Tuesday, 21 April 2015

MAJIMBO YAPASUA KICHWA WANA-UKAWA

Mwenyekiti wa Ukawa, Profesa Ibrahim Lipumba.

HATIMA ya kuachiana kwa majimbo ya uchaguzi kwa vyama vya siasa vya upinzani vinavyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (UKAWA), inatarajiwa kujulikana wiki ijayo.
Itajulikana baada ya mkutano baina vyama washirika, uliolenga kutaka kufikiwa kwa mwafaka wa ugawanaji wa majimbo katika uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Hayo yamethibitishwa na mmoja wa viongozi wa Ukawa, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taifa wa Chama cha Wananchi (CUF), Profesa Ibrahim Lipumba.
Vyama vingine vinavyounda umoja huo ni Chadema inayoongozwa na Freeman Mbowe, NCCRMageuzi ya James Mbatia na NLD ya Dk Emmanuel Makaidi.
Alikuwa akizungumza na gazeti hili juzi mjini hapa juu ya mchakato wa makubaliano ya majimbo, ambayo baadhi yamezua mvutano ndani ya Ukawa. Kwa Lipumba, suala hilo limepangwa kumalizwa Aprili 28, mwaka huu jijini Dar es Salaam, ambapo viongozi vinavyounda umoja huo vitatu watakutana.
Aliwataja viongozi kutoka vyama hivyo, watakaohusika katika majadiliano ya kina ni pamoja na wenyeviti wa vyama, makamu wenyeviti, makatibu na wajumbe wa sekretarieti kutoka ndani ya vyama hivyo watakuja kufikia makubaliano ya mwisho.
Ukawa ulianzishwa Februari mwaka jana wakati wa Bunge Maalumu la Katiba baada ya kushikamana katika kulipinga bunge hilo la kihistoria na baadaye kususa, kabla ya kusaini makubaliano kwa ajili ya kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi zote kuanzia udiwani, ubunge na urais.
Hata hivyo, Lipumba alisema baada ya majadiliano ya muda mrefu ya viongozi wa Ukawa kuhusu Umoja wao, kulijitokeza mvutano wa kuachiana majimbo kadhaa, ambapo kila chama kilidai kinakubalika kwenye maeneo hayo na hivyo suala hilo kuachwa kulifanyiwa kazi kwa kina zaidi.
"Majimbo yote bado kufikiwa mwafaka wa pamoja na sasa tumepanga kukutana Aprili 28, mwaka huu Dar es Salaam kuweza kuweka wazi juu ya majimbo haya," alisema Profesa Lipumba.
Alisema kwa Jimbo la Morogoro Mjini pia bado maafikiano yanaendelea na kwamba moja ya sifa ni kuweka mgombea anayekubalika na wananchi wote.
Katika taarifa yake kwa umma hivi karibuni, Mkuu wa Idara ya Habari na Mawasiliano,Tumaini Makene alisema Chadema na washirika wenzake wa UKAWA, bado wanaendelea na mazungumzo ya kusimamisha mgombea mmoja kwa nafasi za udiwani, uwakilishi, ubunge na urais katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu.
Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mazungumzo bado yanaendelea vizuri, hayajafikia tamati na yakikamilika na makubaliano kufikiwa, viongozi wakuu wa UKAWA watatoa taarifa rasmi kwa umma wa Watanzania.CHANZO: HABARI LEO (Muro)

No comments: