Baada
ya Acacia kutangaza kupunguza operesheni zake Bulyanhulu, kampuni hiyo
imeanza kuikabidhi Serikali baadhi ya mali zake kwenye Mgodi wa Buzwagi
ambao unatarajiwa kufungwa miaka mitatu ijayo.
Katika
utekelezaji wa makabidhiano hayo, jana kampuni hiyo iliikabidhi
Serikali uwanja wa ndege uliopo katika mgodi huo. Huu ni mgodi wa pili
kufungwa na kampuni hiyo baada ya ule wa Tulawaka ambao iliuuza kwa
Shirika la Taifa la Madini (Stamico) mwaka 2013.
Jana,
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga, Zainab Telack alisema hiyo ni hatua ya
awali katika mchakato wa mgodi huo kusitisha shughuli zake za uchimbaji
madini kwa mujibu wa mkataba uliopo.
“Tumeanza na uwanja wa ndege baadaye tutakabidhiwa majengo na vitu vingine kama ulivyo utaratibu,” alisema Telack.
Alisema
Desemba mwaka huu utakuwa mwisho wa shughuli za uchimbaji na baada ya
hapo wataanza kusaga mawe yaliyochimbwa kwa miaka mitatu mfululizo mpaka
2020.
Juzi,
kampuni hiyo ilitoa taarifa ikibainisha lengo lake la kupunguza
operesheni zake kwenye Mgodi wa Bulyanhulu baada ya kuzuiwa kusafirisha
mchanga wa dhahabu tangu Machi hivyo gharama za uendeshaji kuwa juu
kuliko ilivyotarajia huku mapato yakishuka.
Kwa miezi sita ya kutosafirisha mchanga huo, Acacia imedai kuwa imepoteza zaidi ya Sh583 bilioni.
Katika
utekelezaji wa mkakati wake wa kubana matumizi, kampuni hiyo inatarajia
kupunguza wafanyakazi na kandarasi mbalimbali ilizonazo. Kwa sasa, ina
wafanyakazi 1,200 na wakandarasi 800 kwenye Mgodi wa Bulyanhulu.
Taarifa
hiyo pia ilibainisha kucheleweshwa kwa leseni za wakandarasi wa
machimbo ya chini ya ardhi kwenye Mgodi wa Buzwagi jambo linaloongeza
changamoto.
Ingawa
mazungumzo baina ya Serikali na kampuni ya Barrick inayomiliki asilimia
64 ya hisa za Acacia bado yanaendelea, uamuzi wa kupunguza operesheni
kwenye mgodi huo unatarajiwa kupunguza uzalishaji kwa karati 100,000
kutoka kati ya karati 850,000 hadi 900,000 zilizokadiriwa awali.
Kwa
mujibu wa taarifa iliyotolewa Jumatatu, bei ya hisa zake kwenye Soko la
London (LSE) ilishuka kwa asilimia sita mpaka Pauni 1.94 huku kwenye
Soko la Dar es Salaam (DSE) ikishuka kutoka Sh5,940 mpaka Sh5,400 jana
mchana. Tangu kutolewa kwa zuio hilo, bei ya hisa hizo imepungua kwa
asilimia 65.
Taratibu
za kupunguza operesheni zake kwenye Mgodi wa Bulyanhulu zitakamilika
ndani ya miezi mitatu na kampuni hiyo inaamini itatengamaa kuanzia
mwakani.
No comments:
Post a Comment