Sunday, 17 May 2015

Wanawake 140 hufariki kwa uzazi Sengerema


HATUA ya wanawake wengi kuchelewa kwenda hospitali kwa wakati pindi wanapokuwa wajawazito, imewafanya 140 kufariki kwa mwaka katika Mkoa wa Mwanza kwa uzazi huku 53 kati yao wakitoka katika Wilaya ya Sengerema mkoani hapa.

Kauli hiyo imetolewa jana na Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Dk. Ismael Sarumbo, wakati wa uzinduzi wa chumba cha upasuaji na wodi ya wazazi katika Hospitali Teule ya Wilaya ya Sengerema.

Alisema katika wilaya za Mkoa wa Mwanza, Sengerema inaongoza kwa kuwa na idadi kubwa ya vifo vinavyotokana na uzazi.

“Sehemu kubwa ya wilaya hii ni eneo la visiwa hivyo kuchelewa kuhudhuria kliniki wakati wa ujauzito kwa wanawake bado ni changamoto ambayo tunakabiliana nayo,” alisema Dk. Sarumbo.

Kwa upande wake, Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Wilaya Sengerema, Dk. Marie Jose, alisema hospitali ilikuwa ikikabiliwa na tatizo la akina mama wengi kupoteza maisha kutokana na kuwa na miundombinu isiyokidhi viwango, ambapo wagonjwa watatu walikuwa wakitumia kitanda kimoja.

Naye msimamizi wa hospitali hiyo, Joseph Massawe, alisema hospitali hiyo kwa sasa inakabiliwa na tatizo la madaktari na wameiomba Serikali kuangalia namna ya kutatua tatizo hilo.

Mmoja wa akina mama wanaotumia wodi hiyo, Catherine Deus, ameushukuru uongozi wa hospitali kwa hatua hiyo ya kuongeza wodi za wazazi na kusema itasaidia kupunguza tatizo lililokuwepo  awali la wanawake watatu kutumia kitanda kimoja.

No comments: