FREDERICK Sumaye, Waziri Mkuu Mstaafu ameeleza kushangazwa na Serikali ya Rais John Magufuli kupenda kusifiwa zaidi na kuchukia kukosolewa
Sumaye bila kumtaja jina Rais Magufuli ameleza kushangazwa na hatua ya serikali kuminya uhuru wa habari na kwamba, kufanya hivyo kunalenga kuficha madudu yanayofanywa na watendaji wake.
“Wapowatawala ambao hawapendi kusemwa lakini wanapenda sana kusifiwa. Kiongozi mwenye tabia ya udikteta hataki kusikia kingine zaidi ya sifa zake tu.
“Huyo ni mtu hatari na katika nchi ya namna hiyo hakuna uhuru wa habari wala uhuru wa kutoa maoni kwa woga wa kupotezwa kusikojulikana,”amesema Sumaye.
Akizungumza leo na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam katika maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari yaliyoratibiwa na Chama cha Waandishi wa Habri za Siasa (TAPOREA), Sumaye amesema, serikali inakiuka Katiba ya nchi.
Amesema, serikali yoyote inayopambana na vyombo vya habari na kuminya uhuru wa kufanya kazi zao huwa ina tatizo kwa upande wa wanaotawala.
Akitolea mfano wa hatua ya serikali kuzuia matangazo ya moja kwa moja ya bunge Sumaye amesema, kwa kufanya hivyo serikali imevunja Katiba.
“Unapoondoa matangazo ya moja kwa moja ya vipindi vya Bunge, kwanza ni kuvunja katiba. Ibara ya 18 (d) ya Katiba inasema, kila mtu ana haki ya kupewa taarifa wakati wote.
“Kwa kuzuia Bunge kuoneshwa ‘live’ (moja kwa moja) wewe serikali unataka kutoa taarifa ya Bunge kwa wakati unaoutaka na kwa taarifa unayoitaka wewe,” ameeleza Sumaye.
Kuhusu sababu iliyotolewa kwamba, matangazo hayo yanatumia gharama ya Sh. 4 bilioni amesema haina mashiko.
Sumaye amesema, hata kama matangazo hayo yatarushwa na ofisi za bunge bado, gharama zitaongezeka zaidi kwa sababu Bunge litahitaji kununua mitambo pamoja na kuajiri wafanyakazi wake.
Sumaye amesema, serikali yenye demokrasia ya kweli lazima ikubali wananchi wake kutoa maoni.
“Serikali yoyote yenye utawala bora, ingependa mambo yake inayoyafanya kwa ajili ya wananchi wake mambo hayo yajulikane kwa wananchi hao.
“Ukiona serikali inaficha mambo yake lazima kuna mambo wanayoyafanya ambayo hayafai na wasingependa jamii ijue,” amesema Sumaye.
George Maziku, Mkurugenzi Mtendaji wa TAPOREA amezungumzia ripoti ya hali ya uhuru wa waandishi wa habari na uhuru wa vyombo vya habari kimataifa, iliyotolewa na Shirika la Waandishi wa Habari Wasio na Mipaka lenye Makao Makuu yake nchini Ufaransa haipendezi.
Amesema, ripoti hiyo inaonesha kuwa, katika miaka 10 iliyopita zaidi ya waandishi wa habari 800 kutoka mataifa mabalimbali duniani wameuawa wakiwa wanatekeleza kazi zao.
“Kitisho kingine kwa uhuru wa vyombo vya habari nchini ni utamaduni mpya ulioasisiwa na kuimarishwa na watawala wa sasa na kuvishinikiza vyombo vya habari kutomkosoa Rais John Magufuli na serikali yake.
“Matokeo yake, vyombo vingi vya habari nchini vimelazimika kuandika habari za kumfurahisha Rais Magufuli,” amesema Maziku.
No comments:
Post a Comment