Tuesday 7 October 2014

BABA ATELEKEZA MAPACHA HOSPITALINI BAADA YA MKE KUFARIKI MUDA MFUPI BAADA YA KUJIFUNGUA.






MWANAUME mmoja aliyejulikana kwa jina la Aison Majiyatamu mkazi wa Nankukwe Wilaya ya Chunya Mkoa wa Mbeya anatafutwa na uongozi wa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya kitengo cha Ustawi wa jamii kwa kutelekeza watoto wake Hospitalini.
Akizungumzia kisa hicho, Afisa Ustawi wa jamii, Hospitali ya Rufaa ya Mbeya, Annah Geretha, alisema wanalazimika kumtafuta mzazi huyo kutokana na kutoonekana Hospitali hapo kufuatilia maendeleo ya watoto wake kwa muda mrefu tangu walipozaliwa.
Alisema Mama mzazi wa watoto hao ambao ni mapacha wa kike aliyejulikanakwa jina la Edah Simia alifariki dunia muda mfupi baada ya kujifungua watoto hao salama kabisa ambapo mume aliuchukua mwili wa marehemu kwa lengo la kwenda kuzika kijijini kwao Namkukwe lakini tangu kipindi hicho hakuweza kurudi tena.
Alisema tukio hilo lilitokea Agosti 18, mwaka huu ambapo tangu kipindi hicho watoto wamekuwa wakihudumia na kuhifadhiwa kwenye chumba cha Joto katika Hospitali ya Wazazi ya Meta.
Alisema lengo la kuwatafuta ndugu wa watoto hao ni kutokana na muda wa kuendelea kukaa kwenye chumba cha joto umepitiliza kutokana na umri wao hivyo wanashindwa kuwatoa kwa sababu hawana mtu wa kuweza kuwahudumia nje ya Chumba hicho kutokana na uhaba wa wauguzi unaoikabili hospitali hiyo.
Alisema yoyote atakayekuwa na taarifa za ndugu wa marehemu ama baba wa watoto hao atao taarifa Hospitali ya Rufaa ya Mbeya au Hospitali ya Wazazi ya Mbeya kwa taratibu zingine.

No comments: