Monday 4 May 2015

Ubunge Wa Godbless Lema NJIA PANDA.....Vijana wa CHADEMA Waanza Kampeni Za Kumng'oa



SIKU chache kabla ya kuanza kampeni za Uchaguzi Mkuu wa  Rais, wabunge na madiwani, hali si shwari kwa Mbunge wa Jimbo la Arusha Mjini, Bw. Goodbless Lema (CHADEMA), kutokana na baadhi ya makada, wanachama wa chama hicho, kufanya kampeni za kutaka kumng'oa mbunge huyo.

Kampeni hizo zinadaiwa kufanywa na makada hao kimyakimya wakitumia mwamvuli wa chama kuhakikisha Bw. Lema anaanguka katika uchaguzi huo kama chama chake kitampitisha kuwania nafasi hiyo katika Uchaguzi Mkuu ujao.

Akizungumza na vyombo vya habari jana kwa niaba ya Bw. Lema, Katibu wake Bw. Inocent Kisayange, alisema kundi hilo limefanikiwa kukusanya makada wengine na kuwashawishi waungane kumkataa mbunge huyo ili asiweze kupita.

Alisema baadhi ya makada hao wamefukuzwa uanachama na wengine walijifuta wenyewe kutokana na makosa waliyofanya ambao wameungana na wenzao kutoka Arumeru Mashariki na Igunga ili kumchafua Bw. Lema aweze kukosa ubunge kwa madai mbunge huyo hajafanya lolote tangu achaguliwe.

Aliongeza kuwa, makada hao wanatumia mbinu mbalimbali kuwakusanya wananchi na kuwaambia wao ni viongozi katika sekretarieti ya chama na kumchafua mbunge huyo.

"Tumefanya uchunguzi wa kutosha na kugundua nyuma ya hawa vijana yupo kada mmoja wa CCM anayetaka kuwania
ubunge wa jimbo hili hivyo anawawezesha hawa vijana ili wafanye mikutano na kumchafua Bw. Lema," alisema.

Bw. Kisayange alisema, katika kundi hilo ambalo limejikita zaidi kufanya kampeni za kukiharibia chama hicho, limekuwa likitumia mbinu za kutaka kuwasaidia wanawake na vijana kwa kuwapa mikopo jambo ambalo si kweli.

Alisema tayari ofisi ya mbunge imeshajipanga kupambana na kundi ambalo limeamua kuasi chama kwa ajili ya maslahi binafsi na kusambaza habari za uongo dhidi ya Bw. Lema.

No comments: