Friday, 17 April 2015

TAMKO LA WATETEZI WA HAKI ZA BINADAMU KUMTAKA RAIS ASITIE SAIN YA SHERIA YA TAKWIMU YA 2015 NA SHERIA YA MAKOSA YA MITANDAO BILA KUFANYIWA MAREKEBISHO



Mtandao  wa Watetezi wa  Haki za Binadamu kwa kushirikiana na baadhi ya Wanachama wake, Kituao cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), SIKIKA,  Mtandao wa Jinsia-TGNP, Jamii Forum, Mtandao wa Watoa Huduma za Msaada wa Kisheria (TANLAP)   tumeshtushwa  an kusikitishwa  na kitendo cha Bunge la Jamhuri   ya Muungano  kupitisha  Mswaada wa  Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2015 na Pamoja na Sheria ya Makosa ya Mtandaoni bila kurekebisha au  kuviondoa vifungu vinavyokwenda kinyume na Katiba  ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977.

Muswada wa sheria ya makosa ya Mtandaoni unaainisha makosa yanayohusiana na matumizi ya mfumo wa kompyuta na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano, na kuweka utaratibu wa upelelezi, ukusanyaji na matumizi ya ushahidi wa kieletroniki na masuala mengine yanayohusiana na hayo.

Muswada wa Sheria ya Takwimu ya Mwaka 2013 ni  muswada wa sheria ya kufuta sheria ya Takwimu, kuanzisha Ofisi ya Taifa ya Takwimu, na Bodi ya usimamizi wa takwimu, kuweka masharti yanayohusu uratibu wa mfumo wa Kitaifa wa Takwimu, na kuweka masharti na kuipa mamlaka makubwa  Ofisi na Bodi ya Takwimu, na masharti mengine yanayohusiana na hayo.

Katika Bunge hili la 19, Serikali ilipeleka Miswaada  zaidi ya mitano chini ya Hati ya Dharura kitu ambacho katika historia ya nchi hii hakijawahi tokea. Utaratibu huu unaonyesha  ni kwa  jinsi gani viongozi wetu   ambao siku za karibuni wamegeuka kuwa watawala  na kutumia  nguvu  kubwa kutaka kuzima uhuru wa  habari, taasisi binifsi, vyuo vikuu na taasisi za utafiti na wanachi kwa ujumla   kutafuta na kutoa habari, kufanya tafiti na kutoa taarifa za kitakwimu  kwa manufaa ya umma.  Kitendo cha kupeleka miswaada hii bila kushirikisha wadau na wanachi ni dalili tosha kuwa  sheria hizi hazijatungwa kwa lengo la kulisaidia Taifa bali kuzuia mawazo huru na  mbadala yatakatokana na tafiti mbalimbali.

Mtandao kwa kushirikiana na wanachama wake tunapinga Mswaada wa Takwimu uliopitishwa na Bunge kwa kwa sababu zifuatazo:

I.            Malengo ya Sheria hii sio tu kuratibu Takwimu za Kitaifa bali umetoa madaraka Makubwa kwa Ofisi ya Taifa ya Takwimu kama Kitovu cha utoaji wa Takwimu nchini.  Maana yake ni kwamba Tasisi zote za Serikali, Mashirika  Binafsi, Taasisi za elimu ya juu, Vyuo vikuu na Taasisi za Utafiti hazitokuwa na uhuru wa kutoa matokeo ya tafiti wanazozifanya bila ya kibali au ridhaa ya Ofisi ya Takwimu.
II.            Sheria hii imezitambua taarifa na takwimu zote nchini hata kutoka taasisi binafsi kuwa  katika mfumo wa Kitaifa  wa Takwimu unaoratibiwa na Ofisi ya Takwimu. Utaratibu huu haukubaliki kabisa na ni hatari kwa mustakabali wa Taifa.

III.            Sheria hii inazitaka tasisi zote zikiwemo binafsi kuwajibika kwa Ofisi ya Takwimu na kupata ridhaa ya Mkurugenzi Mkuu wa Ofisi ya Takwimu kutoa taarifa za kitakwimu , Mfano Kifungu cha 20 (2)  kinasema takwimu zote zitakazotolewa na wakala (Kwa mujibu wa sheria hii wakala ni taasisi binafsi, mashiirika ya utafiti, wadau wa maendeleo, watumiaji au wazalishaji wengine wa Takwimu) zinapaswa kuwa zinakidhi matakwa ya Ofisi ya Takwimu na kuidhinishwa na Mkurugenzi Mkuu.

IV.            Sheria hii imeweka adhabu kali na kubwa kwa vyombo vya habari, asasi za kiraia, taasisi za utafiti na vyuo vya elimu ya juu vitakavyotenda  makosa yalianishwa katika Sehemu ya Tatu ya Sheria.  Mfano wa makosa yanayotishia shuguhuli za utafiti hapa nchini pamoja na adhamu zifuatazo;  Kifungu cha 37  cha Sheria hii kinasema mtu yoyote au tasisi itakayotoa takwimu au taarifa za kitaifiti ambazo Ofisi ya Takwimu inaziona ni za uongo anatenda kosa na kustahili kifungo cha miezi sita na faini isiyopungua million mbili. Vifungu hivi ni hatari kwa kuwa hakuna utaratibu unaoweza tambua kuwa tafiti ya tasisi fulani ni ya uongo, bali nafasi hii itatumika na Serikali na baadhi ya watawala kuminya uhuru wa taasisi binafsi kutoa taarifa mbalimbali za kitafiti zikiwemo vyuo vikuu.
V.            Sheria hii pia imelenga kuuwa uhuru wa habari kwa kuweka adhabu ya faini isiyopungua milion10 na kuifungo cha  miaka miwili.  kwa kuchapisha taarifa au takwimu za uongo au za upotoshaji.  Wakati Taifa linahubiri kuzingatia uhuru wa vyombo vya habari na haki ya kupata habari, tunashangazwa kuona serikali hiyo hiyo inazidi kuongeza sheria kandamizi dhidi ya uhuru wa habari.
VI.            Kwa ujumla sheria hii, imekuja kuzima kazi zote za kitafiti zinazofanywa na taasisi binafsi, vyuo vikuu na vyombo vya habari. Mfano tafiti zozote zinazofanywa na vyuo vikuu, taasisis za kitafiti kama  vile REPOA, ESRF, REDET, NIMRI; mashirika yasiyo ya kiserikali kama vile LHRC, TWAWEZA, HAKIELIMU, SIKIKA, HAKIARDHI na zingine nyingi  ni lazima sasa zipite chini ya usimamizi wa ofisi ya Takwimu.
VII.            Pia sheria hii ina utofouti mkubwa toka sheria iliyochapishwa kwa lugha ya Kiswahili na lugha ya Kingereza. Mfano adhabu karibu zote zilizotolewa na sheria hii zinatofitiana toka toleo la Kiswahili na la Kingereza.

WITO WETU

Kutokana na sababu hizo tajwa , sheria hii inapaswa kupingwa kwa nguvu zote na wadau wote wa wamaendeleo wakiwemo wananchi. Sheria hii inavunja haki nyingi za kikatiba na hivyo haipaswi kuingia kwenye orodha ya sheria kandamizi zilizopo sasa.  Kwa manaa hiyo  wito wetu kwa kwa makundi haya ni:

i.                    Raisi wa Jamhuri wa Muungano wa Tanzania, amekuwa akijahidi kuanzisha progamu mbalimbali za uwazi na ukweli kama vile Open Government Partneship na mengineyo. Hivyo tunamsihi sana asikubali kutia sahihi sheria hii ya Takwimu kwa kuwa inakwenda kinyume na Misingi ya Utawala Bora pamoja na vifungu vya kikatiba. Asitishe kutia saini kwenye sheria hii hadi itakapofanyiwa marekebisho ya vifungu vinavyolalamikiwa
ii.                  Wadau wote wa masula ya utafiti hapa nchini pamoja na mashirika yasiyo ya kiserikali  kuungana na nasi kwa pamoja kupinga Mswaada huu uliopitishwa bila kushirikisha wadau na wenye madhara makubwa katika sector ya utafiti nchini
iii.                Vyombo vya habari , kutumia vyombo vyao vizuri muda huu kuonyesha ubaya wa sheria hii tu siyo katika kazi za utafiti hapa chini bali hata katika uhuru wa habari nchini
iv.                Wananchi wote kama walaji na wanufaikaji wa tafiti na takwimu mbalimbali nchini kunga mkono juhudi hizi za kupinga sheria hii kandamizi
v.                  Wadau wa maendeleo nchini waungane na sisi kumshauri Rais asitie saini sheria hii kwa kuwa kazi zote wanazozifadhili za utafiti hapa nchi zitakuwa hazina chachu yoyote kwa serikali.
vi.                 Wabunge, tunawasihi  Wabunge wa Bunge Tukufu  la Jamhuri ya Muungano   kuwa na msukumo wa kuelewa miswada mbalimbali inayopitishwa ili kuepuka kutokuweza kuwawakilisha vyema wananchi wao kwa lengo la kutimiza wajibu wa dhamana waliyopewa na wananchi.
Mwisho
Pamoja na hayo sambamba na kupitishwa kwa sheria hii,  tunamshauri Mhe Rais kutafakari upya changamoto zilizoanishwa  katika sheria ya Makosa ya Mitandao ya 2015. Sheria hii kama imeletwa kwa malengo mazuri ya kupinguza matumizi mabaya ya mitandao, basi tungezani ingekuwa busara kushishirika umma wa Watanzania kabla ya kupitisha.

Sheria hii ya Mitandao itabinya kwa kiasi kikubwa uhuru wa waanchi kuwasilina na kupashana habari kama itasainiwa bila marekebisho. Ni dhahiri sheria hii imelenga kufuta kabisa matumizi ya mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Whatsup twiter n.k. Kupitishwa kwa sheria hii  bila kufanyiwa marekebisho kutasabisha watanzania wengi kuwekwa hatiani bila sababu , lakini pia kutaondoa kabisa uhuru wa habari nchini. Sheria hii imetungwa kwa uharaka kwa malengo yaliyofichika hasa kipindi hichi cha vuguvugu la uchaguzi  bila kuzingatia madhara yake kwa jamii ambayo hivi sasa inatumia kwa wingi mitandao ya kijamii kuwasiliana na kujadili mambo muhimu.

Tunawasihi watanzania wote na watumiaji wa mitandao ya kijamii kumtaka Mhe Rais asitishe kupitisha miswaada hii , bali atoe muda wa Watanzania kutoa maoni na mapungufu ya sheria hizi kwa ajili ya marekebisho.

Mtandao kwa kushirikiana na wadau wengine wa habari na utafiti hapa nchini tunaendelea kutafari zaidi ni hatu gani za kuchukua dhidi ya sheria hizi kandamizi. Tunawasihi watanzania wote na vyombo vya habari viunge mkono jitahada hizi za kupambana na sheria hizi kandamizi kabla hazijaanza kutumika.
Kwa niaba ya wanamtandao wote


Onesmo Olengurumwa

Mratibu wa Kitaifa wa Mtandao

No comments: