Monday 23 January 2017

Mikataba 9 Iliyosainiwa na Serikali ya Tanzania na Uturuki Leo

Na Beatrice Lyimo-MAELEZO

Serikali ya Tanzania na Serikali ya Uturuki zimesaini mikataba tisa ya makubaliano ya kiuchumi inayolenga katika kuimarisha uhusiano na ushirikiano wa maendeleo baina ya nchi hizo.

Mikataba hiyo inahusisha sekta za uchukuzi, mawasiliano, habari, elimu, utalii, utafiti, viwanda, afya na ulinzi.

Akizungumza mara baada ya kusaini kwa mikataba hiyo  leo Ikulu Jijini Dar es Salaam, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John Magufuli alisema ujio wa Rais wa Uturuki na ujumbe wake ni kielelezo cha ukuaji wa mahusiano baina ya Tanzania na Uturuki katika nyanja ya biashara na kimaendeleo baina nchini hizo.

Rais Magufuli alisema katika mazungumzo yake aliyofanya na Rais Recep Erdogan kuhusu ujenzi wa Reli ya Standard Gauge nchini, alimjulisha kiongozi huyo kuwa miongoni mwa wakandarasi walioomba zabuni ya ujenzi wa reli hiyo kuwa ni kampuni kutoka Uturuki, hivyo endapo itashinda zabuni hiyo itasaidia kukuza uhusiano uliopo baina ya nchi hizi mbili.

Aidha, Rais Magufuli alisema kuwa, Serikali ya Tanzania inatarajia kuomba  mkopo kupitia Benki ya Exim ya Uturuki katika kujenga sehemu ya kipande cha ujenzi wa reli hiyo.

Rais magufuli alisema Tanzania inaendelea kunufaika na uwepo wa Shirika la Ndege la Uturuki kwa kufanya safari zake za moja wka moja kutoka nchini Uturuki, kwa kuwa utasaidia kuongezeka kwa idadi ya watalii nchini na hivyo kukuza uchumi wa nchi hizo.

Kwa upande wake Rais wa Uturuki, Recep Erdogan alisema kuwa uwepo wa mikataba hiyo baina ya Tanzania na Uturuki itasaidia kupata matokeo mazuri ya uhusiano pamoja na fursa mbalimbali za ushirikiano katika nyanja ya Kilimo, Utalii, Ulinzi, Reli ambazo zitawezesha kukuza uchumi wa mataifa hayo.

Rais Erdogan alisema kuwa Uturuki imelenga kukuza ushirikiano uliopo baina yake na  Tanzania kupitia makongamano ya wafanyabiashara yenye malengo ya kukuza uchumi, kuongeza ajira pamoja na kukuza ujasiriamali baina ya Tanzania na Uturuki.

“Kiwango cha Biashara ya uwekezaji katika nchi ya Uturuki ni Dola za kimarekani 150 ambapo lengo letu ni kufika Dola za kimarekani 500,” alisema Rais huyo.

Aidha Rais Erdogan alisisitiza kuwa kufanya kazi kwa pamoja kutasaidia nchi hizi kusonga mbele na kufanikiwa katika nyanja mbalimbali.

Nae Waziri wa Maliasili na Utalii Prof. Jumanne Maghembe alisema kuwa makubaliano ya mkataba baina ya Tanzania na Uturuki katika Sekta ya Utalii yatasaidia katika kutangaza vivutio vilivyopo nchini, kubadilishana wataalamu, kubadilishana taarifa na kuongeza idadi ya watalii nchini.

Prof. Magembe aliongeza kuwa makubaliano hayo yatakuza sekta ya utalii katika kuvutia uwekezaji wa katika maeneo ya hoteli, fukwe na mbuga za wanyama zilizopo nchini

No comments: