Mwenyekiti Kamati ya Uongozi katika Chama cha Wananchi (CUF), Julius
Mtatiro, amesema kuwa Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Mhe. Tundu
Lissu, atarejea kwa nguvu zote na kwa kishindo kizito.
Mtatiro amesema hayo kupitia ukurasa wake wa Facebook kwa kuandika
machache baada ya kumtembelea Mhe. Lissu hospitali Jijini Nairobi
anapoendelea na matibabu baada ya kushambuliwa kwa kupigwa risasi na
watu wasiofahamika Septemba 7, mwaka huu akiwa nyumbani kwake Area D,
Mkoani Dodoma.
Mtatiro ameandika yafuatayo;
“SALAMU KUTOKA NAIROBI.
Mtatiro. J
Hapa jijini Nairobi leo nimepata fursa ya kumtembelea na
kuzungumza kwa kirefu na ndugu yetu Tundulissu. Kama kuna mtanzania
imara, asiyeogopa na mwenye maono makubwa ni Lissu. Lissu hana wasiwasi
and he will strike hard very soon!
Risasi zote zilizopenya kwenye mwili wa Lissu zimemtengenezea
uimara maradufu, mara sabini, mara mia moja. Waliodhani kuwa kumuua
Lissu ndiyo kuua harakati za Watanzania kudai taifa la haki na
linalofuata misingi ya sheria na katiba bora, wanajidanganya.
Lissu ameniambia “Mtatiro nenda kawaambie kuwa nitarudi nikiwa
mzima na tutaendelea na mapambano maradufu zaidi, faraja muhimu
nayohitaji kutoka kwa Watanzania hivi sasa ni kuendeleza mapambano ya
kudai haki na kupambana na udikteta, tusikubali nchi yetu iharibiwe na
kikundi cha watu wanaoogopa kukosolewa”
Nimemwambia Lissu fikra zangu, kuwa “..siku nilipotaarifiwa kuwa
umepigwa risasi nyingi ikiwa ni njia ya kukuua, nilitabasamu, nilijua
mapambano ya kudai haki yamekolea, nilijua umekuwa imara mno maishani
mwako na kwamba mateso utakayopitia yatakujenga na yatatujenga sisi
zaidi!”
Mimi binafsi kama Mtatiro, kumuona Lissu kumenijenga zaidi,
kumenifundisha kuwa ukipigwa risasi hata 100 kwa sababu u mkosoaji wa
watawala yapo mambo mawili yatatokea, aidha utapona kama Lissu au
utakufa kama ilivyowatokea wapigania haki wengi.
Uki-survive kama Lissu jambo moja litatokea, utaungana na
wananchi wote kupigania haki kwa nguvu kubwa zaidi. Ukiuawa kwa risasi
kama wapigania haki wengi jambo moja kubwa litatokea, kifo chako
kitapandikiza mbegu kubwa ya ukombozi, kifo chako kitaliamsha taifa
kupigania haki na kupambana na madikteta wajinga.
Kama wapuuzi waliomshambulia Lissu walidhani kuwa wanatutisha,
kutuogofya na kuturudisha nyuma, wanajidanganya. Wanatuandaa kimwili na
kiroho kulipigania taifa na kupambana kudai utawala wa haki, utawala wa
sheria na katiba bora. Wanatuandaa kujitolea maisha yetu kwa ajili ya
Taifa.
Nataka kuwaambia watanzania kuwa nchi yetu siyo Rwanda, siyo
Burundi, siyo Congo wala siyo Uganda. Zipo njia zilitumika kuwazoesha
Wanyarwanda, Warundi, Waganda na Wakongo udikteta. Kama yupo mtu
anadhani anaweza kuipeleka Tanzania udiktetani anajidanganya.
Tutalipigania taifa letu, utu wetu na uhuru wetu wa kuzaliwa bila
kuogopa mikanda ya risasi.
Salamu kutoka Nairobi, he is going to strike soon and we will strike with him, harder and harder!
#Mtatiro J,
Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi,
The Civic United Front (CUF),
08 Oktoba 2017 – Nairobi, Kenya.”
No comments:
Post a Comment