Monday, 29 October 2012

SAFU YA ULINZI YA AZAM NA MICHEZO MIKUBWA



Wakati wakifungwa na Yanga katika michuano ya Kagame Cup, Azam walionekana kutawala sana mchezo ule wa fainali, lakini wakakwamishwa na uwezo wao mdogo wa safu ya ulinzi katika kuzuia. Matokeo yake wakafungwa kirahisi mabao 2-0. Wakarejea katika mchezo muhimu wa Ngao ya Jamii, na wakawa mbele kwa mabao 2-0, lakini, Simba, ikasawazisha na kuibuka na ushindi wa mabao 3-2. Na baada ya kucheza michezo nane pasipo kufungwa, Azam, imepewa 'onyo' kali na washambuaji wa Kimataifa wa Simba, Felix Sunzu na Okwi kuwa ni timu dhaifu katika kucheza mipira ya juu, ile ya krosi na kona inawasumbua sana walinzi wao wote, kuanzia kwa Aggrey Morris, Said Mourad hata mzoefu, Ibrahimu Shikanda, wote hawajui nani ni mchezaji hatari wa mipira ya juu katika timu pinzani na anatakiwa kuwa chini ya nani. Ni mambo ambayo yamekuwa yakiigharimu timu hii hasa katika wakati ambao wanatakiwa kuzifunga timu kubwa au ngumu ili waweze kuwa juu yao. Ni vitu ambavyo vinatakiwa kufanyiwa kazi sana na maofisa wao habari, kuchunguza kila mbinu za wachezaji wa timu pinzani hasa katika michezo muhimu. Kama huwa wanafanya basi wanashindwa kutimiza wajibu wao. Safu hii ya ulinzi imekuwa ikiwaaangusha katika kipindi muhimu zaidi ambacho kablu inahitaji kufika tangu kuanzishwa kwake.
        CHA KUJIFUNZA NA CHA KUZINGATIA BAADA YA MCHEZO
Timu zote zitaiwakilisha nchi katika michuano ya CAF, hapo mwakani, Simba watacheza michuano ya Klabu bingwa na Azam FC kwa mara ya kwanza wataingia katika soka la Afrika wakicheza michuano ya Shirikisho. Kwa mchezo wa jana ambao ni wa mwisho mkubwa kwa Simba mwaka huu, umeonesha kuwa Simba bado inahitaji nguvu zaidi katika idara ya kiungo mlinzi na ile ya beki namba tano. Anatakiwa kupatika mtu anayetambua majukumu yake hasa katika nafasi husika, tena wanatakiwa kuwa wachezaji wazoefu zaidi na si wanaokuja kujifunza soka.
Kwa upande wa Azam, wanatakiwa kuongeza ubunifu hasa wanapokuwa wamekamatwa. Azam, ni kama ilivyo kwa Barcelona, haina mbinu mbadala ya kujiepusha na 'kipigo mbele ya timu inayoingia uwanjani na kuwazima mapema kamna walivyofanya Simba hapo jana. Azam, wanakwenda katika michuano ya Kimataifa, lakini tayari wakiwa na mkusanyiko mzuri wa wachezaji, lakini bado haitoshi wanahitaji kuwa na mlinzi kama Joseph Owino katika ngome yao ili awesaidie katika kuondosha mipira ya juu. Ni lazima watafute mlinzi mmoja wa kuaminika wa kati kwa sababu hawana mlinzi yoyote ambaye anaweza kusimama na kuisogeza timu hiyo mbele kimataifa.

No comments: