwaonyesha njia sahihi ya kupita lakini kuwafanyia fitina ni kuzihalalisha Simba na Yanga kuendelea kuishi kimasikini wakati zinao uwezo wa kujitoa kwenye tabia ya kuombaomba.

Wazee wetu walipambana kweli kuzifikisha hapo zilipo Simba na Yanga, lakini wanatakiwa wakubali kuwa hatuwezi kuishi maisha yaleyale kisa tu wakati timu hizo zinaanzishwa na kukuzwa hatukuwepo.

Dunia ya sasa soka ni biashara kubwa, idadi ya mashabiki au wanachama ndiyo mtaji wenyewe na ndiyo maana mabilionea wa Ulaya wanatoa fedha nyingi kuwekeza kwenye klabu, wanajua ili wao wapate faida ni lazima wazifanye timu zao zipate mafanikio.

Haki namba moja ya shabiki wa timu ni kushangilia na kuzomea, ndiyo maana shabiki anatoa kiingilio chake ili apate burudani ya kuzomea au kushangilia na hakuna anayejali nani anafanya nini nje ya hapo ilimradi timu iwe na maendeleo na yeye kiingilio chake kitendewe haki.

Wale mashabiki wanaoenda mbele zaidi na kuwa wanachama ni haki yao kuhoji masuala kadhaa ya kiutawala lakini yawe na hoja za msingi yenye kulenga kusaidia klabu na siyo kuifanya ibaki masikini kisha yeye huyohuyo awe analaumu kuwa klabu au timu yake haipati maendeleo.

Siku kadhaa zilizopita Simba iliitisha mkutano kwa mujibu wa katiba yao, moja ya hoja iliyopangwa ni kuhusu Mo kuwekeza klabuni hapo, wakati wanachama wakiusubiri mkutano huo anaibuka mzee wangu ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa Simba, Hamisi Kilomoni akidai hatambui mkutano huo.

Wanasema mtu mzima akikosea huwa hakosolewi hadharani lakini katika hili nalazimika kumwambia mzee wangu kauli ya kiutu uzima kuwa mara baada ya kumaliza kusoma makala haya, akirudi nyumbani, usiku wa leo wakati anajiandaa kuutafuta usingizi achukue dakika tano tu atafakari kwa umakini sana hiki alichotumwa kukizungumza kuhusu klabu yake, pia kabla ya kusinzia autafakari ule msemo wa ‘AKILI ZA KUAMBIWA CHANGANYA NA ZAKO’.

Msemo huo unaweza kuchukuliwa pia na wale wa Yanga wanaopinga uwekezaji wa Manji.

Kuna siku nilimsikia Katibu wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja akisema kuwa kama matajiri hao wanataka kuwa na timu wakaanzishe timu zao.

Ni kauli ya kishabiki ambayo kwangu mimi haina mashiko, ukaanzishe timu Tanzania hii nje ya Simba na Yanga na utegemee ikuingizie kipato kikubwa! Inawezeka lakini siyo kwa sasa.

Azam FC ilianzishwa kwa uwekezaji mkubwa lakini bado ukweli ni kuwa kile kilichowekezwa na kinachoingia klabuni hapo ni vitu viwili tofauti, tusiwe wanafiki, huo ndiyo ukweli.

Awali Azam FC ilionekana imeanzishwa ili kuwa sehemu ya kutangaza bidhaa za mmiliki, baadaye malengo yalibadilika lakini kwa asili ya soka letu bado ipo chini ya vivuli vya wakongwe hao wawili.

Simba na Yanga ni mtaji mkubwa, zinatakiwa kuwa mfano, kisha nyingine ziige lakini kuacha mitaji hiyo iendelee kuwa masikini kisha nguvu kubwa itumike kuanzisha klabu nyingine ni kupoteza muda na hakuna anayeweza kufanya hivyo kwa sasa, tusidanganyane.

M zee wangu Kilomoni nakukumbusha… ‘AKILI YA KUAMBIWA CHANGANYA NA YAKO’

Na John Joseph
TANGU naanza kupata uelewa wa kutambua vitu, nilizikuta Simba na Yanga zikiwa ni klabu kubwa na zenye mtaji mkubwa wa mashabiki japo wanachama ‘hai’ hawakuwa wengi.

Asikudanganye mtu hizi timu zinapendwa na Watanzania, ilifikia hatua kila Mtanzania ambaye anazaliwa na kuanza kupata ufahamu kama nilivyokuwa mimi ilikuwa ni lazima achague kuishabikia moja kati ya timu hizo mbili labda tu awe siyo mtu wa michezo.

Nikiwa mdogo hata mama yangu japo siyo mtu wa soka lakini alikuwa akishangilia moja ya timu hizo na kutaniana na baba yangu ilipotokea mmoja wao timu yake imefungwa.

Miaka ya zamani kuna matajiri wachache walitumia fursa ya klabu hizo kuwa na mtaji wa watu wengi kujineemesha binafsi kwa gia ya kuwa wadhamini au wafadhili. Lakini natambua kuwa wapo waliotoa fedha zao kwa mapenzi na hawakuwa na lengo la kuingiza kwa mlango wa nyuma.

Matajiri wengi walijineemesha kwa mlango wa nyuma na sisi tulishangilia bila kujua, leo hii matajiri wa kizazi cha sasa wanataka kuingia kwenye klabu hizo kujineemesha kwa mlango wa mbele au naweza kusema ni wa halali, tunaanza kuwapiga vita.

Yusuf Manji anaitaka Yanga lakini fitina anazokutana nazo anazijua yeye na watu wake wa karibu, Mohamed Dewji ‘Mo’ anataka kuwekeza ndani ya Simba, naye kama ilivyo kwa Manji anakutwa na yaleyale.

Najua hakuna biashara inayoanza kisha ikawa sahihi kwa kila kitu lakini tunatakiwa kujifunza kuwa dunia ya leo siyo ya mwaka 1993. Tunatakiwa kubadilika.

Kuwakosoa Manji na Mo inatakiwa iwe katika msingi wa kuwaonyesha njia sahihi ya kupita lakini kuwafanyia fitina ni kuzihalalisha Simba na Yanga kuendelea kuishi kimasikini wakati zinao uwezo wa kujitoa kwenye tabia ya kuombaomba.

Wazee wetu walipambana kweli kuzifikisha hapo zilipo Simba na Yanga, lakini wanatakiwa wakubali kuwa hatuwezi kuishi maisha yaleyale kisa tu wakati timu hizo zinaanzishwa na kukuzwa hatukuwepo.

Dunia ya sasa soka ni biashara kubwa, idadi ya mashabiki au wanachama ndiyo mtaji wenyewe na ndiyo maana mabilionea wa Ulaya wanatoa fedha nyingi kuwekeza kwenye klabu, wanajua ili wao wapate faida ni lazima wazifanye timu zao zipate mafanikio.

Haki namba moja ya shabiki wa timu ni kushangilia na kuzomea, ndiyo maana shabiki anatoa kiingilio chake ili apate burudani ya kuzomea au kushangilia na hakuna anayejali nani anafanya nini nje ya hapo ilimradi timu iwe na maendeleo na yeye kiingilio chake kitendewe haki.

Wale mashabiki wanaoenda mbele zaidi na kuwa wanachama ni haki yao kuhoji masuala kadhaa ya kiutawala lakini yawe na hoja za msingi yenye kulenga kusaidia klabu na siyo kuifanya ibaki masikini kisha yeye huyohuyo awe analaumu kuwa klabu au timu yake haipati maendeleo.

Siku kadhaa zilizopita Simba iliitisha mkutano kwa mujibu wa katiba yao, moja ya hoja iliyopangwa ni kuhusu Mo kuwekeza klabuni hapo, wakati wanachama wakiusubiri mkutano huo anaibuka mzee wangu ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa Simba, Hamisi Kilomoni akidai hatambui mkutano huo.

Wanasema mtu mzima akikosea huwa hakosolewi hadharani lakini katika hili nalazimika kumwambia mzee wangu kauli ya kiutu uzima kuwa mara baada ya kumaliza kusoma makala haya, akirudi nyumbani, usiku wa leo wakati anajiandaa kuutafuta usingizi achukue dakika tano tu atafakari kwa umakini sana hiki alichotumwa kukizungumza kuhusu klabu yake, pia kabla ya kusinzia autafakari ule msemo wa ‘AKILI ZA KUAMBIWA CHANGANYA NA ZAKO’.

Msemo huo unaweza kuchukuliwa pia na wale wa Yanga wanaopinga uwekezaji wa Manji.

Kuna siku nilimsikia Katibu wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja akisema kuwa kama matajiri hao wanataka kuwa na timu wakaanzishe timu zao.

Ni kauli ya kishabiki ambayo kwangu mimi haina mashiko, ukaanzishe timu Tanzania hii nje ya Simba na Yanga na utegemee ikuingizie kipato kikubwa! Inawezeka lakini siyo kwa sasa.

Azam FC ilianzishwa kwa uwekezaji mkubwa lakini bado ukweli ni kuwa kile kilichowekezwa na kinachoingia klabuni hapo ni vitu viwili tofauti, tusiwe wanafiki, huo ndiyo ukweli.

Awali Azam FC ilionekana imeanzishwa ili kuwa sehemu ya kutangaza bidhaa za mmiliki, baadaye malengo yalibadilika lakini kwa asili ya soka letu bado ipo chini ya vivuli vya wakongwe hao wawili.

Simba na Yanga ni mtaji mkubwa, zinatakiwa kuwa mfano, kisha nyingine ziige lakini kuacha mitaji hiyo iendelee kuwa masikini kisha nguvu kubwa itumike kuanzisha klabu nyingine ni kupoteza muda na hakuna anayeweza kufanya hivyo kwa sasa, tusidanganyane.