Thursday 11 May 2017

Walimu Wawili Watiwa Mbaroni Jijini Dar Kwa Kuvujisha Mtihani wa Kemia wa kidato cha sita

Jeshi la  Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam, linawashikilia walimu wawili na mwanafunzi wa Shule ya Sekondari Chang'ombe (Mazoezi) kwa tuhuma za kukutwa na mtihani wa Kemia wa kidato cha sita. Mitihani hiyo inaendelea kufanyika nchini.

Kamishna wa Kanda hiyo, Simon Sirro, aliwataja watuhumiwa hao kuwa ni Musa Elius na Innocent Murutu ambao ni walimu wa shule hiyo. Mwanafunzi ni Ritha Mosha.

Kamishna Sirro alisema wiki iliyopita saa 1:00 usiku Jeshi la Polisi lilipokea taarifa kutoka kwa Ofisa wa Baraza la Mitihani, Aron Mweteni, aliyesema alimkuta kwenye shule hiyo mwalimu Elius na mtahiniwa Ritha wakiwa na karatasi yenye maswali na majibu ya somo la vitendo la kemia.

Alisema baada ya kuwatilia shaka na baadaye kuwatia mbaroni, walifanya ufuatiliaji wa awali kwa Baraza la Taifa la Mitihani (Necta) ambako ilibainika kuwa mtihani huo ni miongoni mwa ile ya kidato cha sita inayofanyika mwaka huu.

"Watuhumiwa wanaendelea kuhojiwa polisi na upelelezi ukikamilika tutawachukulia hatua za kisheria ikiwa ni pamoja na kuwafikisha mahakamani," Sirro alisema.

Katika tukio lingine, Kamishna Sirro alisema mvua zinazoendelea kunyesha jijini Dar es Salaam zimesababisha kifo cha mkazi wa Gulani Suka, Alice Genadi ambaye alitumbukia kwenye shimo la choo cha jirani yake ambacho kilikuwa kimejaa maji na hakikuwa kimefunikwa.

Kamanda Sirro alisema msichana huyo alikuwa akimfuata dada yake dukani.

Wakati huo huo, Jeshi hilo linawashikilia watuhumiwa wawili kwa kukutwa na vipande sita vya meno ya tembo.

Pia kamanda Sirro alisema wanawashikilia watuhumiwa watatu waliodaiwa kukutwa na lita 36,000 za gongo yenye thamani ya Sh. milioni 72.

No comments: