Saturday 16 September 2017

Serikali Yaapa Kupambana na Wanaojihusisha na Mapenzi ya Jinsi Moja


SeeBait
Serikali imesema inapambana kwa nguvu zote na vitendo vya mapenzi ya jinsi moja na kwamba, mwanamume atakayethibitika kufanya vitendo vya kike ataadhibiwa kisheria.

Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk Hamisi Kigwangalla alisema hayo jana Ijumaa alipojibu swali la Mbunge wa Viti Maalumu (Chadema), Susan Lyimo.

Mbunge huyo alisema kumekuwa na biashara kati ya wanaume na wanawake lakini pia ipo ya watu wa jinsi moja. “Nataka kufahamu hao wanachukuliwa hatua gani?” alihoji Lyimo.

Naibu waziri alisema sheria inakataza watu wa jinsi moja kufanya mapenzi  kinyume cha maumbile na pia inakataza wanaume kufanya vitendo vya jinsi ya kike.

Alisema kuna adhabu kali hutolewa na sheria hiyo kwa mtu anayebainika kufanya vitendo hivyo na kwamba, adhabu yake ni kifungo cha hadi zaidi ya miaka 30 jela.

“Tumekuwa tukipambana kwa nguvu zetu zote na makundi haya ambayo yamekuwa yakishiriki katika vitendo vya mapenzi ya jinsi moja, kuyahamasisha ama kuyahalalisha  au kuyafanya kuonekana kama ni vitu vya kawaida katika nchi yetu,” alisema.

Dk Kigwangalla alisema wamefanikiwa kwa kiasi kikubwa kwa kufanya operesheni nchi nzima. Amesema taasisi mbalimbali ambazo zilikuwa na mwelekeo wa kutekeleza afua za kinga katika sekta ya afya wamezifuta na kuzibadilisha.

Katika swali la msingi, Mbunge wa Geita Mjini (CCM), Costantine Kanyasu alihoji kazi ya kuwakamata wanawake wanaojiuza imefanikiwa kwa kiasi gani nchini.

Dk Kigwangalla alisema tatizo hilo ni kubwa katika mikoa ya Dar es Salaam, Mwanza, Arusha, Mbeya na Dodoma.

“Kitendo cha mwanamke kuishi akitegemea kipato chake au sehemu ya kipato chake kutokana na ukahaba ni kosa la kisheria,” alisema.

Naibu waziri alisema katika kutekeleza sheria ipasavyo, viongozi katika mikoa ukiwemo Mkoa wa Dar es Salaam wamekuwa wakikamatwa na kuchukuliwa hatua kwa mujibu wa sheria ya wanawake wanaojiuza.

Alisema Wizara ya Afya kwa kushirikiana na Ofisi ya Rais Tamisemi na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi wataendelea kuhakikisha wanawake wanaojihusisha na biashara hiyo wanaendelea kukamatwa ili kulinda heshima, utu na hadhi ya wanawake wa Tanzania.

No comments: