Thursday 23 April 2015

Wanafunzi wasomea kwenye mti Dodoma



Dodoma;
WANAFUNZI wa Shule ya Msingi Chang’ombe B, iliyopo katika Manispaa ya Dodoma, wanalazimika kusomea chini ya mti kutokana na uhaba wa vyumba vya madarasa.

Taarifa hiyo ilitolewa mjini Dodoma juzi na Mwalimu Mkuu wa Shule hiyo, Jacob Kalonga, alipokuwa akitoa taarifa kwa Ofisa Elimu, Mkoa wa Dodoma, Juma Kaponda, aliyekuwa ametembelea shuleni hapo

Kalenga alimwambia ofisa elimu huyo kwamba shule hiyo ina vyumba vitatu vya madarasa na chumba kimoja cha darasa hakijakamilika kwa kipindi cha miaka minane.

"Shule yetu ina wanafunzi 761 na idadi halisi ya vyumba vya madarasa inayohitajika ni vyumba 18 na madawati 254, lakini kwa sasa kuna madawati 60 tu.

“Kwa kuwa hatuna vyumba vya madarasa vya kutosha, wanafunzi wanalazimika kusomea chini ya mti mkubwa uliopo shuleni hapa na mti huo hutumiwa na madarasa mawili tofauti.

“Uhaba wa vyumba vya madarasa na madawati unatokana na mwamko mdogo wa wazazi wa kuchangia ujenzi wa madarasa pamoja na michango mingine wanayotakiwa kutoa,” alisema Mwalimu Kalonga.

Diwani wa Kata hiyo, Bakari Fundikira, alisema tatizo hilo ni kubwa, hivyo akataka viongozi waliotembelea shuleni hapo washirikiane kulitatua.

No comments: