Wednesday, 13 September 2017


SeeBait
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mh. Job Ndugai, amesema ana uwezo wa kumzuia Mbunge wa Kigoma Mjini Zitto Kabwe kuzungumza mpaka mwisho wa bunge, kwani hawezi kupambana naye.

Spika Ndugai ametoa kauli hiyo Bungeni ambapo amesema Zitto Kabwe hawezi na hapaswi kujibizana naye, na kumtaka Zitto Kabwe kutomfananisha na aliyekuwa Spika wa Bunge marehemu Samuel Sitta, kwani hawezi kufanana naye na kila mtu ana muda wake, kama ambavyo Spika wa bunge aliyepita mama Anna Makinda alivyokuwa na muda wake kuliongoza bunge hilo.
"Hawa ni watu nawaheshimu sana na wamenilea sana na ni  sehemu nilipofika hapa leo. Utanilinganishaje mimi na milima mikubwa kama Kilimanjaro? Hata siku moja sikio haliwezi kuzidi sikio," amesema.

Amesema katika Bunge la 9 Zitto aliwahi kupeleka hoja ya Mgodi wa Buzwagi ambayo ilikataliwa na Bunge lakini ikazuka hoja ya kimaadili ambapo alihukumiwa hapo hapo.

"Alihukumiwa hapo hapo akapigwa miezi mitatu. Mnataka niende mkuku mkuku kama lile la Bunge la tisa nifanane na mzee Sitta? Hilo pia naliweza kwa nini mnaalika matatizo nashangaa unapambana na Spika," amesema.

"Ninauwezo wa kupiga marufuku kuzungumza hadi miaka yote mitano iishe hauna pa kwenda, hakuna cha swali, nyongeza wala kuzungumza utanifanya nini?

Amemtaka kupambana na mtu mwingine lakini sio yeye.

"Kwa haya ya Spika sina sababu nayo lakini ya kulidharau Bunge hayo sitaweza kuyavumilia nitalinda mihimili huu kwa nguvu zangu zote," amesema.

Amesema hawawezi kuacha wabunge kulidhalilisha Bunge na kuhoji kwamba watachukuliaje Watanzania wengine watakapolidhalilisha Bunge.

Amesema hilo kosa la pili kwa Zitto na kuagiza liende katika kamati ya maadili.

"Tutaenda sambamba mguu kwa mguu hadi kieleweke," amesema

Hapo jana Spika Ndugai alimtaka Zitto Kabwe kufika kwenye kamati ya maadili kutoa maelezo juu ya taarifa alizoziweka kwenye mtandao, na Zitto Kabwe kumjibu kuwa mambo anayoyafanya Spika yanaporomosha bunge

No comments: