Thursday 22 December 2016

TAMKO LA PAMOJA KULAANI KITENDO CHA KUWEKWA KIZUIZINI MWANDISHI WA HABARI WA KITUO CHA ITV KHALFAN LIUNDI MKOANI ARUSHA

Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu Tanzania (THRDC), Baraza la Habari Tanzania (MCT) pamoja na Umoja wa Vilabu vya Waandishi wa Habari Tanzania (UTPC) , tumesikitishwa na vitendo vinavyoendelea nchini,   chini ya uratibu  wa baadhi ya viongozi wa serikali za Mitaa ( hasa Wakuu wa Wilaya) vya kutaka kunyamazisha ama kuzuia kabisa waandishi wasifanye kazi zao kwa uhuru.  Matukio kadhaa yanaonyesha kuwa uhuru wa waandishi wa habari kutafuta na kutoa habari umezidi kubinywa na kujenga hofu miongoni mwa wanahabari kwa kipindi cha mwaka mmoja sasa toka viongozi wapya waingie madarakani.

Mwandishi wa habari wa kituo cha Televisheni (ITV), Bwana Khalfan Liundi ameendelea kushikiliwa na Polisi Wilayani Arumeru kwa amri ya Mkuu wa Wilaya hiyo Alexander Mnyeti toka tarehe 21/12/2016 hadi hivi sasa tunapotoa tamko hili bila kifikishwa mahakamani. Taarifa za awali kutoka Arusha zinaonyesha kuwa Mkuu wa Wilaya ya Arumeru hakupendezwa na taarifa iliyorushwa na ITV tarehe 20/12/2016 na kuonyesha wananchi waliokuwa wakiandamana kudai haki yao ya kupata maji. Kwa mujibu wa wandishi wa habari mkoani Arusha mwandishi huyu amekamatwa kwa kutoa taarifa hiyo ya maji ambayo kwa mujibu wa Mkuu wa Wilaya inaonekana kuwa ni ya kichochezi.

Matukio ya viongozi wa Serikali za Mitaa hasa Wakuu wa Wilaya kutishia na kutoa amri waandishi kuwekwa kuzuizini wanapotoa taarifa toka maeneo yao ya kazi yamefikia zaidi ya matano toka January 2016.  Kwa mujibu wa Sheria ya Wakuu wa Mikoa na Wilaya ya mwaka 1962 na Sheria ya Serikali za Mitaa zilizokuwa pia zinaumika kipindi cha mkoloni Mkuu wa Wilaya au Mkoa ana mamlaka ya kuamrisha polisi kumweka mtu yoyote kuzuizini na kumlaza rumande na kesho yake kumwachia bila mashtaka yoyote. Yafuatayo ni baadhi ya Matukio ya kutiwa kizuizini kwa waandishi wa habari kwa amri za wakuu wa wilaya;

i) Tabora Igunga mwandishi wa Chanel Ten Jumbe ismail aliswekwa rumande kwa masaa na kwakosa la kurupoti maandamano ya wananchi
ii) Mwandishi wa ITV Kanda ya ziwa Cosmas Makongo alikamatwa tarehe  8/10/2016 kwa amri ya Mkuu wa Wilaya ya Kyerwa Mkoani Kagera, Shaaban Lissu (Mwanahabari mwenzake) baada ya kuripoti janga la njaa iliyokuwa ikiwakabili wananchi wa wilaya hiyo, na baada ya hapo alitakiwa kukanusha habari aliyoiripoti na ndiyo akawekwa lumande kwa takribani saa 2 kabla ya kuachiwa.
iii) Mwandishi wa Radio Free Africa na Gazeti la Mwananchi, Baraka Tiluzilamsomi ambaye alikamatwa 6th /4/2016 na kuwekwa mahabusu kwa saa 7 baada ya amri ya mkuu wa Wilaya ya Chato, Shaaban Ntarambe, aliyedai mwandishi huyo aliingia eneo la hospitali ya wilaya ya Chato bila kupata kibali kutoka kwake.
iv) Mkuu wa Wilaya ya Iringa, Richard Kasesela, aliwakamata waandishi wa habari wa kituo cha Radio Ebony FM cha mjini Iringa na kuwaachia tarehe 1/4/2016 siku baada ya kuwafikisha kituoni.
v) Mkuu wa Wialya ya Kibaha, Assumpter Mshama, alitumia mamlaka yake tarehe 29/11/2016 kumwita mwandishi wa Mwananchi Sanjto Msafiri mbele ya mkutano na kumsuta na huku akimtaka akanushe habari ambayo aliitoa mbele ya wafanyabiashara. Mkuu wa Wilaya alidai taarifa alizotoa mwandishi ni za kumchonganisha na Rais na hakufuraihishwa nazo.
vi) Mkuu wa Wilaya ya Handeni, ambaye aliwahi kuwa mtangazaji wa kituo cha ITV, Godwin Gondwe, aliamuru Polisi kuwasweka ndani waandishi wa habari waliokuwa wakifuatilia tukio la kufukuzwa kwa wachimbaji wadogo 3000 eneo la mlima wa mazigamba Kijiji cha Nyasa, Wilayani humo. Tukio hilo lilitokea 4/11/2016 majira ya saa nane mchana ambapo mwandishi wa Clouds Tv, Saleh Masoud na mwandishi wa Star Tv, Mackdonald walikamatwa na kuwekwa mahabusu kwa saa nane huku mwandishi wa gazeti la Tanzania Daima akifanikiwa kutoroka.

Haya ni baadhi ya matukio yanayodhihirisha kuwa uhuru wa kutafuta na kutoa habari hapa nchini upo shakani kwa sasa. Matumizi haya ya mamlaka ya viongozi kutaka waandishi ama watetetezi wa haki za binadamu kutoa taarifa zitakazowafuraisha au zinazoficha ukweli umejenga hofu kubwa miongoni wa waandishi na watanzania kwa ujumla.

Vitendo hivi vya Wakuu wa Wilaya vinakiuka Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, chini ya Ibara ya 18 (kama ilivyorekebishwa mwaka 2005) inatoa haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza habari bila kufungwa/kuzuiliwa na mipaka ya kitaifa. Katiba inakataza kuingiliwa kwa mawasiliano binafsi na wakati huo huo ina vifungu vyenye kutoa haki ya kupewa taarifa kwa wakati wote katika matukio mbalimbali ya nchi na duniani kwa ujumla ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na jamii.  Ibara ya 18 ya Katiba imetoa imesisitiza kuwa, kila mtu;
a) Ana uhuru wa kutoa maoni na kueleza mawazo yake;
b) Ana haki ya kutafuta, kupokea na kusambaza taarifa bila kujali mipaka ya kitaifa;
c) Ana uhuru wa kuwasiliana na kupata ulinzi bila ya kuingiliwa mawasiliano yake; na
d)  Ana haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali muhimu ya maisha na shughuli za watu na pia masuala muhimu kwa jamii.
    Wito wetu;
• Tunawataka viongozi   wanaotumia madaraka yao kwa lengo la kutaka waandishi waandike kile kinachowapendezesha wajirekebishe kwani wanachokifanya ni kinyume na katiba.
• Sheria zote zinatoa mamlaka kwa wakuu Wilaya/Mkoa kuwaweka kuzuizini waandishi ama raia wanaotoa taarifa au maoni kinzani kufutwa katika orodha ya sheria za Tanzania.
• Viongozi watakaona kuwa waandishi wahabari wamewakosea wapeleke malalamiko yao katika Baraza la Habari (MCT), badala ya kuchukua hatua za kuwa walalamikaji, wakamataji na watoa hukumu katika masuala yahusiyo tasnia ya habari.
• Viongozi waache kufanya kazi kwa woga kwa kutaka kuficha taarifa za matatizo ya wananchi kwa kuogopa kutumbuliwa.  Kitendo hiki kinapaswa kukemewa kwani matatizo mengi ya wananchi yatakosa utatuzi kwa hofu za viongozi kuonekana maeneo yao yanamatatizo.
• Tunamshauri Mh, Rais John Pombe Magufuli kuchukua hatua stahiki kwa viongozi watakaonekana kuzuia waandishi wasifanye kazi ya kuhabarisha umma pamoja na ofisi yake matatizo yanayowakumba wananchi
• Serikali ya Awamu ya Tano ambayo imejipambanua kuwa ya wanyonge, haina budi kufanya kazi karibu na waandishi wa habari pamoja watetetezi wa haki za binadamu ili kufikia malengo yake ya kumsaidia mwananchi wa kawaida.
• Tunamtaka Mkuu wa Wilaya ya Arumeru amwachie mwandishi Liundi na kumwomba radhi kwa kumweka ndani bila sababu za msingi. Tunamshauri kama ana malalamiko na Mwandihsi huyo apeleke malalamiko yake MCT.
• Tunawasihi Jeshi la Polisi Wilayani Arumeru kutoa ushirikiano kwa wakili wa Mtandao wa Watetezi wa Haki za Binadamu (THRDC), alietumwa wilaya humo  kwa kazi ya kusimamia maswala yote ya kisheria dhidi ya Khalfani Liundi.

Tamko limetolewa leo tarehe 22/12/2016 na;
Kajubi Mukajanga,
Mkurugeniz Mtendaji-MCT

Deogratius Nsokolo,
Rais Umoja wa Vilabu vya Waandishi Tanzania-UTPC

Onesmo OlengurumwA,
Mratibu Taifa-THRDC

C & P

No comments: