Sunday, 17 May 2015

Profesa Lipumba aibua mapya BVR


CHAMA cha Wananchi (CUF), kimeibua madai mapya katika zoezi la uandikishaji wa wapiga kura kwa kutumia mfumo wa kielektroniki (BVR) linaloendelea katika mikoa ya Kusini.
 
Chama hicho kilitembelea mikoa ya Ruvuma, Lindi na Mtwara na kubaini kuwa katika baadhi ya maeneo kadi ya mpiga kura inasomeka tofauti na kituo alichoandikishwa.
 
Akizungumza na waandishi wa habari  jana jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa CUF, Profesa Ibrahim Lipumba, alisema mmoja wa wapigakura alijiandikisha katika Kijiji cha Makoha Wilaya ya Newala, lakini kadi yake ilisomeka amejiandikisha Kijiji cha Nambali ‘A’  ambacho kipo umbali wa kilomita 15.
 
 “Kijiji kingine ni cha Mchemo ‘A’ Wilaya ya Newala, watu walikwenda kuandikishwa lakini kadi ikasomeka jina la kijiji kingine,” alisema Profesa Lipumba.
 
Alisema katika Kijiji cha Makoha waandikishaji walishindwa kutatua tatizo hilo na kuamua kuondoa mashine hivyo aliandikishwa mtu mmoja tu.
 
Kwa mujibu wa Profesa Lipumba, katika Kijiji cha Mchemo ‘A’ waliandikishwa watu 31 badala ya 3,059.
 
Pia alisema katika baadhi ya vijiji vya Mkohe na Engapano, mashine ziliondolewa wakati watu wengine walikuwa bado hawajaandikishwa.
 
Chama hicho kililalamikia ugawaji wa BVR kutofuata utaratibu na kusababisha vituo vyenye watu wengi kupelekewa mashine chache huku vyenye watu wachache vikipelekewa mashine nyingi.
 
Akitoa mfano, alisema katika Kijiji cha Milonde watu 2,260 walikuwa na sifa ya kuandikishwa lakini waliandikishwa 920 tu kutokana na uhaba wa mashine.
 
Aidha, alisema katika kila kituo kuna waandikishaji wawili tu wanaolipwa posho ya Sh 100,000 kila mmoja, hivyo wakichoka kunakuwa hakuna mtu wa kuwasaidia na kusababisha wafanye kazi katika mazingira magumu.
 
“Tuna wasiwasi wananchi wengi watakosa fursa ya kuandikishwa katika daftari, ni vyema NEC ikatumia siku 14 badala ya siku saba...wanataka waonekane wamefika kila mkoa lakini si watu wote watakaoandikishwa,” alisema.
 
Chama hicho kimeitaka Serikali kutenga bajeti ya kutosha ili kuhakikisha watu wote wenye sifa wanaandikishwa na kuachana na taratibu za kutaka kutumia fedha kwa mambo ambayo hayawezekani.
 
Akijibu madai hayo Mwenyekiti wa NEC, Jaji mstaafu, Damian Lubuva, alisema kama kuna mtu aliandikishwa kituo ‘A’ halafu kadi ikasomeka ameandikishwa kituo ‘B’, suala hilo litaangaliwa.
 
“Mambo mengi yanayoelezwa ni uongo kabisa...hivi sasa niko Mtwara na jana nilikuwa Masasi tumetembelea vituo vyote hakuna mtu aliyeachwa. Hivyo vikasoro vya hapa na pale sio ‘major issue’ (suala kubwa), la msingi ni kuendelea na uandikishaji,” alisema Jaji Lubuva.
 
Mwenyekiti huyo pia alivishutumu vyama vya siasa kuwa havisaidii zoezi hilo kukamilika badala yake vimekuwa vikiangalia makosa madogo yanayojitokeza.

No comments: