Mbunge
wa Kigoma Mjini Zitto Ruyagwa Kabwe jana amefikishwa kwenye Kamati ya
Haki, Maadili na Madaraka ya Bunge, kama ilivyotakiwa na Spika wa Bunge
Job Ndugai, kujibu tuhuma za kutoa kauli za kulidhalilisha bunge.
Kwenye Kamati hiyo ambayo alifikishwa chini ya ulinzi wa Polisi, Mbunge Zitto Kabwe amekiri kwamba kauli hiyo ni kweli aliitoa na kueleza haya.....
Uhuru Wangu wa Maoni Ulilenga Kulinda Uhuru, Haki, Hadhi na Heshima ya Bunge
Mheshimiwa Mwenyekiti wa Kamati,
Mnano
tarehe 13 Septemba, 2017 nilipata wito wa kufika mbele ya Kamati yako
kutoa ushahidi wa masuala mbalimbali. Nilipata wito husika saa nane na
dakika 40 mchana, nikitakiwa kufika mbele ya kamati yako, hapa Dodoma
saa saba mchana siku hiyo hiyo.
Nililetewa
wito huo na RCO Mkoa wa Kigoma nikiwa kwenye kikao cha Baraza la
Madiwani la Manispaa ya Kigoma Ujiji. Sikuweza kufika, isingewezekana
katika mazingira hayo niwe na uwezo wa kusafiri kutoka Kigoma na kufika
mbele ya kamati yako hapa Dodoma. Kwanza muda ulishapita, lakini hata
taratibu za kiusafiri pamoja na umbali kati ya Kigoma na Dodoma
hazikuwezesha Jambo hilo.
Siku
iliyofuata nilipata ajali, ambapo nyumba yangu iliwaka moto wakati
nikiwa njiani kwenda Nairobi kumuona mbunge mwenzetu mgonjwa, ndugu
Tundu Lissu. Jana tarehe Septemba 20, 2017 nikiwa natokea Kigoma ili
kuja kwenye Kamati nilikamatwa na Polisi ili kufikishwa mbele ya Kamati
yako.
Leo nimefika mbele yenu na nitajibu wito wenu kama ifuatavyo:
A:
Kwamba maoni yangu kwenye mtandao wa Twitter kuwa "Bunge siku hizi ni
Idara ya Tawi la Utawala" yanadhalilisha Mhimili Wa Bunge.
Maneno
hayo ni ya kwangu na nimeyatoa kama raia wa Tanzania. Ninaamini kwa
dhati kuwa Bunge la Kumi na Moja limekuwa likifanya kazi kwa kuingiliwa
na Serikali chini ya ndugu Rais John Pombe Magufuli.
Maneno
na vitendo vya Rais yanaashiria kuwa Bunge halina Uhuru wake, na mimi
kama Mbunge nina wajibu wa kuonyesha kutopendezwa kwangu na hali hiyo.
Nina mifano kumi (10) kuthibitisha maelezo yangu hayo kama ifuatavyo:
- 1. Kuzuiwa kwa "Bunge Live" kwa kisingizio cha kupunguza gharama za uendeshaji wa mhimili wa Bunge, wakati Mikutano yote ya mhimili wa Serikali, hasa ya Rais ikirushwa live (mubashara) ni dalili ya wazi ya kufifisha sauti ya Bunge na kupandisha sauti ya serikali. Hata vituo binafsi ambavyo vilipanga kurusha bunge Live bila malipo (na hivyo kutokuwa na gharama) vilizuiwa, lakini vinarusha Live mikutano ya Rais.
- Kitendo cha Uongozi wa Bunge kurudisha serikalini shilingi Bilioni 6 bila ridhaa ya wabunge kwa kisingizio kwamba zimebaki kutokana na kubana matumizi. Hii ni dalili ya wazi ya Bunge "kujipendekeza" kwa serikali. Wakati Uongozi wa Bunge ukirejesha kiwango hicho cha Fedha, kuna taarifa kwamba kamati nyingi za Bunge zinashindwa kutekeleza wajibu wake kwa sababu ya ukata.
- Maelekezo ya mhimili wa Serikali kwa mhimili wa Bunge, kupitia maagizo ya Rais Magufuli kwa Spika Ndugai kuwa "Awashughulikie wabunge" (kwa kuwafukuza bungeni) aliowaita "waropokaji" ili waje wazungumze nje ya Bunge na yeye Rais (Serikali) apate nafasi ya kuwashughulikia. Kauli hii ya Rais aliyoitoa wakati akipokea Ripoti ya Prof. Osoro kuhusu Mikataba ya Madini, Juni 12, 2017 inaonyesha picha iliyo dhahiri kuwa Bunge linapokea Maelekezo kutoka Serikalini ya kuwadhibiti wabunge hasa wanaoiwajibisha serikali. Na hatuwahi kuliona Bunge likiyakana maelekezo hayo ya Rais kwa Spika.
- Kitendo cha Bunge kuhariri hotuba za kambi ya upinzani kwa kushinikiza kuondolewa kwa vipengele vinavyoikosoa Serikali. Mathalani, Wakati wa Bunge la Bajeti, hotuba ya Msemaji wa Kambi ya upinzani wa Wizara ya Mambo ya Ndani, ndugu Godbless Lema, iliamriwa kuondolewa maneno yanayohusu kashfa ya Mkataba wa Lugumi, kumhusisha Rais na kuuzwa kwa nyumba za Serikali, Mauaji ya wanasiasa, pamoja na Bunge kulinda wahalifu.
- Kauli ya Rais Magufuli ya Novemba 4, 2016 akizungumza na wahariri wa vyombo vya habari kuwa "mzizi wa mhimili wa serikali ni mrefu zaidi kuliko mihimili mingine" mara baada ya kuulizwa juu ya matumizi ya Serikali Nje ya Bajeti iliyoidhinishwa na bunge, unaonyesha dhahiri fikra ya Rais na Serikali yake juu ya ukuu wa mhimili wa Serikali dhidi ya Bunge.
- Kitendo cha Ripoti ya Kamati ya Bunge ya Tanzanite na Almasi kusomwa nje ya Bunge na kuwasilishwa kwa Waziri Mkuu na Rais bila kuwasilishwa na kujadiliwa Bungeni ili kuwekewa azimio la Bunge. Kitendo hiki kinaifanya Kamati hiyo kuonekana kuwa ya Serikali badala ya Kamati ya Bunge.
- Kauli ya Rais kuwa Spika alimpigia simu kumuuliza juu wajumbe wa kuwaweka kwenye Kamati za Bunge za Tanzanite na Almasi inaonyesha dhahiri kuwa Spika anafanya kazi kwa maelekezo ya Rais. Na Bunge na Spika hawajawahi kuikana kauli hii ya Rais.
- Kwa mara ya kwanza kwenye Historia ya Nchi yetu tumeshuhudia Mbunge akishambuliwa kwa risasi wakati Mkutano wa Bunge ukiwa unaendelea. Haijapata kutokea katika historia ya Bunge letu, Wabunge kukamatwa hovyo mbele ya mageti ya Bunge na kusafirishwa usiku usiku bila hata Spika kujulishwa kama taratibu za Mabunge ya Jumuiya ya Madola zinavyotaka. Kitendo cha 'Watu Wasiojulikana' kummiminia risasi zaidi ya thelathini Mbunge wa Singida Mashariki, ndugu Tundu Lissu, wakati akitokea Bungeni, tena kwenye makazi yake, ambayo kwa mujibu wa sheria ni sehemu ya Bunge, ni dharau ya hali ya juu kwa Mhimili huu. Ni tukio linalolenga kuliziba mdomo Bunge. Makala yangu ya Nani alitaka kumwua Tundu Lissu (kwa lugha ya Kiingereza) naiambatanisha katika maelezo yangu haya.
- Kitendo cha Serikali kutowasilisha 'Taarifa za Utendaji wa Robo Mwaka' kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti kama inavyotakiwa kwa mujibu wa Sheria ya Bajeti ya mwaka 2014 ni dharau kubwa kwa Mhimili wa Bunge. Ni dharau zaidi kwamba Serikali ilileta Muswada wa sheria kuondoa kifungu kinacholazimisha Waziri wa Fedha kutoa Taarifa hizo, na Bunge kupitisha kuwa Sheria, hivyo kuondoa kabisa Uwajibikaji wa kibajeti wa Serikali ndani ya Bunge, hivyo kudunisha hadhi ya bunge.
- .Bajeti ya Bunge kutowekwa kwenye Mfuko wa Bunge kwa mujibu wa sheria, na Spika kutakiwa kuomba vibali vya safari za Wabunge kwa Mkuu wa Tawi la Utendaji (Serikali) ni maelezo tosha kuwa Bunge ni Tawi la Utendaji na sio Mhimili unaojitegemea.
Ninayo mifano mingine mingi tu ya kuonyesha kama ushahidi wa jambo hili, kwa sasa hiyo 10 naomba itoshe.
Kwa
mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, nchi yetu ina
mihimili mikuu mitatu ya dola ambayo ni Serikali, Bunge na Mahakama.
Katiba na Sheria mbalimbali za nchi zimewekwa kuhakikisha kila mhimili
unafanya kazi kwa uhuru bila kuingiliwa na mhimili mwingine. Kikatiba,
mbali na wajibu wake wa kutunga sheria, Bunge lina wajibu wa kuisimamia
serikali. Kwa lugha nyingine, katika utekelezaji wa majukumu yake, Bunge
ni "Kiranja" wa kuibana na kuisimamia Serikali.
Tangu
kuingia madarakani kwa serikali ya awamu ya tano, kumekuwepo na kauli
na matendo ya viongozi wa serikali na Bunge yanayoashiria uelekeo wa
serikali kuminya na kuingilia uhuru wa Bunge. Baadhi ya vitendo hivi
vimefanywa hata na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania. Kwa kutambua
wajibu wangu katika kulinda heshima, uhuru, hadhi, haki, ufanisi na
madaraka ya Bunge katika kutekeleza majukumu yake, mara kadhaa
nimekumbusha na ilipobidi kuonya ndani na nje ya Bunge dhidi ya vitendo
hivi.
Maoni
yangu yaliyonifanya niitwe hapa, pamoja na Mifano kumi (10) niliyoitoa
hapo juu vinaonyesha wazi nia yangu njema ya kuonya na kutaka kulindwa
kwa hadhi, heshima, haki na madaraka ya Bunge letu tukufu. Naamini bunge
lilipaswa kunipongeza ni kunishajiisha kwa kazi hiyo, na si kinyume
chake ninapotuhumiwa na kuletwa mbele ya Kamati yako kuwa
nimelidhalilisha bunge pamoja na spika wa bunge. Jambo hili litavunja
morali ya wabunge kutetea hadhi ya bunge letu.
Mheshimiwa Mwenyekiti (Mzee George Huruma Mkuchika),
Wewe
ni miongoni mwa wazee ninaowaheshimu sana hapa nchini, nilivyo sasa kwa
kiasi kikubwa ni sehemu ya malezi yako kwangu hapa bungeni, umeshiriki
kunifinyanga niwe mbunge imara kwa busara na hekima zako, pamoja na
kunipa ujasiri wa kuisimamia kutokana na uzoefu wako. Nakutambua kama
muumini wa Siasa ya Ujamaa na Kujitegemea, iliyotangazwa kupitia Azimio
la Arusha. Napenda ninukuu sehemu ya Azimio la Arusha kuhusu Uhuru wa
mawazo. Azimio linasema "kwamba TANU inaamini: kila Raia wa Tanzania ana
haki ya Uhuru wa Mawazo..."
Napenda
kusisitiza kuwa kama Mtanzania ninao Uhuru wa Mawazo na Maoni, hiyo ni
kwa mujibu wa Katiba yetu, Ibara ya 18. Kitendo cha mimi kuitwa mbele ya
Kamati yako kwa maoni yangu haya, naamini ni mwendelezo wa kufinywa kwa
haki na uhuru wa mawazo na maoni ya raia.
Mimi
kama mtanzania ninaruhusiwa kuwa na maoni yangu, na pia nina haki ya
kutoa maoni yangu hayo. Kunituhumu kwa maoni yangu binafsi kuwa
yanavunja heshima, hadhi, haki na mamlaka ya bunge, na kuwa maoni yangu
hayo ni kulidhalilisha Bunge na Spika si sahihi kabisa, ni uonevu dhidi
yangu, ni ukiukwaji wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, ni
kinyume na Haki za Binadamu, hasa kwa kuwa mifano hiyo 10 niliyoitoa
imeonyesha usahihi wa maoni yangu hayo.
Maoni
yangu yalilenga kulinda hadhi, haki, heshima na madaraka ya bunge letu
tukufu. Ni maoni yaliyolenga kulinda heshima ya spika, ili azitumie
nguvu alizonazo kwa mujibu wa Katiba na Kanuni za Bunge kulinda heshima
na hadhi ya Bunge isiporomoke, ni maoni yaliyolenga kuonyesha imani
niliyokuwa nayo juu yake (Spika), ni maoni yaliyolenga kulizindua Bunge
juu ya hali ya kukosa mshawasha/msisimko ambao Watanzania wameuzoea.
Tafsiri
kuwa maneno yangu kuwa Spika hajafikia viwango vya Maspika
waliotangulia kabla yake kuwa ni kumdharau si sahihi. Maoni yangu
hayakulenga kuonyesha dharau, bali yalilenga kutaka Bunge liyalinde yale
mambo mazuri yaliyosimikwa na Maspika hao wa nyuma katika kuisimamia
Serikali.
Jambo
hili (la kutaka kuendelezwa na kulindwa kwa mambo mazuri ya maspika wa
nyuma yaliyoimarisha hadhi ya Bunge) ni ahadi ya Spika wetu, ndugu
Ndugai, wakati wa kikao maalum cha Bunge cha msiba wa Spika wa Bunge la
9, ndugu Samuel John Sitta. Hivyo ni dhahiri, mimi kukumbushia ahadi
hiyo ya Spika mwenyewe haiwezi kwa namna yoyote ile kuwa ni kudhalilisha
Bunge na kumdhalilisha Spika, bali kitendo cha kuitwa hapa mbele ya
kamati yako kwa maoni yangu binafsi nje ya bunge, maoni yaliyolenga tu
kukumbushia ahadi husika, hakika kinalidhalilisha Bunge na Spika wa
Bunge
Kuona
mawazo huru haya yangu kuwa ni kudhalilisha Bunge si sawa. Ni kinyume
kabisa na misingi ya TANU iliyoasisi Utaifa wetu, ni kinyume na
Utanzania wetu. Wananchi wangapi wataletwa mbele ya Kamati yako kuhojiwa
kwa kutoa maoni yao juu ya hadhi ya mhimili wa Bunge?
Imani
yangu ni kuwa, Hadhi, Heshima, Haki na Madaraka ya Bunge haitotokana na
kuhoji wanaotoa maoni juu ya mwenendo wa bunge, kutumia maguvu ya Jeshi
la Polisi, wala vitisho vya Kiongozi wa Mhimili wetu huu dhidi ya
wabunge, bali ni mwenendo wake wa kuisimamia Serikali mbele ya umma ndio
utakaojenga hadhi, heshima, haki na madaraka ya Bunge kwa wananchi.
Mheshimiwa Mwenyekiti
Iwapo
Bunge litaendelea kuwa 'paraded ' Ikulu kila wakati na kupewa maelekezo
na wakati mwengine kusimangwa na Serikali, kupitia Rais, umma utaona
sio Bunge lao bali ni Tawi tu la Serikali, na kamati yako itakuwa na
kazi ya kuita maelefu ya Watanzania.
Nawashukuru sana kwa kunisikiliza.
Naomba Kuwasilisha.
Kabwe Zuberi Ruyagwa Zitto
Mbunge, Kigoma Mjini - ACT Wazalendo
Dodoma
Septemba 21, 2017
No comments:
Post a Comment