Rais John Magufuli ameagiza kusimamishwa kazi kwa naibu kamishna wa
uhamiaji kwa tuhuma za kuingiza nchini humo raia 50 wa Somalia na kuwapa
vibali vya kuishi.
Kupitia waziri mkuu Kassim Majaliwa kiongozi huyo ametaka kusimamishwa
kazi mara moja kwa bi Grace Hokororo na kuundwa kwa tume itakayochunguza
utoaji wa vibali vya uraia nchini humo.
Kauli hiyo ilitolewa na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa mara baada ya
kumaliza kikao na Makamishna wa uhamiaji kilichofanyika katika makao
makuu ya uhamiaji jijini Dar es salaam.
Tayari Majaliwa amemuagiza waziri wa mambo ya ndani Mwigulu Nchemba kubuni tume hiyo ya uchunguzi.
Amesema kuwa haiwezekani raia wa kigeni kuingizwa nchini humo na baadaye
kupewa vibali vya kuishi bila ya kufanyiwa uchunguzi wa kina.
"Idara ya Uhamiaji tunaitegemea kusimamia mipaka yetu na kuziba mianya
ya watu kuingia bila ya kufuata taratibu lakini kwa mapenzi yake Ofisa
huyu ameruhusu Wasomali kuingia bila kufuata taratibu."
Waziri Mkuu amesema ni lazima uchunguzi ufanyike ili kubaini ni kitu
gani kilichomsukuma kuwapatia vibali Wasomali hao ambao hawakuwepo
nchini.
''Wameingia na kupewa vibali moja kwa moja kwa mapenzi yake tu sasa hii ni dosari hatuwezi kuivumilia."
Amesema Serikali inaitegemea Idara ya Uhamiaji kwa kuzuia mianya ya
uingiaji raia mbalimbali kutoka nje ya nchi bila ya kufuata taratibu.
"Hawa Wasomali aliowapa vibali vya kuishi wala hawakuwa wanaishi nchini
wameingia tu na kupewa vibali, hivyo Mheshimiwa Rais Dkt. John Magufuli
ameagiza ofisa huyo akae pembeni na achunguzwe ili kujua ni kitu gani
kilimsukuma kutoa vibali kwa raia hao."
Pia majaliwa ameiagiza idara ya Uhamiaji kudhibiti kitengo cha utoaji
hati za kusafiria za Kibalozi na kwa wanaomaliza muda kutopewa tena.
" Lazima hati hizo zikaguliwe katika mipaka yote na maeneo yote ya
usafiri ili kujua kama huyo anayeitumia bado anahadhi hiyo na
msiporidhika ichukuweni kwani kuna watu wanazitumia vibaya."
Hata hivyo Waziri Mkuu ameagiza uchunguzi wa kina ufanyike kwa watu wote
walioomba hati za kusafiria pamoja na vibali vya makazi iwapo wanakidhi
matakwa ya kisheria kabla ya kuwakabidhi.
No comments:
Post a Comment