Monday 10 July 2017

Wananchi Mwanza Wajifungia Ndani Wakiogopa Wahalifu wa Kibiti Waliokimbilia Mwanza..........Polisi Yawatoa Hofu, Yasema Hakuna Mhalifu Atakayesalimika

SeeBait
Wakati  wakazi wa mtaa wa Fumagila Mashariki Kata ya Igoma, Mwanza wakiwa na hofu baada ya watu wawili wanaodhaniwa kuwa majambazi kukimbia juzi, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza, limesema linaendesha msako mkali kuwasaka watu hao. 
Majambazi hayo yanadaiwa kutoroka Kibiti na kukimbilia Mwanza ambapo juzi majambazi 6 yaliuawa katika mapambano na polisi yaliyodumu kwa masaa mawili.

Hata hivyo Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Ahmed Msangi ameendelea kuwatoa hofu wakazi hao kuwa hakuna jambo baya litakalotokea kwani polisi wamejipanga vya kutosha na wapo kwenye msako kila kona kuhakikisha kundi lote la uhalifu linatiwa nguvuni.

“Wakazi hao wasiwe na wasiwasi tumejipanga vya kutosha, hakuna kibaya kitakachotokea hilo kundi tumeshapata taarifa zao hivyo tutawasambaratisha wote, kikubwa wananchi waendelee kutoa taarifa na kushirikiana na polisi kwa watu wanaowatilia mashaka.” Amesema.

Katika tukio hilo polisi waliua watu sita, kukamata silaha ya SMG AK47, magazine mbili kila moja ikiwa na risasi 30, risasi 36 za AK 47 ambazo zikuwa nje ya magazine, risasi moja aina ya rafal, risasi nane za shortgun.

Silaha nyingine zilizokamatwa ni bastola nne za kienyeji, sare za jeshi za nchi jirani, kofia sita za kuziba uso, kitambaa cha kichwani, nusu kanzu, nguo mbalimbali za kiume, mabegi matatu yaliyokuwa yakihifadhi silaha hizo, baiskeli mbili, pikipiki moja, unga na dagaa.

Mwenyekiti wa mtaa huo, William Ngemela  jana alisema tukio hilo limetoa elimu tosha katika mtaa huo na mitaa jirani huku akidai tangu azaliwe hajawahi kushuhudia tukio kama hilo.

“Hii ni elimu tosha kwasababu haya yote hatukutegemea kama yanaweza kutokea kwenye mtaa kama huu, lakini angalia silaha zote na vitu vilivyokamatwa, kwakweli inatishia amani,” amesema Ngemela.

Mwenyekiti huyo alisema watu hao walikuja mtaani hapo kama waumini wa dini ya kiislamu kumbe walikuwa na mambo yao.
".... lakini hili limekuwa fundisho kwetu, ni wajibu wetu wote kushirikiana, mimi ni mwenyekiti mmoja lakini jamii ninayoingoza ni kubwa inapaswa kutoa taarifa.”

Alisema tangu lilipotokea tukio hilo juzi, baadhi ya wakazi wa eneo hilo hawakutoka nje ya nyumba zao, walijifungia wakiogopa kuwa hao waliokimbia wanaweza kurudi kufanya jambo baya.
Nyumba waliyokuwa wamejificha wahalifu hao ambapo 6 kati yao waliuawa, Wawili wakakimbia

No comments: