Monday 2 May 2016

Watahiniwa 75,000 Waanza Mtihani wa Kidato cha Sita Leo


Watahiniwa  74,920 leo wanaanza kufanya mtihani wa kuhitimu Kidato cha Sita katika shule mbalimbali nchini huku watahiniwa 11,597 wakifanya mtihani wa Ualimu.

Ofisa Habari wa Baraza la Mitihani (NECTA), John Nchimbi amesema kuwa mtihani wa kidato cha sita unaanza leo hadi Mei 19, mwaka huu. 

Nchimbi amesema kati ya watahiniwa hao waliosajiliwa, watahiniwa 65,610 ni watahiniwa wa Shule huku watahiniwa wa Kujitegemea wakiwa 9,310.

“Kati ya watahiniwa wa shule 65, 610, watahiniwa wasichana ni 24,549 na wavulana ni 41,061 huku watahiniwa wa kujitegemea wasichana wakiwa ni 3,176 na wavulana ni 6,134,” alisema Nchimbi.

Kwa upande wa mtihani wa ualimu, Nchimbi amesema kati ya watahiniwa 11,597 watakaofanya, watahiniwa 10,942 wanafanya Ualimu Daraja A na watahiniwa 654 wanafanya mtihani wa Stashahada ya Sekondari na mmoja anafanya Stashahada ya Ufundi.

“NECTA inatoa mwito kwa kamati za mitihani za mikoa, na wilaya kuhakikisha kuwa taratibu zote za mitihani zinazingatiwa ipasavyo ikiwa ni pamoja na kuhakikisha mazingira ya vituo vya mitihani yapo salama, tulivu na kuzuia mianya yote inayoweza kusababisha udanganyifu. 

“Kwa wanafunzi tunaamini walimu wamewaandaa vizuri, na ni matarajio yetu wanafunzi watafanya mitihani yao kwa kuzingatia taratibu zote za mitihani ili matokeo ya mitihani yaoneshe uwezo wao halisi kulingana na maarifa na ujuzi waliopata katika kipindi walipokuwa shule,” aliongeza Nchimbi.

Aidha, Nchimbi alitoa mwito kwa jamii kutoa ushirikiano unaotakiwa kuhakikisha mtihani unafanyika kwa amani na utulivu na kusisitiza kuwa mtu asiyehusika na mtihani asiingie kwenye eneo la mtihani.

No comments: