Friday 9 December 2016

M zee wangu Kilomoni nakukumbusha… ‘AKILI YA KUAMBIWA CHANGANYA NA YAKO’

Na John Joseph
TANGU naanza kupata uelewa wa kutambua vitu, nilizikuta Simba na Yanga zikiwa ni klabu kubwa na zenye mtaji mkubwa wa mashabiki japo wanachama ‘hai’ hawakuwa wengi.

Asikudanganye mtu hizi timu zinapendwa na Watanzania, ilifikia hatua kila Mtanzania ambaye anazaliwa na kuanza kupata ufahamu kama nilivyokuwa mimi ilikuwa ni lazima achague kuishabikia moja kati ya timu hizo mbili labda tu awe siyo mtu wa michezo.

Nikiwa mdogo hata mama yangu japo siyo mtu wa soka lakini alikuwa akishangilia moja ya timu hizo na kutaniana na baba yangu ilipotokea mmoja wao timu yake imefungwa.

Miaka ya zamani kuna matajiri wachache walitumia fursa ya klabu hizo kuwa na mtaji wa watu wengi kujineemesha binafsi kwa gia ya kuwa wadhamini au wafadhili. Lakini natambua kuwa wapo waliotoa fedha zao kwa mapenzi na hawakuwa na lengo la kuingiza kwa mlango wa nyuma.

Matajiri wengi walijineemesha kwa mlango wa nyuma na sisi tulishangilia bila kujua, leo hii matajiri wa kizazi cha sasa wanataka kuingia kwenye klabu hizo kujineemesha kwa mlango wa mbele au naweza kusema ni wa halali, tunaanza kuwapiga vita.

Yusuf Manji anaitaka Yanga lakini fitina anazokutana nazo anazijua yeye na watu wake wa karibu, Mohamed Dewji ‘Mo’ anataka kuwekeza ndani ya Simba, naye kama ilivyo kwa Manji anakutwa na yaleyale.

Najua hakuna biashara inayoanza kisha ikawa sahihi kwa kila kitu lakini tunatakiwa kujifunza kuwa dunia ya leo siyo ya mwaka 1993. Tunatakiwa kubadilika.

Kuwakosoa Manji na Mo inatakiwa iwe katika msingi wa kuwaonyesha njia sahihi ya kupita lakini kuwafanyia fitina ni kuzihalalisha Simba na Yanga kuendelea kuishi kimasikini wakati zinao uwezo wa kujitoa kwenye tabia ya kuombaomba.

Wazee wetu walipambana kweli kuzifikisha hapo zilipo Simba na Yanga, lakini wanatakiwa wakubali kuwa hatuwezi kuishi maisha yaleyale kisa tu wakati timu hizo zinaanzishwa na kukuzwa hatukuwepo.

Dunia ya sasa soka ni biashara kubwa, idadi ya mashabiki au wanachama ndiyo mtaji wenyewe na ndiyo maana mabilionea wa Ulaya wanatoa fedha nyingi kuwekeza kwenye klabu, wanajua ili wao wapate faida ni lazima wazifanye timu zao zipate mafanikio.

Haki namba moja ya shabiki wa timu ni kushangilia na kuzomea, ndiyo maana shabiki anatoa kiingilio chake ili apate burudani ya kuzomea au kushangilia na hakuna anayejali nani anafanya nini nje ya hapo ilimradi timu iwe na maendeleo na yeye kiingilio chake kitendewe haki.

Wale mashabiki wanaoenda mbele zaidi na kuwa wanachama ni haki yao kuhoji masuala kadhaa ya kiutawala lakini yawe na hoja za msingi yenye kulenga kusaidia klabu na siyo kuifanya ibaki masikini kisha yeye huyohuyo awe analaumu kuwa klabu au timu yake haipati maendeleo.

Siku kadhaa zilizopita Simba iliitisha mkutano kwa mujibu wa katiba yao, moja ya hoja iliyopangwa ni kuhusu Mo kuwekeza klabuni hapo, wakati wanachama wakiusubiri mkutano huo anaibuka mzee wangu ambaye ni Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini wa Simba, Hamisi Kilomoni akidai hatambui mkutano huo.

Wanasema mtu mzima akikosea huwa hakosolewi hadharani lakini katika hili nalazimika kumwambia mzee wangu kauli ya kiutu uzima kuwa mara baada ya kumaliza kusoma makala haya, akirudi nyumbani, usiku wa leo wakati anajiandaa kuutafuta usingizi achukue dakika tano tu atafakari kwa umakini sana hiki alichotumwa kukizungumza kuhusu klabu yake, pia kabla ya kusinzia autafakari ule msemo wa ‘AKILI ZA KUAMBIWA CHANGANYA NA ZAKO’.

Msemo huo unaweza kuchukuliwa pia na wale wa Yanga wanaopinga uwekezaji wa Manji.

Kuna siku nilimsikia Katibu wa Baraza la Michezo la Tanzania (BMT), Mohamed Kiganja akisema kuwa kama matajiri hao wanataka kuwa na timu wakaanzishe timu zao.

Ni kauli ya kishabiki ambayo kwangu mimi haina mashiko, ukaanzishe timu Tanzania hii nje ya Simba na Yanga na utegemee ikuingizie kipato kikubwa! Inawezeka lakini siyo kwa sasa.

Azam FC ilianzishwa kwa uwekezaji mkubwa lakini bado ukweli ni kuwa kile kilichowekezwa na kinachoingia klabuni hapo ni vitu viwili tofauti, tusiwe wanafiki, huo ndiyo ukweli.

Awali Azam FC ilionekana imeanzishwa ili kuwa sehemu ya kutangaza bidhaa za mmiliki, baadaye malengo yalibadilika lakini kwa asili ya soka letu bado ipo chini ya vivuli vya wakongwe hao wawili.

Simba na Yanga ni mtaji mkubwa, zinatakiwa kuwa mfano, kisha nyingine ziige lakini kuacha mitaji hiyo iendelee kuwa masikini kisha nguvu kubwa itumike kuanzisha klabu nyingine ni kupoteza muda na hakuna anayeweza kufanya hivyo kwa sasa, tusidanganyane.

No comments: