Wednesday, 1 July 2015

Kamati ya katiba, sheria na utawala yashauri baadhi ya ibara kwenye mswaada wa sheria zifutwe.


Kamati ya katiba, sheria na utawala imeshauri baadhi ya ibara zilizopo kwenye muswada wa sheria ya kulinda watoa taarifa za uhalifu na mashahidi zifutwe na nyingine zifanyiwe marekebisho ili ziweze kukidhi maudhui yaliyokusudiwa kwani baadhi ya tafsri zina mapungufu ikiwemo ile ya wakuu au viongozi wa taasisi za umma na binafsi kuwa na mamlaka za kupokea taarifa za kihalifu.
Makamu mwenyekiti wa kamati hiyo Mh Gosbert Blandes akiwasilisha maoni ya kamati hiyo bungeni mjini Dodoma amesema jambo hilo linaweza kuathiri utekelezaji wa sheria hiyo kwani watumishi waliopo katika taasisi hizo watakuwa na hofu ya kutoa taarifa za uhalifu dhidi ya wakuu wao wa kazi hasa pale zitakapokuwa zinawagusa.
 
Msemaji wa kambi rasmi ya upinzani bungeni katika wizara hiyo Mh Tundu Lissu akiwasilisha maoni ya kambi hiyo amesema kambi imependekeza bunge liwe na mamlaka ya kiuchunguzi katika muswada huo kama sehemu ya utekelezaji wa mamlaka yake ya kuisimamia serikali chini ya ibara ya 63 kifungu kidogo cha pili ya katiba ya nchi.
 
Akiwasilisha muswada huo bungeni waziri wa katiba na sheria Dk Asharoze Miigiro amesema vitendo vinavyoweza kutolewa taarifa kwenye mamlaka husika ni pamoja na makosa ya jinai au uvunjwaji wa sheria, vitendo vinavyoathiri afya au usalama wa mtu binafsi au jamii, ubadhilifu wa mali ya umma, matumizi mabaya ya madaraka na uharibifu wa mazingira.
 
Baadhi ya wabunge wakichangia muswada huo wametaka adhabu kwa wavujisha siri za watoa taarifa iongezwe, watoa taarifa sahihi zitakazowezesha ama kuzuia uhalifu uliokuwa ufanyike au kuokoa hasara ambayo taifa ilikuwaipate wapewe motisha pamoja na kuwapa ulinzi watoa taarifa hizo.

No comments: