Baraza
la vijana CHADEMA (BAVICHA) limepinga kauli alizotoa Kamishna Kanda
maalumu ya Dar es salaam, Lazaro Mambosasa kuhusu maombi yao kitaifa
kumuombea Mbunge Tundu Lissu na kusema wao hawajapanga kuandamana bali
watafanya maombi kumuombe Lissu.
Akiongea
jana na waandishi wa habari Katibu Mkuu (BAVICHA) Taifa, Julius Mwita
alisema kuwa wameshangazwa na kusikitishwa na kauli kadhaa alizozitoa
Mambosasa kuhusu maombi yao na kusema ametafsiri ndivyo sivyo kauli zao
kwani wao hawajapanga kufanya maandamano.
"Tumeshangazwa
na kusikitishwa na kauli kadhaa alizozitoa Mambosasa akionesha kuwa
amezuia maombi hayo kwa sababu alizodai kuwa yatakuwa ni maandamano na
kinyume cha taratibu. Tungependa kusema shughuli yetu ya Jumapili
haijapangwa kuhusisha wala haitahusisha maandamano yoyote kama ambavyo
SACP Mambosasa ametafsiri. "
Julius
Mwita aliendelea kuweka wazi kwamba wameamua kukutana kwenye uwanja huo
ili kutoa nafasi kwa watu wa imani zote kuweza kukutana na kufanya sala
na dua kwa pamoja.
"Tumesema
wazi katika taarifa yetu kwa jeshi hilo wilayani Kinondoni, kuwa
shughuli ambayo tumeiandaa inahusu maombi ambayo yatahusisha watu wa
imani za dini mbalimbali ambao kimsingi hawawezi kukutana ndani ya
nyumba moja ya ibada lakini wote hao wanaweza kukutana sehemu moja,
mahali pa wazi na kuomba dua/ sala kwa utulivu pamoja" alisema Julius Mwita
Mwita
amesema wao wanaendelea na maandalizi ya shughuli hiyo kama kawaida kwa
kuwa waanamini hakuna utaratibu wala sheria ambayo wamevunja na kumtaka
Mambosasa aipokee hiyo barua ya maombi yao kisha aitafakari na
kulinganisha na kauli zake alizozitoa leo mbele ya waandishi wa habari.
"Tunaelewa
sheria na taratibu za nchi zinazosimamia mikusanyiko mbalimbali
haziwapatii Polisi mamlaka yoyote ya kuzuia mikusanyiko au kutoa kibali
cha mikusanyiko, bali sheria na taratibu hizo zimeelekeza wahusika wa
shughuli hiyo kutoa taarifa Polisi na kueleza siku, mahali, muda na
wahusika wa mkusanyiko husika."
Mwita aliendelea kutoa ufafanuzi juu ya jambo hilo na kudai
"Baada
ya kusikia kauli ya SACP Mambosasa, tunatoa wito kama ifuatavyo
tunamsihi SACP Mambosasa apate nakala ya barua yetu ya taarifa kuhusu
shughuli hiyo ambayo tumepeleka mamlaka za kipolisi kama sheria
inavyoelekeza, ili aweze kutafakari uzito wa shughuli hiyo ya maombi ya
Kitaifa ya Vijana kisha alinganishe na kauli zake alizotoa leo" alisema Mwita
Mbali
na hilo Katibu Mkuu wa (BAVICHA) Julius Mwita alisema wao wanaendelea
na maandalizi na kuwataka watu wenye mapenzi mema na taifa na ambao
wameguswa na tukio la kinyama na kikatili la kupigwa risasi kwa Mbunge
wa Singida Mashariki Tundu Lissu kuhakikisha wanafika Jumapili Sinza
Darajani katika uwanja wa TP kwa ajili ya maombezi hayo na kusema jambo
hilo si la kisiasa kama ambavyo Mambosasa amekuwa akisema.
No comments:
Post a Comment