Monday 5 March 2018

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI WAKIWA NA SILAHA.

                                                                                  
                                                       
TAARIFA YA JESHI LA POLISI MKOA WA MBEYA KWA VYOMBO VYA HABARI “PRESS RELEASE” TAREHE 05.03.2018.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya limeendelea kukabiliana na vitendo vya uhalifu ili kuhakikisha kuwa wageni na wakazi wa Mkoa huu wanaendelea kuwa salama na mali zao. Aidha Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya linaendelea kushirikiana na wananchi na wadau wengine wa usalama hali inayopelekea kupata mafanikio makubwa ikiwa ni pamoja na kukamata watuhumiwa mbalimbali wa uhalifu, silaha na vifaa mbalimbali vya kutengenezea silaha.

KUKAMATWA KWA WATUHUMIWA WA TUKIO LA MAUAJI WAKIWA NA SILAHA.

Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya mnamo tarehe 03.03.2018 majira ya saa 18:30 jioni liliendelea na msako mkali uliofanyika huko maeneo ya Itezi – Uyole, Kata ya Itezi, Tarafa ya Iyunga hapa Jijini Mbeya na kufanikiwa kuwakamata watu watano [05] wakiwa na Silaha bunduki aina ya Pump Action Shortgun yenye namba 009009906-MP-18EM-M mali ya SUMA JKT ikiwa imefichwa nyumbani kwenye Stoo ya kuhifadhia vitu mbalimbali.

Watuhumiwa waliokamatwa wamefahamika kwa majina ya:-

HAMIS SHABAN [19] Mkazi wa Itezi
IBRAHIM MBILINYI [22] Mkazi wa Itezi
STAN WEMA [21] Mkazi wa Uyole
BAHATI LAULENDI [22] Mkazi wa Iduda
SAMBAA SAMSON [32] Mkazi wa Isyesye

Watuhumiwa baada ya kupekuliwa walikutwa na silaha nyingine ambazo ni:-
Mapanga matatu [03].
Maganda matatu tupu ya risasi



Mnamo majira ya saa 01:30 usiku wa kuamkia tarehe 26.02.2018 huko maeneo ya Kituo cha Mafuta kiitwacho MANYANYA kilichopo Uyole, Kata ya Nsalaga, Tarafa ya Iyunga, Jijini Mbeya, watu wasiofahamika majina walimvamia mlinzi wa SUMA JKT aitwaye CHEWE WILSON [34] Mkazi wa Iduda, Mlinzi wa Suma JKT akiwa lindoni katika Kituo cha mafuta cha MANYANYA kilichopo Uyole na kisha kumjeruhi mlinzi huyo kwa kumkata kwa panga sehemu za kichwani na mguu wa kulia na kisha kumpora silaha bunduki aina ya Shortgun mali ya SUMA JKT na kutoweka nayo.

Na mnamo tarehe 01.03.2018 majira ya saa 06:00 asubuhi CHEWE WILSON [34] alifariki dunia akiwa anaendelea kupatiwa matibabu katika Hospitali ya Rufaa Mbeya kutokana na majeraha aliyoyapata sehemu ya kichwani na mguu wake wa kulia.

Kutokana na tukio hilo, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lilifanya msako mkali na kufanikiwa kuwakamata watuhumiwa watano [05] ambao baada ya kuhojiwa wamekiri kuhusika katika tukio hilo. Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara baada ya Upelelezi kukamilika.

KUKAMATWA WATUHUMIWA WAWILI WAKIWA NA SILAHA [GOBORE].

Mnamo tarehe 03.03.2018 majira ya saa 12:00 mchana, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya liliendelea na misako mikali katika maeneo mbalimbali ya Mkoa wa Mbeya. Katika msako uliofanyika huko Kitongoji cha Kibaoni, Kijiji na Kata ya Kambikatoto, Tarafa ya Kipembawe, Wilaya ya Chunya, Jeshi la Polisi lilifanikiwa kuwakamata watu wawili wakiwa na bunduki aina ya Shortgun iliyotengenezwa kienyeji pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengenezea bunduki.

Watuhumiwa waliokamatwa wamefahamika kwa majina ya:-
FADHILI MAYEGA [60] Mkazi wa Kambikatoto
MASHAKA SAMWEL [38] Mkazi wa Kambikatoto

Aidha baada ya watuhumiwa kupekuliwa walikutwa na bunduki hiyo pamoja na vifaa mbalimbali vinavyotumika kutengenezea bunduki aina ya shortgun za kienyeji ambavyo ni:-
Mkono wa kuwekea risasi kwenye bunduki [Cocking Handle]
Unga wa Baruti wenye uzito wa gramu moja.
Mafuta ya kusafishia bunduki
Risasi 25 zilizotengenezwa kienyeji
Tupa 10
Chuma kimoja cha kukatia risasi
Tindo za kukatia mawe
Vipande vya vyuma viwili [02]
Visu vitano [05]

Nyundo kubwa mbili.
Praise moja
Bisibisi moja
Mguu wa Pedal ya Baiskeli
Triger 2

Watuhumiwa watafikishwa Mahakamani kwa hatua zaidi za kisheria mara tu baada ya upelelezi kukamilika.

WITO:

Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mbeya Naibu Kamishina wa Polisi MOHAMMED R. MPINGA anatoa wito kwa vijana na jamii kwa ujumla kuacha tamaa ya kupata mali kwa njia zisizo halali kwa kujihusisha na vitendo vya uhalifu kwani ni kinyume cha sheria na badala yake wajishughulishe na kazi halali kwa ajili ya kujipati kipato. Aidha Kamanda MPINGA anatoa onyo kali kwa yeyote atakaye jihusisha na uhalifu, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mbeya lipo imara kuhakikisha usalama wa raia na mali zao na halitasita kumkamata na kumfikisha Mahakamani mtu/watu au kikundi cha watu watakaojihusisha na uhalifu kwa hatua zaidi za kisheria. Pia Kamanda MPINGA anaendelea kuomba ushirikiano kwa raia wema, viongozi wa mitaa kuendelea kutoa taarifa kwa Jeshi la Polisi ili wahusika wakamatwe na kuchukuliwa hatua za kisheria.

             Imesainiwa na:         
[MOHAMMED R. MPINGA - DCP]
KAMANDA WA POLISI MKOA WA MBEYA

No comments: