JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA
WIZARA YA MAMBO YA NDANI YA NCHI
JESHI LA POLISI TANZANIA
Ofisi ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Mbeya,
Namba ya simu 2502572 S. L. P. 260,
Fax - +255252503734 MBEYA.
E-mail:- rpc.mbeya@tpf.go.tz
tanpol.mbeya@gmail.com
TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 31.05.2017.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kufanya misako, operesheni na doria zenye tija katika maeneo mbalimbali ili kudhibiti uhalifu na wahalifu na limekuwa likishirikiana na wananchi na wadau wengine katika jitihada hizo za kukabiliana na uhalifu na wahalifu na kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kupungua kwa matukio makubwa ya uhalifu.
Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya pia linaongeza jitihada za kuzuia na kupunguza ajali za barabarani kwa kuhakikisha madereva na watumiaji wengine wa barabara wanatii sheria za usalama barabarani. Aidha kumekuwa na matukio 02 ya ajali za vifo kama ifuatavyo:-
Mnamo tarehe 29.05.2017 majira ya saa 20:30 Usiku huko Bagamoyo, Kata ya Bagamoyo, Tarafa ya Tukuyu Mjini, Wilaya ya Rungwe, Mkoa wa Mbeya katika barabara kuu ya Tukuyu – Mbeya, Gari isiyofahamika ikiendeshwa na dereva ambaye bado hajafahamika ilimgonga mtembea kwa miguu ambaye bado hajatambulika jina wala anuani yake mwenye umri kati ya miaka 25-30, jinsi ya kiume na kumsababishia kifo chake.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya wilaya ya Rungwe. Chanzo cha ajali mwendokasi. Upelelezi unaendelea ikiwa ni pamoja na kumtafuta dereva aliyehusika katika tukio hili.
Mnamo tarehe 29.05.2017 majira ya saa 21:00 Usiku huko Sinde, Kata ya Sinde, Tarafa ya Sisimba, Jiji na Mkoa wa Mbeya, Pikipiki yenye namba za usajili MC 458 BSW T-BETTER ikiendeshwa na dereva aliyetambulika kwa jina la GABRIEL GEOGRE [25] Mkazi wa Ghana Jijini Mbeya iligongana na Bajaji MC 634 BMS iliyokuwa ikiendeshwa na dereva aitwaye JACKSON SAMSON [23] Mkazi wa Iganzo na kusababisha kifo cha dereva wa pikipiki.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Rufaa Mbeya. Chanzo cha ajali ni mwendokasi wa Pikipiki. Bajaji imekamatwa na upelelezi kuhusiano na tukio hili unaendelea.
Mnamo tarehe 30.05.2017 majira ya saa 17:30 jioni huko katika Kijiji cha Msangamwelu kilichopo Kata Mjele, Tarafa Usongwe, Wilaya ya Kipolisi Mbalizi katika barabara kuu ya Mbalizi kwenda Mkwajuni, Pikipiki yenye namba za usajili MC 755 AMX T- Better iliyokuwa ikiendeshwa na PETER NASSON [21] Mkazi wa Ifumbo iliacha njia na kuanguka na kusababisha kifo cha mwendesha pikipiki huyo.
Aidha katika ajali hiyo, abiria wawili waliokuwa wamepakizwa walijeruhiwa ambao ni EMMANUEL SAILASI [14] Mkazi wa Ikukwa na GRIVATUS BAHATI [19] Mkazi wa Ufumbo, ambao wamelazwa Hospitali Teule ya Ifisi.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa Hospitali Teule ya Ifisi. Chanzo cha ajali ni mwendo kasi.
Mnamo tarehe 30.05.2017 majira ya saa 19:00 Usiku huko eneo la Igalako, Kata ya Mahongole, Tarafa ya Ilongo katika barabara ya Ilongo – Igalako, Pikipiki isiyofahamika usajili wake ambayo ilikuwa ikiendeshwa na dereva asiyefahamika iligongana na Pikipiki nyingine isiyofahamika usajili wake ikiendeshwa na dereva asiyefahamika na kusababisha kifo cha mtoto aitwae AGAPE DICKSON mwenye umri wa miezi 5 Mkazi wa Ituha jijini Mbeya na majeruhi kwa NEEMA JEROME [38] Mkazi wa Ituha Mbeya ambaye ni mama mzazi wa marehemu.
Mwili wa marehemu umehifadhiwa katika Hospitali ya Wilaya ya Mbarali. Madereva wote wawili walikimbia mara baada ya tukio hilo. Chanzo cha ajali ni mwendo kasi wa pikipiki zote mbili. Juhudi za kuwatafuta watuhumiwa waliohusika na tukio hilo zinaendelea/Upelelezi unaendelea.
WITO:
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi DHAHIRI A. KIDAVASHARI anatoa wito kwa madereva kuwa makini wanapotumia vyombo vya moto ikiwa ni pamoja na kufuata sheria na alama za usalama barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika. Pia kwa waendesha Pikipiki kuacha kupakia abiria zaidi ya mmoja [Mishikaki] kwani ni kinyume cha sheria na ni hatari kwa usalama wa abiria na dereva mwenyewe. Aidha anatoa wito kwa watembea kwa miguu kuwa makini wanapotembea barabarani ikiwa ni pamoja na kufuata/kuzingatia sheria na alama za barabarani ili kuepuka ajali zinazoweza kuepukika.
[DHAHIRI A. KIDAVASHARI - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA
No comments:
Post a Comment