Wednesday, 6 September 2017

Mahakama Yawapa Kinga Wabunge 19 wa CUF


SeeBait
Baada ya wabunge wanane wa viti maalumu wa CUF, kuvuliwa uanachama wa chama hicho na kisha kupoteza nyadhifa zao, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam imewapa kibali wabunge 19 wa majimbo wa chama hicho kuomba kuwekewa kinga.

Mahakama hiyo imetoa kibali hicho kwa wabunge hao baada ya kukubaliana na maombi yao waliyofungua mahakamani hapo dhidi Bodi ya Wadhamini wa CUF, mwenyekiti wa CUF na katibu mkuu wa chama hicho.

Katika maombi hayo namba 69 ya mwaka 2017, wabunge hao wanaowakilishwa na Wakili Mohamed Tibanyendela walikuwa wakiiomba mahakama iwaruhusu kufungua maombi kuomba kinga ili wasiguswe kutokana na mgogoro wa kiuongozi unaoendelea ndani ya chama hicho.

Wakiongozwa na Mbunge wa Temeke, Abdallah Mtolea, wabunge hao walifungua maombi hayo ya kibali cha kuomba kinga Agosti 25 na yalisikilizwa upande mmoja (waombaji pekee) Agosti 31 na kutolewa uamuzi huo juzi na Jaji Wilfred Dyansobera.

Tibanyendela alisema jana kwamba baada ya kupata kibali hicho, watafungua maombi hayo mahakamani hapo baada ya kukamilisha taratibu zote.

“Ndio nakamilishakamilisha hapa kuandaa maombi haya na baada ya hapo itabidi kwanza wateja wangu wote wasaini. Kama unavyojua kwa sasa wote wako Dodoma, bungeni, lakini tutafanya utaratibu ambao utawawezesha wote kusaini kisha tutayapeleka mahakamani,” alisema.

Katika maombi watakayofungua, wabunge hao wataomba kupewa kinga ili wasiguswe kwa namna yoyote na wajibu maombi au watu wanaofanya kazi kwa maelekezo yao, ili kutokuathiri haki na masilahi yao.

Pia, wabunge hao wataiomba Mahakama iwalazimishe wajibu maombi hao kumaliza tofauti zao kwa mujibu wa katiba ya chama na sheria za nchi.

Wabunge hao wa majimbo wamestuka na kuchukua hatua hizo baada ya wenzao wanane kupoteza nyadhifa zao kutokana na uamuzi wa chama hicho upande wa Profesa Ibrahim Lipumba anayetambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa kuwavua uanachama.

Chama hicho kimekuwa katika mgogoro wa kiuongozi kwa muda mrefu tangu Profesa Lipumba alipotangaza kujiuzulu mwaka 2015 na baadaye kubatilisha uamuzi wake huo mwaka jana.

Kurejea kwake kwa kuandika barua ya kutengua ile ya kujiuzulu, kulisabisha kuibuka kwa makundi mawili ya wanachama wa chama hicho, moja likiongozwa na Katibu Mkuu, Maalim Seif Sharif Hamad linalompinga na jingine linalomuunga mkono.

Katika mwendelezo wa mgogoro huo, kambi inayoongozwa na Profesa Lipumba ilitangaza kuwahoji na kuwachukulia hatua wanachama na viongozi mbalimbali wakiwamo wabunge kwa tuhuma mbalimbali zikiwamo kukihujumu chama kwa kushirikiana na vyama vingine.

Kundi la kwanza kuitwa kwa ajili ya kuhojiwa na Baraza Kuu la Uongozi ni wabunge hao wa viti maalumu ambao wako kambi ya Maalim Seif.

Wabunge hao wanane ni Severina Mwijage, Saumu Heri Sakala, Salma Mohamed Mwassa, Riziki Shahari Ngwali, Raisa Abdallah Mussa, Miza Bakari Haji, Hadija Salum Al-Qassmy na Halima Ali Mohamed ambao hata hivyo, hawakuitikia wito huo na matokeo yake walivuliwa uanachama na kupoteza ubunge.

Wabunge 19 wa majimbo ambao pia wako kambi ya Maalim Seif,  kwa mujibu wa taarifa hiyo lilikuwa ni kundi la pili kuitwa kuhojiwa na kisha kufuatiwa na kundi la tatu ambalo ni viongozi wa ngazi za juu.

No comments: