MFANYABISHARA Timotheo Wandiba amehukumiwa kifungo cha miaka 81 jela baada ya kupatikana na hatia katika mashtaka 27 yaliyokuwa yakimkabili ya kujipatia Sh.bilioni 2.1 kwa njia udanganyifu.
Aidha, Mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa Dickson Okololo na Simon Efrem waliokuwa wakishtakiwa na Wandiba baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuthibitisha mashtaka dhidi yao pasipo kuacha shaka.
Akisoma hukumu hiyo, Hakimu Mkazi Mkuu Wilbard Mashauri, kwa niaba ya Hakimu Joyce Minde aliyeandika hukumu hiyo, amesema upande wa mashtaka kupitia mashahidi 14 imethibitisha makosa yote 82, kuwa mshtakiwa alitenda kosa.
Katika makosa hayo 82, mashtaka 27 ni ya kughushi, 27 ya kutoa nyaraka za uongo, 27 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu na Moja la utakatishaji fedha.
Hakimu Mashauri amesema Mahakama hiyo imemtia hatiani mshtakiwa Wandiba katika makosa 27 ya kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu, baada ya kuridhishwa na ushahidi uliotolewa na mashahidi wa upande wa mashtaka.
Hakimu Mashauri amesema katika makosa hayo 27, katika kila kosa mshtakiwa Wandiba atatumikia kifungo cha miaka 3 jela, mbapo jumla itakuwa ni miaka 81, lakini vifungo hivyo vitaenda kwa pamoja, hivyo atatumikia kifungo cha miaka mitatu tu gerezani.
Aidha Hakimu Mashauri amesema Mahakama hiyo imewaachia huru washtakiwa Okololo na Efrem katika makosa mengine yote baada ya upande wa mashtaka kushindwa kuyathibitisha pasipo kuacha shaka yoyote.
Katika shtaka la kujipatia fedha kwa njia ya udanganyifu ambalo limemtia hatiani Wandiba, inadaiwa kati ya Desemba 3, mwaka 2012 na Februari 5,mwaka 2013, Dar es Salaam mshtakiwa alijipatia Sh.119,039,398.96 kutoka Benki ya Africa (BoA) kwa njia ya udanganyifu.
Pia wanadaiwa kughushi fomu za makubaliano ya kuhamisha fedha kutoka Benki ya BOA ikionyesha akaunti ya Sogea Sauthom imeiomba benki hiyo kuilipa akaunti ya Tracom Sh 2,119,039,398.96.
Katika shtaka la utakatishaji fedha, inadaiwa walilitenda kati ya Desemba 4, 2012 na Aprili 30, mwaka 2014 walijipatia Sh.2,119,039,398.96 kutoka akaunti ya Sogea Sauthom katika benki ya (BoA) kwenda akaunti ya Tracom NMB tawi la Ban House wakati wakijua fedha hizo ni zao la uhalifu la kosa la kughushi.
Hata hivyo, upande wa mashtaka umesema haujaridhishwa na uamuzi uliotolewa na mahakama na watakata rufaa.
No comments:
Post a Comment