Wakazi wa jiji la Nairobi wakienda makazini kwa miguu asubuhi hii kufuatia mgomo wa matatu. Picha kwa hisani ya Daily Nation
Na Fadhy Mtanga
WAKAZI wa
jiji la Nairobi nchini Kenya wameonja joto ya jiwe asubuhi hii baada ya
kulazimika kwenda makazini na maeneo mengine kwa miguu kufuatia mgomo
mkubwa wa madereva wa usafiri wa umma, maarufu kama matatu.
Madereva
hao waliamua kuifunga barabara ya Thika karibu na daraja la waenda kwa
miguu la Pangani. Kisa cha kadhia hiyo ni kuongezeka kwa gharama ya
kupaki jijini hapo.
Gazeti la
Daily Nation la nchini humo limeripoti kuwa madereva hao waliyaweka
magari yao kwenye mzunguko mkubwa wa Donholm na kuwalazimisha wakazi wa
jiji hilo kutumia barabara ya Jogoo ili waweze kufika makazini ama
maeneo mengine kadri ya mahitaji yao.
Mkuu wa
kitengo cha usalama barabarani Nairobi amesema polisi wamefanya jitihada
kubwa ili kuweza kuzifungua barabara za Jogoo, Thika na Donholm
kufuatia madereva kuweka vizuizi asubuhi ya leo.
Adha hiyo pia imewafanya wakazi kadhaa kuporwa vitu vyao na vibaka huku wakiilalamikia mamlaka husika kwa kuchangia kadhia hiyo.
Chama cha wafanyabiashara jijini hapo, Nairobi Metropolitan
Union kimemtaka Gavana kushusha gharama hizo. Waendeshaji hao wa matatu
wanataka gharama kwa matatu ya abiria 14 kushushwa hadi shilingi za
Kenya 3,650 kutoka shilingi 5,000, huku zile za abiria 41 zikishushwa
kutoka shilingi 8,000 hadi 5,000.
Tayari mamlaka za kaunti zimeridhia madai hayo.
No comments:
Post a Comment