Sunday 1 September 2013

MULUGO ATAHADHARI​SHA MATUMIZI MABAYA YA SIMU NA MITANDAO


3 ad63f
Elizabeth Thomas (aliyeshika kipaza sauti) kutoka Halmashauri ya Manispaa ya Ilala akimueleza Naibu Waziri Mulugo kuhusu Tamasha la Mnazi Mkinda linaloandaliwa na halmashauri hiyo kuboresha sekta ya elimu katika eneo hilo
hdg

NAIBU Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Philip Mulugo ameitaka jamii kupiga vita matumizi mabaya ya simu za mikononi, kompyuta na mitandao ya kijamii yenye muelekeo hasi kwa mustakbali wa taifa la Tanzania.
Waziri Mulugo ameyasema hayo wakati akizindua maonesho Vodacom Elimu Expro 2013 yaliyofanyika kwenye viwanja vya Posta Kijitonyama jijini Dar es Salaam mwishoni mwa wiki iliyopita.
Lengo la maonesho hayo ni kuboresha utoaji wa huduma mbalimbali za kielimu miongoni mwa wanafunzi, walimu, wakufunzi,wahadhiri na jamii nzima ujumla kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Alitoa wito kwa wazazi, walezi na jamii yote kutumia teknolojia ya elimu masafa na mitandao kwa matumizi mazuri ya kupata taarifa za kitaaaluma na kimaendeleo bila kuangalia mitandao ambayo watu wengine hutukana matusi ya nguoni, kuangalia picha ngono na mambo mengine yenye muelekeo hasi.
"Tunasema ni jukumu letu sisi sote kulinda mila na desturi zetu kama Watanzania pamoja na maadili ya watoto wetu na vizazi vyetu kama nchi yetu ya Watanzania ilivyo, taarifa zinazowekwa kwenye mtandao ziwe sahihi ili zisiwapotoshe watoto na vijana kwenye shule na vyuo vikuu." alisema Waziri Mulugo.
Akifafanua kuhusu suala la wanafunzi kuwa na simu, Waziri Mulugo alisema si kosa kwa mwanafunzi kuwa na simu maadam anaitumia kwenye matumizi chanya.
"Lakini asiingie na simu darasani na mimi nitakuwa mtu wa kwanza nikimkuta mwanafunzi ana simu namnyang'anya ili tuweze kuwajenga watoto kwenye maadili kwa sababu wanatumia simu kwenye matumizi hasi, ujumbe wa kimapenzi, mitandao ya picha za ngono n.k"alisema Waziri Mulugo na kuongeza:
"Sisi kama Serikali tunalinaoinda maadili ya watoto hatuwezi kuruhusu jambo hili kwa hiyo naomba mwanafunzi anapotumia simu atumie kwa matumizi chanya, aangalie 'material' kama ambavyo nia ya maonesho ya leo yalivyo, tusipotoshe umma"
Akizungumzia lengo la maonesho hayo na malengo ya Serikali, Waziri Mulugo alisema kuwa Tanzania inahitaji elimu bora tena kwa nguvu sana kwani kuna shule nyingi, vyuo vikuu na vya kati vimeanzishwa, hivyo ni lazima wanafunzi wapate taarifa kamili tena zilizo sahihi na zinazoeleweka.
Alisema katika ulimwengu wa utandawazi hakuna budi kutumia TEHAMA ili kujiletea maendeleo endelevu katika sekta mbalimbali na kampuni za mawasiliano na vyombo vya habari vina mchango mkubwa katika kufanikisha hilo.
"Ninyi mlioandaa jambo hili ni lazima mfanye utafiti na nyinyi mnaoonesha maonesho haya ni lazima mshirikiane na Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi ili kutoa taarifa sahihi kwa Watanzania" alisema Waziri Mulugo.
Aliongeza kwa kuwataka kuwa kabla hawajaingiza mambo kwenye mitaandao na kwenye kompyuta aliwaomba waingize taarifa zilizo sahihi kwani Vodacon Elimu Expro 2013 imelenga kuwafaidisha wanafunzi, walimu na wadau wote wa elimu kupata taarifa mbalimbali za kimasomo kwa njia ya elimu masafa
Alibainisha kuwa Serikali ipo katika hatua za mwisho kutengeneza mkongo wa taifa utakaounganisha upatikanaji wa mtandao kwa nchi nzima na kuahidi kuwa wizara yake kupitia mpango wa Tanzania Beyond Tomorrow itashirikiana na kampuni mbalimbali ya mawasiliano katika kuboresha elimu masafa.
Maonesho hayo yenye lengo la kuboresha elimu ya Tanzania yamedhaminiw na Vodacom na iliandaliwa na kampuni ya Masoko Agency kwa kushirikiana na kampuni ya Elimu Solutions, ambapo wanafunzi wanapata fursa ya kulipa ada kupitia M-PESA na NMB Mobile na kukopa mikopo benki

No comments: