Simba iliongeza 'gepu'
la pointi baina yake na Azam FC, katika msimamo wa ligi kuu Bara, baada
ya kuifunga timu hiyo iliyokuwa haijapoteza mchezo wowote katika ligi.
John Bocco alifunga mapema tu, dakika ya nne ya mchezo huo, lakini,
Felix Sunzu, aliisawazishia timu yake dakika tatu baadaye, kabla ya
Emmanuel Okwi kufunga mara mbili na kutengeza pengo la pointi nne baina
yao, huku, Azam ikilala kwa mara ya kwanza baada ya kukubali kipigo cha
mabao 3-1.
Iliingia katika mchezo huo ikiwa na
presha ya kuhakikisha ni lazima washinde, baada ya sare tatu mfululizo,
wapenzi, wanachama na mashabiki wa timu hiyo waliingia katika presha ya
kuushinikiza uongozi wao wa juu kuitisha mkutano wa dharura. Wachezaji
kadhaa wakaondolewa kikosini kwa sababu mbalimbali, Haruna Moshi,
akasimamishwa kwa siku 21, Juma Nyosso, akapelekwa kikosi B, akaimarishe
kiwango chake. Wengi wakataka kuona itakuwaje katika mchezo wa jana,
kocha, Milovan Curkovic, akawa na jibu.
Urejeo wa mchezaji, Shomari Kapombe
katika safu ya ulinzi wa kati ilionekana ni nafuu zaidi kuliko kama
angetumika mchezaji mwingine yoyote katika nafasi hiyo ndani ya Simba,
aliweza kucheza vizuri na kuhakikisha njia zote ambazo viungo wa Azam
FC, huwa huwatengenezea nafasi washambuliaji wao, John Bocco na Kipre
Tcheche, hazionekani. Kapombe alicheza kama namba nne sahihi, na kuna
wakati akawa akijibadilisha na kuwa namba sita 'kivuli', alimzima
kabisa, Bocco hasa baada ya mshambuliaji huyo wa Azam, kufunga mwanzoni
tu mwa mchezo. Wakati mzuri zaidi kwa, Simba jana ilikuwa ni pale
walinzi hawa wawili wa kati ( Paschal Ochieng na Kapombe) walipokuwa
wakibadilishana majukumu kwa namna washambuaji, Kipre na Bocco, walivyokuwa wakijaribu kujibadilisha zaidi kutoka washambuliaji hadi
kuwa viungo washambuaji, lakini walizimwa na Simba ikaonesha uwezo wa
juu kuanzia katika mikono ya Kipa, Juma Kaseja hadi safu ya ulinzi.
Ushindi wa Simba ilikuwa ni walinzi hawa kwa kushirikiana na wale wa
pembeni, Nassorro Chollo na Amir Maftah wakiwazima wafungaji bora wa
Azam, Bocco mwenye mabao manne na Kipre mwenye mabao matano.
Waliiingia huku
wakiamini matatizo makubwa yaliyopo ndani ya timu ya Simba yatawasaidia
kuondoka na ushindi 'mnono' na mara baada ya kupata bao la kuongoza
kabla ya hata dakika ya tano, Azam wakaamini, Simba inafungika. Wakajiamini
zaidi, kuliko walivyokuwa wakijiamini awali. Lilikuwa kosa, wakasahau
kuwa wanacheza na timu kubwa nchini, wakasahau kuwa wanacheza na Simba
ambayo ndiyo bingwa mtetezi wa ligi kuu. Ili kuwa bingwa wa michuano
yoyote ile ni lazima kwanza uzifunge timu ambazo unagombea nazo ubingwa
wa michuano husika. Msimu uliopita kama, Azam ingeshinda walau mchezo
mmoja tu dhidi ya Simba, bila shaka yoyote
wangekuwa mabingwa wa ligi kuu. Wakati wakimaliza msimu wakiwa pointi
tatu pungufu dhidi ya Simba, Azam wangenufaika sana kama wangepata
pointi mbele ya Simba, lakini walishindwa.
Uwezo wao mdogo wa kiufundi katika
michezo mikubwa umeendelea kuwasumbua. Katika mchezo wa jana, Azam
ilikuwa katika ' shepu nzuri ya mchezo kuliko Simba' lakini Simba
walitumia kila wanaloweza kuhakikisha hawapotezi mchezo huo, kwani
walitambua wazi kuwa endapo watafungwa watawaacha wapinzani waende juu
yao kwa tofauti ya pointi moja zaidi uku wakiwa na mchezo mmoja mkononi.
Lakini wakati, wenzao wakijiamini zaidi, Simba waliendelea kutafakari
kwa kina matukio yote ambayo yametokea ndani ya klabu yao ndani ya wiki
nzima, na wachezaji wakaingia huku
wakijua fika wanakwenda kucheza mchezo mgumu, lakini ili kutuliza mambo
ni lazima washinde. Azam ilikuwa na viungo wanne wazuri katikati ya
uwanja. Abdulhalim Humud, Jabir Aziz, Himid Mao, na Salum Abubakary,
lakini wachezaji hawa ambao wamekuwa ni silaha ya kujihami ya timu hiyo
walijigeuka kutoka viungo wachezesha timu bora hadi kuwa viungo
'wachapa viatu' bora, walionekana kukosa ubunifu mbele ya Amri Kiemba,
Jonas Mkude na Mwinyi Kazimoto, ambao wao waliamua kujiondoa katika
utamadauni wa Simba wa mchezo wa pasi fupi fupi hasa wakianzia nyuma na
kusogea na mpira, na Simba ikaamia katika mchezo wa mipira mirefu,
Mwinyi akawa anapiga pasi ndefu, Kwa Mrisho Ngassa upande wa pembeni, au
kwa Emmanuel Okwi, upande mwingine.
Viungo wa Azam, wakaanza kukimbia huku
wakiitazama mipira ikipita kutoka upande mmoja wa uwanja hadi upande
mwingine, wakashindwa hata kujikusanya wenyewe na kutafakari nini
wanatakiwa kufanya, kila mmoja akaanza kucheza rafu pale alipoona
anazidiwa, wakaanza kupata kadi za 'manjano' na matokeo yake wakakosa
kujiamini, wakakosa mbinu mpya za
kuituliza timu na mwisho wakaaanguka wao na timu yao hadi katika nafasi
ya tatu, baada ya mchezo mmoja tu dhidi ya timu ambazo zinatawala ligi
kuu ya Tanzania Bara kwa miaka mingi. Azam, walionekana kukosa njia
mbadala na hata pale walipoamua kujaribu kujinasua katika hali hiyo,
wakajikuta wakipigwa kitanzi na Okwi, Ngassa, akawa juu kiuwezo na
kumsumbua mlinzi, Samih Nuhu.
No comments:
Post a Comment