Monday 18 May 2015

Wabunge walia na rushwa ofisi za umma




 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma, Celina Kombani.
KUKOSEKANA kwa Sheria ya kutenganisha biashara na uongozi ili kuweka nidhamu kwa viongozi wa umma kumesababisha kuwepo na mmomonyoko mkubwa wa maadili kwa viongozi hao, ambao wamekuwa wakitumia ofisi za umma kwa maslahi binafsi, hivyo kufanya vitendo vya rushwa kukithiri.
Wakichangia mjadala wa hotuba ya Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma bungeni jana, wabunge mbalimbali walisema ukosefu wa sheria hiyo umesababisha kuwepo kwa mianya mingi ya rushwa inayofanywa na baadhi ya watumishi wa umma.
Akichangia hoja hiyo, Mbunge wa Manyoni Mashariki, John Chiligati (CCM) alisema hivi sasa kuna mmomonyoko mkubwa wa maadili na baadhi ya viongozi wa umma hutumia ofisi za umma kwa maslahi binafsi.
“Kuna mmomonyoko mkubwa kwa viongozi wa umma, na jambo hili lilianza kwenda mrama baada ya kuruhusu viongozi wa umma kufanya biashara, rushwa nayo imeshamiri na utajiri wa ajabu kwa viongozi wetu,” alisema Chiligati.

Mapendekezo ya marekebisho ya kubadili Sheria ya kutenganisha biashara na uongozi kwa mujibu wa Sekretarieti ya Maadili, ilisema inafanya kwanza utafiti kabla ya kutoa mapendekezo ya kuibadili hatua ambayo hadi sasa bado mwafaka wake haujafikiwa.
Akizungumzia rushwa, Chiligati alisema ni jambo la kushangaza kuona kiongozi wa umma ambaye mshahara wake unajulikana, lakini mali alizonazo ni nyingi na hakuna aliyechukua hatua za kuwahoji.
“Hili la rushwa ndio baya, mnafahamu mshahara wa mtumishi wa umma, lakini mali alizonazo ni nyingi kuliko kipato chake, ana maghorofa kedekede, kwa nini hamjamhoji?” alihoji Chiligati.
Mbunge wa Tarime, Nyambari Nyangwine (CCM), alisema Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru) inabidi ipewe meno zaidi ili iweze kuyatumia kikamilifu kupambana na rushwa nchini.
Aliongeza kuwa, wala rushwa nchini ni tatizo kubwa na ndio wanaokwamisha maendeleo ya nchi kwa kujinufaisha wao, na kutaka sheria kali itungwe kuwabana na ikiwezekana, watoa rushwa na wala rushwa wauawe kwa kupigwa risasi.
“Hili la rushwa ni baya, na ni tatizo kubwa nchini itungwe sheria kali itakayowabana watoa na wala rushwa na ikiwezekana wapigwe risasi, Takukuru ipewe meno iwe na nguvu ya kuwafikisha watuhumiwa hao mahakamani na sio kusubiri kibali cha Mwendesha Mashataka wa Serikali (DPP),” alisema Nyangwine.
Aliongeza kuwa, ni vyema serikali ikapanua wigo wa kuchunguza watumishi wa umma na kwenda hadi ngazi ya wilaya, kwani wapo watumishi walioajiriwa miaka ya hivi karibuni ila wana utajiri wa kutisha.
Aidha, akizungumzia suala la tofauti kubwa ya mishahara baina ya watumishi wa umma, Nyangwine alisema Bodi ya Mishahara ilipaswa kuangalia tofauti kubwa iliyopo baina na watumishi hao, jambo linalochangia utendaji kushuka.
Alisema haiwezekani kwa watumishi wa sekta moja au taasisi moja kuwa na tofauti kubwa ya mishahara, na kutoa mfano baina ya Mkurugenzi wa Taasisi na mtumishi wa kawaida, na kusema tofauti hiyo kubwa inachangia kushusha morali ya utendaji kazi wa watumishi.
“Kuna tofauti kubwa sana baina ya mishahara ya watumishi kwenye taasisi moja, sasa hili sio zuri, bodi ya mishahara ilitakiwa ihakiki hili na kuja na njia ya kumsaidia huyo mtumishi wa kawaida, ambaye kiwango cha utendaji kazi kimeshuka kwa kukosa morali ya kazi, tofauti ya mishahara ni kubwa mno,” alisema Nyangwine.
Akisoma maoni ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Katiba, Sheria na Utawala, Mwenyekiti wa kamati hiyo, Mbunge wa Bukoba Vijijini, Jasson Rweikiza(CCM), aliishauri serikali kuipa meno Takukuru, ili iweze kushughulikia vitendo vya rushwa kwa ufasaha zaidi.
Wameshauri Takukuru iongezewa nguvu na ishirikiane na vyombo vingine vya uchunguzi kama Polisi, na usalama wa taifa ili kufanya uchunguzi wa tuhuma mbalimbali za rushwa katika vocha za pembejeo za kilimo, maliasili na uchunguzi kwenye suala la akaunti ya Tegeta Escrow.
“Uchunguzi huo ukifanywa na jopo hilo tuna imani haki itatendeka na watakaobainika walitoa rushwa au kula rushwa wafilisiwe,” alisema Rweikiza.
Akizungumzia mpango wa Kurasimisha Rasilimali na Biashara za Wanyonge Tanzania (Mkurabita), Rweikiza alisema ni vyema serikali ikahakikisha imetenga fedha za kutosha kwenye bajeti.
Kadhalika, kamati imeshauri serikali kuchukua hatua madhubuti za kuzielimisha taasisi za kibenki nchini kuhusu uhalali wa hati miliki za kimila kutumika katika dhamana ya mikopo.CHAZO HABARI LEO

No comments: