Wednesday, 15 July 2015

VAN GAAL ANENA-VALDES NJE, DE GEA.....DI MARIA....!!


960Meneja wa Manchester United Louis van Gaal amesema Kipa Victor Valdes atauzwa baada ya kugoma kuidakia Timu yao ya Rizevu.
Akiongea huko Seattle, USA walikopiga kambi kabla kuanza Mechi zao 4 za Ziara huko USA, Van Gaal alisema: "Hafuati falsafa yangu. Hamna nafasi kwa Mtu kama hayo."
Valdes, Kipa wa Kimataifa wa Spain mwenye Miaka 33, hayumo kwenye Kikosi cha Wachezaji 27 ambao wako huko USA.
Valdes, aliewahi kutwaa Ubingwa wa La Liga mara 6 akiwa na Barcelona, Mwaka Jana alijiunga na Man United na kufanya Mazoezi nao kwa Miezi kadhaa baada ya Mkataba wake na Barca kumalizika wakati alipokuwa akijiuguza Goti lake aliloumia vibaya na kisha kupewa Mkataba wa Miezi 18.
Akifafanua kutokuwepo Valdes huko Marekani, Van Gaal alisema: "Mwaka Jana aligoma kuchezea Timu ya Pili na vipo vitu vingine vinahitajika ukitaka kuwa Kipa wa United. Kama hufuati msimamo huo, ipo njia moja tu na hiyo ni nje. Inasikitisha. Inahuzunisha kwa sababu tulimpa nafasi apone na awe fiti, tukampa Mkataba na sasa yuko fiti kucheza."
Valdes alicheza Mechi 3 za Timu ya Vijana ya U-21 Msimu uliopita dhidi ya Liverpool, Chelsea na Tottenham kati ya Miezi Januari na Machi.
Mechi pekee ya Timu ya Kwanza aliyochezea ni ile ya mwisho kabisa ya Msimu dhidi ya Hull City wakati Kipa Namba Moja David De Gea alipoumia.
Kuhusu David De Gea anaehusishwa na kuhamia Real Madrid, Van Gaal aliisema: "Siwezi kusema lolote. Yeye hana tatizo hapa. Ni ujinga kuuliza."
Alipoulizwa kama Angel Di Maria atabaki Old Trafford huku kukiwa na rippoti Mabingwa wa France Paris St-Germain wametoa Ofa kubwa kumnunua, Van Gaal alijibu: "Sijui lolote. Tutaona. Kwa sasa bado ni Mchezaji wa Manchester United."

No comments: