Tuesday 1 April 2014

BIASHARA YA POMBE AINA YA VIROBA YA PAMBA MOTO MBEYA

Na Eliud Ngondo, Mbeya

LICHA ya Serikali kukataza uingizaji wa pombe halamu kutoka nchi
jilani za Malawi na Zambia maarufu kama viroba hatimaye wananchi
wamezidi kuziingiza pombe hizo na kutapakaa jijini Mbeya.

Uchunguzi uliofanywa na Mtandao huu Mkoani Mbeya umebaini kuwa pombe
hizo zimekuwa  zikiingizwa kwa njia za panya kupitia vivuko visivyo
halali Wilayani Kyela na kusafirisha hadi jijini Mbeya ambako
imeonekana kuwa ndiko kuna watumiaji wengi wa pombe hizo.

Katika wilaya ya Kyela wafanyabiashara wa pombe hizo wamekuwa
wakisafirisha mithili ya gunia la Mchele, juu yake wakiwa wamejaza
maharage na wengine huweka dagaa za Nyasa ili vyombo husika visiweze
kubaini kilichomo ndani yake.

Imebainika pia kuwa wafanyabiashara hao wamekuwa wakipitisha pombe
hizo katika Wilaya ya Ileje kwa kutumia Baiskeli na kuziingiza nchi
kupitia eneo la Mbebe, Msia, Mapogolo, Ikumbilo, Bupigu, Ilondo na
Ilulu.

Wakizungumza na Mwandishi wa habari baadhi ya wafanyabiashara wilayani
Ileje wamesema kuwa biashara ya viroba kutoka nchi jirani za Malawi na
Zambia inawalipa sana kutokana na bei zao kuwa ndogo licha ya
kusafirisha kwa gharama ukilinganisha na viroba vya hapa nchini.

Wafanyabiashara hao ambao waliomba hifadhi ya majina yao wamesema kuwa
mfuko wa viroba 300 wananunua kwa bei ya shilingi 40000 kwa bei ya
jumla kutoka Malawi wakati wao wanauza kwa bei ya shilingi elfu 60000.

Hata hivyo walidai kuwa wakati mwingine wanauza kwa bei ya reja reja
ambapo kiroba kimoja kinauzwa kwa bei ya shilingi 250 -300 jambo
ambalo walisema kuwa inawanufausha sana kuliko viroba vya hapa nchini.

Waliongeza kuwa viroba hivyo vimekuwa vikipendwa sana na watumiaji
wakitanzania kutokana na bei zake kuwa ndogo ambapo walisema kuwa
zinaendana na uchumi walionao kwani watumiaji hao hutumia gharama
ndogo ukilinganisha na viroba vya Konyagi na Varue.

Walisema kuwa viroba vya hapa nchini vinauzwa kwa bei ghari ndiyo
maana walio wengi hawapendi kuvitumia kwani kiroba kidogo kinauzwa kwa
bei ya shilingi 600-700 wakati vikubwa vinauzwa kwa bei ya shilingi
1200-1500.

Aidha walisema kuwa viroba vya Bwenzi Charger, Raider, Boss na Power
No 1 vikubwa vinauzwa kwa bei ya shilingi 400-500 jambo ambalo
linawafanya watanzania wengi kukimbilia kuvinunua kuliko vya hapa
nyumbani.

Akizungumzia kuhusu uingizwaji wa pombe hizo Meneja wa Mamlaka ya
chakula na dawa (TFDA) Mkoa wa Mbeya Rodney Alananga amesema kuwa
kunachangamoto kubwa kuweza kuzuia uingizwaji wa pombe hizo nchini.

Alananga alisema kuwa suala la viroba linapaswa kushughulikiwa na
wananchi kwa pamoja ili kuweza kutokomeza uingizwaji huo kwani kuachia
vyombo husika haviwezi kutekeleza kwa muda mfupi.

Meneja huyo alisema kutokana na uhatari wa viroba hivyo kwa afya za
watumiaji serikali ya Mkoa wa Mbeya imeunda kikosi maalumu kwa ajili
ya kufanya operesheni kubwa ambapo kila atakaye bainika atachukuliwa
hatua kali za kisheria.

Alisema kuwa Mkuu wa mkoa wa Mbeya Abass Kandolo kwa kushirikiana na
vyombo vya ulinzi na Mamlaka husika wako katika hatua za mwisho kuanza
kwa operesheni hiyo ya kukamata wale wote wanaouza viropba hivyo.

Aliongeza kuwa wananchi wanapaswa kutoa ushirikiano na Mamlaka yake
kwa kutoa taarifa wale wote wanaoingiza viroba kwa njia za magendo
ikiwa ni pamoja na kutoa mianya inayotumika katika usafirishaji wa
pombe hizo halamu.

Aidha alisema kuwa kutokana na kuwepo kwa vivuko vingi Wilayani Kyela
serikali inakusudia kusajiri vivuko hivyo ili kudhibiti uingizwaji
holela wa pombe hizo pamoja na baadhi ya bidhaa nyingine kutoka nchi
hizo.

Alisema kuwa viroba vingi kutoka nchi jirani za Malawi na Zambia
havijathibitishwa na mamlaka husika kama vile TBS hivyi ni hatari kwa
watumiaji kwani havina uora wa viwango vinavyotakiwa kutumia.

No comments: