Wednesday, 13 May 2015

SERUKAMBA AWASHA MOTO BUNGENI


MBUNGE wa Kigoma Mjini, Peter Serukamba (CCM), ametonesha vidonda vya ufisadi baada ya kuzungumzia ripoti ya Katibu Mkuu Kiongozi, Ombeni Sefue iliyowasafisha baadhi ya watendaji serikalini waliohusika katika kashfa ya Escrow.


Serukamba ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu, alishangazwa na taarifa hiyo kuwasafisha baadhi ya watu waliohusishwa katika kashfa hiyo na kuwaacha wengine, jambo ambalo alisema ni ubaguzi.

Kauli hiyo aliitoa  bungeni mjini Dodoma jana alipokuwa akichangia Hoja ya Bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu, Mizengo Pinda aliyoiwasilisha bungeni juzi akiomba  Sh trilioni 5 kwa mwaka wa fedha wa 2015/2016.

Katika mchango wake, Serukamba alisema ni vizuri Bunge likaitaka Serikali itangaze kuwa wote waliohusishwa katika kashfa hiyo nao ni wasafi.

Alisema haoni mantiki kwa Serikali kumsafisha Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati na Madini, Eliackim Maswi na Waziri  Profesa Sospeter Muhongo na kuwaacha wengine waliowajibika pamoja.

Serukamba alisema kwa kuwa Serikali imewasafisha viongozi hao ni wazi kuwa muamala uliofanyika wa uchotwaji wa zaidi ya Sh bilioni 200 katika akaunti ya Tegeta Escrow ni halali.

Mbunge huyo alisema ili kutenda haki kwa watu wote ni vema wanasiasa wengine waliojiuzulu nyadhifa zao na kuwajibishwa kwa Azimio la Bunge warejeshwe katika nyadhifa zao.

Waliopoteza nyadhifa zao kutokana na kashfa ya Escrow ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Profesa Sospeter Muhongo na Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka.

Wengine ni Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Jaji Frederick Werema, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Bajeti, Andrew Chenge na Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Sheria na Katiba, William Ngeleja.

“Kuhusu suala la Escrow, juzi Katibu Mkuu Kiongozi alitoa ripoti baada ya uchunguzi kufanyika ripoti ikasema katibu mkuu wake na waziri wake ni safi maana yake mwamala ule ni safi. 
 
“Kama mwamala ule ni safi, katibu ni safi waziri ni safi, Chenge anakuwaje mchafu? Tibaijuka anakuwaje mchafu? Ngeleja anakuwaje mchafu?  Mliowapeleka mahakamani wanakuwaje wachafu?  Haiwezekani tuache hizi ni style za zamani.
 
“Bunge lako linadhalilishwa watu walidanganya watu walileta document (nyaraka) feki wanatetewa, Tibaijuka tulimhukumu kwa nini?  Ina maana kwa Serikali hii kuna watu ni wazuri na wengine ni wabaya tuambieni. Nataka waziri mkuu aje atuambie usafi wa hawa watu ni nini.

“Jingine mheshimiwa spika ni suala la Tokomeza, mmefanya vizuri sana, mheshimiwa spika tuliomba ripoti ya Tokomeza hawakuleta na kama Serikali mmesema mawaziri wale ni safi naomba muwarudishe katika wizara zao.

“Kule Kenya kipindi fulani Waziri wa Fedha alituhumiwa kwamba amekula rushwa akajiuzulu, Mwai Kibaki (rais mstaafu) akaunda tume ya judicial (tume ya kimahakama) kama mlivyounda kwenye Tokomeza, ripoti ilipotoka ilionyesha kuwa Waziri wa Fedha, Amos Kimunya hana kosa lolote, rais alimteua kuwa Waziri wa Viwanda na Biashara.


No comments: