Thursday 12 October 2017

Walichoongea Mtukufu Aga Khan na Rais Magufuli Ikulu


Kiongozi wa Jumuiya ya Ismailia, Mtukufu Aga Khan amesema  wamedhamiria kuunga mkono juhudi za Serikali kwa kupanua hospitali.

Amesema Hospitali ya Aga Khan jijini Dar es Salaam itapanuliwa na pia watajenga chuo kikuu kikubwa katika ukanda wa Afrika Mashariki mkoani Arusha.

Mtukufu Aga Khan amesema hayo jana Jumatano Ikulu jijini Dar es Salaam, alipofanya mazungumzo na Rais John Magufuli.

Alisema upanuzi wa hospitali utahusisha kuongeza idadi ya vitanda vya wagonjwa kutoka 72 vya sasa hadi 172, kuimarisha matibabu ya moyo na saratani.

Taarifa ya Ikulu kwa vyombo vya habari imesema upanuzi wa hospitali pia utahusisha ufundishaji wa madaktari na wataalamu wengine wa afya.

Kuhusu chuo kikuu, Mtukufu Aga Khan alisema jumuiya imedhamiria kujenga kikubwa ambacho kitafundisha viongozi si tu wa Tanzania na Afrika Mashariki, bali Afrika nzima ili wawe chachu ya mabadiliko na maendeleo.

Rais John Magufuli katika taarifa hiyo alimshukuru Mtukufu Aga Khan kwa taasisi zake kutoa huduma za kijamii nchini Tanzania.

Alitoa wito kwa taasisi hizo kupunguza gharama za huduma ili wananchi wamudu na hasa ikizingatiwa kuwa zimekuwa zikipata msamaha wa kodi kutoka serikalini.

Rais Magufuli alisema Serikali ipo tayari kuendeleza na kuimarisha ushirikiano na Aga Khan na amemuomba kiongozi huyo wa dini kuendelea kupanua wigo wa huduma za taasisi zake ikiwa ni pamoja na kuwekeza mjini Dodoma yaliko makao makuu ya Serikali.

No comments: